Jumatano, 13 Sha'aban 1446 | 2025/02/12
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Uhamishaji wa Watu wa Gaza

(Imetafsiriwa)

Swali:

Al Jazeera ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo tarehe 26/1/2025: “Rais wa Marekani Donald Trump alisema kwamba anaishinikiza Jordan, Misri na nchi nyingine za Kiarabu kupokea wakimbizi zaidi wa Kipalestina kutoka Gaza, baada ya vita vya Israel dhidi ya Ukanda huo kusababisha mgogoro wa kibinadamu. Alipoulizwa ikiwa hili lilikuwa pendekezo la muda au la muda mrefu, Trump alisema, “Inaweza kuwa hili au lile.”

Je, hii haimaanishi kuwa Trump anawaweka watawala wa Jordan na Misri katika duara la aibu, hasa kwa vile walishasema awali kwamba hawakukubali uhamishaji huu? Je, hii ina maana kwamba Trump anapanga kuuondoa Ukanda wa Gaza na watu wake ili kuunganisha na umbile la Kiyahudi, hasa kwa kuwa watawala wa Kiarabu, na kwa hakika watawala wote wa Waislamu wamenyamaza kimya mithili ya makaburi bila kusonga mbele kumkabili? Je, hii ina maana kwamba kuna mabadiliko katika sera ya Marekani au ni ile ile lakini kwa mtindo tofauti?

Jibu:

Ili kufafanua majibu ya maswali ya hapo juu, tutahakiki mambo yafuatayo:

1- Trump hafichi malengo yake, bali anayasema waziwazi, tofauti na mtangulizi wake Biden. Kwa mfano, Biden alikuwa akiwahadaa watu kwamba Marekani inajitahidi kutekeleza mradi wa dola mbili, lakini yalikuwa ni maneno tu yasiyo na maana! Al Jazeera ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo tarehe 4/1/2024: “Rais wa Marekani Joe Biden alisema jana, Ijumaa, kwamba kuna miundo kadhaa ya suluhisho la dola mbili, akionyesha kwamba nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa hazina vikosi vyao vya kijeshi...” (Al Jazeera 4/1/2024) yaani, Biden anakusudia serikali ya aina hiyo isiyo na jeshi! Hata hivyo, Trump alitaja ukweli wa lengo lake bila kuwahadaa watu. Alisema wakati wa kampeni yake ya uchaguzi, akisema: “Unapotazama ramani, ramani ya Mashariki ya Kati, ‘Israel’ ni sehemu ndogo ikilinganishwa na ardhi hizi kubwa. Kwa hakika nilisema: ‘Je, kuna njia yoyote ya kupata zaidi?’” (Sky News 19/8/2024), akimaanisha kwamba anataka kupanua umbile la Kiyahudi kwa uhalali wa makaazi katika Ukingo wa Magharibi na kuwapa uhuru wa kunyakua ardhi na kuanzisha makaazi mapya juu yake.

2- Hili linathibitishwa na uteuzi wake wa mtu ambaye ana maoni kama yake kama Balozi wa Marekani katika umbile la Kiyahudi, yaani Mike Huckabee, ambaye Trump alimuelezea kwenye akaunti yake ya Ukweli wa Kijamii mnamo tarehe 13/11/2024 kama “Mwenye kuipenda 'Israel' na watu wa 'Israel', na vile vile watu wa 'Israel' wanampenda, na Mike atafanya kazi bila kuchoka kuleta amani Mashariki ya Kati.” Miongoni mwa matamshi ya hapo awali ya Mike Huckabee ni yale ambayo BBC ilichapisha mnamo tarehe 13/11/2024, ikinukuu Chaneli 12 ya Kiyahudi, kwamba Huckabee anajulikana kwa kauli zake za kuunga mkono umbile la Kiyahudi, ikiwa ni pamoja na kauli alizozitoa mwaka 2015 ambapo alisema: “Uhusiano wa kihistoria wa Israel na eneo hilo, uliodumu kwa maelfu ya miaka, uko imara zaidi kuliko uhusiano wa kihistoria wa miaka 400 wa Amerika na Manhattan.” Ana video kwenye mitandao ya kijamii alizochapisha mwaka 2017 ambapo alisema, “Hakuna kitu kama Ukingo wa Magharibi, ni Judea na Samaria, hakuna kitu kama makaazi, ni jamii, ni vitongoji, ni miji, hakuna kitu kama ukaliaji kimabavu.”

3- Balozi huyu alirudia kauli zake kwa Chaneli 7 ya Kiyahudi mnamo tarehe 15/11/2024, akisema: “Siwezi kusema kitu ambacho sikiamini. Kamwe sikutaka kutumia neno Ukingo wa Magharibi. Hakuna kitu kama hicho. Ninazungumza juu ya Judea na Samaria. Ninawaambia watu hakuna ukaliaji kimabavu.” Alisema: “Kumbuka kwamba katika kipindi cha miaka minne ambayo Trump alikuwa rais, hakukuwa na rais aliyeiunga mkono Israel zaidi yake katika historia. Kila kitu kuanzia kuitambua Jerusalem kama mji mkuu hadi kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem na kuitambua Milima ya Golan kama mali halali ya Dola la 'Israel', na pia kutojaribu kuendeleza suluhisho la dola mbili lisiloweza kutekelezeka, kwa sababu halitekelezeki na haliwezi kutekelezwa.” Alisema: “Siamini kwamba suluhisho la dola mbili ni halali. Huu ni msimamo ambao nimeushikilia kwa miaka mingi, na ni msimamo ambao Trump anakubaliana nao, na ninatarajia utaendelea.” Kupitia matamshi haya, vipengele vya sera ya Trump kuhusu kadhia ya Palestina vinadhihirika, ni kuhalalisha uvamizi katika Ukingo wa Magharibi na makaazi ya walowezi.

4- Hii ina maana kwamba utawala wa Trump hauna mradi maalum mpya kwa kadhia ya Palestina, kuunda dola kwa ajili yao, bila kujali ukubwa wake. Lakini badala yake mambo yanaelekea kwenye utambuzi rasmi wa Marekani wa umbile la Kiyahudi kupitia uhalali wa makaazi katika Ukingo wa Magharibi, kama inavyoonyeshwa na kauli za balozi wa Marekani katika umbile la Kiyahudi, na kauli yake kwamba Trump anamuunga mkono katika hili. Trump alimsifu, ambapo ina maana kwamba alimsifu kwa mawazo yake kuhusu suala hili. Hii inathibitishwa na Trump kuondoa vikwazo kwa walowezi wa Kiyahudi ambao walifanya ukiukaji ambao Amerika iliona kuwa haramu wakati wa utawala wa Biden. Amani ambayo Trump anamaanisha ni kulikubali umbile la Kiyahudi kwenye ardhi iliyonyakua katika Ukingo wa Magharibi na kujenga makaazi juu yake, huku ikiipa Mamlaka ya Palestina haki ya kubaki na baadhi ya uhuru hivi sasa ili iweze kuendelea kutumikia umbile la Kiyahudi chini ya jina la uratibu wa usalama, na kuwachosha watu kwa kukusanya ushuru kutoka kwao, kuwalisha watu wa Mamlaka ya Palestina wakitoa baadhi ya huduma za manispaa.

5- Trump alijaribu kuonyesha uwezo wake wa kufikia anachotaka na kwamba ana uwezo wa kufanya amani ili kuwahadaa watawala wa eneo hilo na kuwapa matumaini kwani shetani huwapa matumaini wafuasi wake. Al Jazeera iliripoti mnamo tarehe 23/1/2025: “Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa utawala wake ulifanya mambo mengi zaidi ndani ya siku 4 kuliko utawala wa Rais wa zamani Joe Biden ulivyotimiza katika miaka 4, akisisitiza kwamba kama si utawala wake, makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yasingekamilika wiki hii. Pia alitaja kwamba Ufalme wa Saudi Arabia utawekeza dolari bilioni 600 nchini Marekani, lakini ataiomba ifikishe dolari trilioni moja. Walakini, Trump aliambatanisha “mfuko wa zawadi” kwa makubaliano haya kwa umbile la Kiyahudi, kama gazeti la Kiyahudi Yedioth Ahronoth liliripoti mnamo 14/1/2025: “‘Israel’ itakuwa na haki ya kukomesha usitishaji vita ikiwa itaona ni muhimu, na Ikulu ya White House itatoa uzito wake nyuma ya kufuta vikwazo vilivyowekwa hapo awali na utawala wa Biden kwa baadhi ya walowezi waliotekeleza vitendo vya kihalifu, na itaanzisha kampeni ya kimataifa dhidi ya mahakama mbili za Umoja wa Mataifa zilizoanzisha uchunguzi au mashtaka dhidi ya Israel, hasa dhidi ya Netanyahu na waziri wake wa ulinzi Galant kwa mashtaka ya kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.”

6- Kwa hivyo, Trump, katika muhula wake wa kwanza na wa sasa, ametabanni maslahi ya Kiyahudi, hata maazimio ya kimataifa ambayo yaliwekwa na Marekani na nchi nyingine kubwa, Marekani ilikuwa inazifuata nchi zilizokiuka maazimio hayo. Trump amehujumu maazimio haya yanayopinga maslahi ya Mayahudi. Amehujumu maazimio ya Umoja wa Mataifa ambayo yanauchukulia Ukingo wa Magharibi kuwa ardhi inayokaliwa kwa mabavu ambapo umbile la Kiyahudi halina haki ya kuishi, bali ni lazima liondoke humo hadi kwenye mipaka ya Juni 4, 1967. Pia amehujumu maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Jerusalem Mashariki kama ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, pamoja na maazimio yake kuhusu Milima ya Golan kama ardhi inayokalia kwa mabavu ya Syria, na ametambua uhalali wa uamuzi wa umbile la Kiyahudi kuziunganisha nalo Jerusalem (al-Quds) na Milima ya Golan. Hili linathibitisha kwamba atatambua uhalali wa makaazi hayo na yale ambayo Mayahudi wameyateka hadi sasa katika Ukingo wa Magharibi na kuruhusu makaazi zaidi kuanzishwa au kupanuliwa. Hili limeanza huku akiwasamehe walowezi ambao walikuwa chini ya vikwazo wakati wa muhula wa Biden.

7- Trump ataendelea na mpango wake wa kulimakinisha umbile la Kiyahudi kwa kuzifanya nchi zingine katika eneo hilo kuinuka na kuhalalisha mahusiano na umbile hili ili kutambua uhalali wake na unyakuzi wake wa Palestina. Miongoni mwa nchi zilizopendekezwa kwa hili ni Saudi Arabia, haswa kwa vile uhusiano wa Mfalme Mtarajiwa wa Saudia ni mkubwa na Trump, ambaye anafuatilia kwa dhati uhalalishaji mahusiano wa umbile hilo na Saudi Arabia. Hili linaweza lisicheleweshwe, kwani kufuata kikamilifu kwa utawala wa Saudi na kile utawala wa Republican unaoongozwa na Trump unataka kunaeleweka na kila mtu mwenye macho na ufahamu. Trump alitangaza mnamo tarehe 23/1/2025 kwamba “Saudi Arabia itawekeza dolari bilioni 600 katika uchumi wa Marekani, na nitaomba kuongeza hadi dolari trilioni.” (Al-Hurra America, 23/1/2025), na alisema kwamba hili lilifanyika kupitia maongezi ya simu na Mfalme Mtarajiwa wa Saudia, Bin Salman, jioni ya Jumatano 22/1/2025. Yaani, kwa simu moja tu, mtawala mkuu wa Saudi Arabia mara moja alitii ombi la rais wa Amerika la kuunga mkono uchumi wa Amerika kwa mamia ya mabilioni ya dolari. Hii inaonyesha kiwango cha utayari wa serikali ya Saudi kutii maombi ya Amerika wakati wa muhula wa Trump. Kwa hiyo, kwa simu nyingine tu, Bin Salman atatangaza utayarifu wake wa kuhalalisha mahusiano na umbile la Kiyahudi atakapotakiwa kufanya hivyo.

8- Kwa hiyo, yeyote anayetafakari hatua za Trump katika kuunga mkono umbile la Kiyahudi atapata kauli ya Trump imejumuishwa katika swali kuhusu kuondoa Ukanda wa Gaza kutokana na watu wake na kuuunganisha kwa Mayahudi, hasa alipoulizwa ikiwa hili lilikuwa pendekezo la muda mfupi au la muda mrefu, Trump alisema, “Inaweza kuwa hili au lile” (Al Jazeera 26/1/202), yeyote anayetafakari hili ataliona kuwa ni jambo la kawaida kwa Trump. Ama kuhusu yale yaliyosemwa katika swali: “Je, hii haimaanishi kwamba Trump anawaweka watawala wa Jordan na Misri katika duara la aibu, hasa kwa vile walishatangulia kusema kwamba hawakukubali uhamishaji huu?” Trump hajali kuhusu wao, iwe wanakosa hewa au la, haswa kwa vile hapo awali alitoa kauli iliyo wazi zaidi kuliko kauli hii, hapo awali alisema: “Unapoangalia ramani, ramani ya Mashariki ya Kati, ‘Israel’ ni sehemu ndogo sana ikilinganishwa na ardhi hizi kubwa. Kwa kweli niliuliza: ‘Je, kuna njia yoyote ya kupata zaidi?’” (Sky News 19/8/2024). Kauli yake ya awali ilikuwa juu ya kupanua umbile, na kauli yake ya sasa ni kauli ya mojawapo ya njia za kupanua umbile hilo, na inaonekana kwamba Trump anataka kuandaa mazingira kwa ajili ya watawala vibaraka kuendelea na uhamishaji huu wa lazima ambao watawala walikuwa wameukataa hapo awali, hasa nchini Misri na Jordan. Kwa maana nyengine, ni mchakato wa “kuyajaribu maji” ili kuona kama watawala hawa wanaweza kuwashinikiza watu kutekeleza kauli ya Trump na kuwaondoa katika nchi zao, kuwaondoa katika nchi zao, kuwaunganisha na Mayahudi, au kuakhirisha hili hadi wakati mwingine ambao Trump ataona kuwa unafaa ikiwa watu watasimama dhidi ya tawala mbili na kuwazuia na hatua hii, ambayo ni khiyana kwa Mwenyezi Mungu, Mtume wake na waumini.

9- Tunatambua kwamba watawala katika nchi za Kiislamu, hasa zinazoizunguka Palestina, hawaoni haya mbele ya Mwenyezi Mungu, Mtume wake, na waumini, na kutekeleza amri ya Trump ni moja ya vipaumbele vyao. Hili liko wazi kutokana na harakati zao za kumpongeza Trump kwa ushindi wake katika uchaguzi na urais wake wa Marekani, ingawa hakuficha uaminifu wake kwa Mayahudi na uadui wake kwa Uislamu na Waislamu. Walakini, watawala hawa walishindana kumpongeza:

a- RT - Arab World News - 6/11/2024, ilichapishwa: Ikinukuu shirika la habari la Saudi SPA, pongezi za mfalme wa Saudi kwa Trump ambaye alisifu “uhusiano tofauti wa karibu wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili marafiki na watu, ambao kila mtu anataka kuimarisha na kuendeleza katika nyanja zote.” Pia ilichapisha pongezi za rais wa Uturuki kupitia jukwaa la X: “Ninampongeza rafiki yangu Donald Trump ambaye alishinda uchaguzi wa rais…tunatumai kuwa uhusiano wa Uturuki na Marekani utaimarishwa.”

b- Al Jazeera ilichapisha mnamo tarehe 6/11/2024 pongezi za Rais wa Misri: “Ninatoa pongezi zangu za dhati kwa Rais Mteule wa Marekani Donald J. Trump ... na kukuza ushirikiano wa kimkakati kati ya Misri na Marekani na watu wao… kuendeleza maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili marafiki.” Na kutoka kwa Mfalme wa Jordan, “Pongezi za dhati kwa Rais Donald Trump kwa kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani.” Ninatarajia kufanya kazi nanyi tena ili kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu wa Jordan na Marekani...” Pia kutoka kwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwenye tovuti ya X, “Hongera kwa Rais Mteule Donald Trump kwa ushindi wake wa kihistoria kwa muhula wa pili.”

c- Hata Ahmad al-Sharaa, mkuu wa utawala mpya nchini Syria, alifuata njia hiyo hiyo na akachapisha kwenye Facebook mnamo tarehe 20/1/2025: “Kwa niaba ya uongozi na watu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria, nampongeza Donald Trump kama Rais wa Marekani.” Alisema, “Tuna imani kuwa yeye ndiye kiongozi wa kuleta amani Mashariki ya Kati na kuregesha utulivu katika eneo hili.”

Hawa ndio watawala wa nchi za Waislamu. Mwenyezi Mungu awalaani wamedanganya kiasi gani.

10- Hata hivyo, tunatambua pia kwamba Umma wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) pamoja na watu wake waaminifu na wanyoofu, utazifanya kauli za Trump na wafuasi wake kutoka kwa watawala hao, kuwa vumbi lililotawanyika. Kushikamana kwa watu wa Palestina, ardhi iliyobarikiwa, ni jambo linalojulikana sana katika nchi yao. Yeyote aliyewatazama wakitembea kwa maelfu kwa miguu yao, katika hali ngumu ya hewa na hata hali ngumu zaidi ya ardhini, wakiharakisha kwenda kwenye nyumba zao, ambazo wanajua zimevunjwa na uvamizi wa kikatili wa Mayahudi, lakini kwao wanachukulia kuzifikia kuwa ni ushindi mkubwa. Yeyote aliyeyaona yote hayo na kuyatafakari anatambua kwamba kauli za Trump na njama zake za kuiondoa Palestina watu wake, hata kama zitachanganywa na njama za watiifu wake kutoka kwa watawala wa Ruwaibidha (wajinga wazembe), yote hayo yatawarudia wao:

﴿وَقَدْ مَكَرُوا مَكْرَهُمْ وَعِنْدَ اللهِ مَكْرُهُمْ وَإِنْ كَانَ مَكْرُهُمْ لِتَزُولَ مِنْهُ الْجِبَالُ

“Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao anavijua Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.” [Ibrahim: 46]. Kisha Ardhi iliyobarikiwa itaregea kwa watu wake, nyumba ya Uislamu. Watawala wote hawa Ruwaibidha watatoweka, na dola ya Kiislamu, Khilafah Rashida, itaregea, Mwenyezi Mungu akipenda. Kupigana na Mayahudi na kuondoa uvamizi wao kutatokea, Mwenyezi Mungu akipenda. Amesema Sadiq al-Musadaq (Mkweli, Mwaminifu) (saw) katika Musnad ya Ahmad kutoka kwa Hudhayfah: « ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ... » “Kisha itakuweko Khilafah kwa Njia ya Utume” Al-Bukhari pia amepokea kutoka kwa Abdullah bin Omar, Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili, ambaye amesema: Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) akisema: «تُقَاتِلُكُمْ الْيَهُودُ فَتُسَلَّطُونَ عَلَيْهِمْ...» “Mayahudi watapigana nanyi na nyinyi mtawashinda” Muslim pia ameipokewa kwa maneno ya Ibn Umar, kutoka kwa Mtume (saw) ambaye amesema: «لَتُقَاتِلُنَّ الْيَهُودَ فَلَتَقْتُلُنَّهُمْ...» “Mtapigana na Mayahudi na mtawauwa...” Kisha ardhi itang’aa kwa ushindi wa Mwenyezi Mungu, Al-Qawi Al-Aziz.

11- Lakini kama tulivyotangulia kusema, na tunarudia katika hitimisho hili:

“Hata hivyo, sheria ya Mwenyezi Mungu ilitaka asiteremshe Malaika kutoka mbinguni ili watusimamishie Khilafah kupigana na adui yetu huku sisi tukiwa tumekaa.

Bali, Yeye huwateremsha Malaika Wake kuwa ni wenye kutilia nguvu na kutoa bishara njema ya Nusrah (ushindi) kwa watu wanaomuamini Mola wao Mlezi, na akawazidishia uwongofu, wanajeshi wa Kiislamu, wenye subira katika vita, wanaolindwa na kiongozi wao na wanaopigana na maadui zao nyuma yake:

﴿بَلَى إِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُمْ مِنْ فَوْرِهِمْ هَذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُمْ بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ

“Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu.” [Aali-Imran: 125]. Hapo tutakuwa miongoni mwa wanaostahiki bishara njema:

﴿نَصْرٌ مِنَ اللهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

“… Nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!” [As-Saf: 13].”

28 Rajab 1446 H

28/1/2025 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu