Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa Pamoja na Wale Waliohusika na Mauwaji ya Halaiki ya Assad Dhidi ya Raia

(Imetafsiriwa)

Mnamo Julai 27, shirika la Amnesty lilichapisha makala inayoeleza kuwa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Syria unafanyakazi moja kwa moja na kundi la – Umoja wa Kitaifa wa Wanafunzi wa Syria (NUSS) – ambalo linatuhumiwa kwa kuusaidia utawala wa Assad katika mauwaji yake ya halaiki dhidi ya wasio na hatia wanaopinga utawala wake nchini humo. Ujumbe wa karibuni wa Facebook wa UNDP Syria umetaja ushirikiano wake na NUSS katika kuandaa mashindano ya uvumbuzi, Zawadi ya Hult, kwenye kampasi za Vyuo Vikuu vya Syria. NUSS kwa kipindi kirefu imefahamika kuungana kwake na utawala wa mauwaji wa Syria na kufanyakazi na idara za usalama za Syria kukandamiza sauti za wanafunzi dhidi ya Mchinjaji Assad. Kwa kweli, NUSS imewajibika kwa ukamataji, mateso ya kinyama, mauwaji na kupotezwa kwa wanafunzi wengi wa Chuo Kikuu cha Syria waliopinga utawala wa Syria au walioshiriki katika maandamano ya amani mwaka 2011. Limekuwa likiitwa, “shirika kubwa zaidi la usalama na ujasusi katika vyuo vikuu na mabaraza ya elimu ya Syria” na pia limewaajiri wanafunzi wa vyuo vikuu vya Syria kuwa kama watoaji habari dhidi ya wanafunzi wanaodhaniwa kutokuwa watiifu kwa utawala. Makala ya Amnesty imeelezea kuwa NUSS pia ina vyumba vya mateso na mahojiano ndani ya Chuo Kikuu cha Damascus.

Kuhusika kwa UN pamoja na watu binafsi, wafanya biashara na taasisi zenye kuunganishwa kwa karibu na utawala wa Assad, pamoja na kufanikisha uovu wa mchinjaji huyu kupitia matendo yao na sera nchini Syria kumenakiliwa vyema. Msaada wa kibinaadamu wa UN kwa mfano, umesaidia kuuweka sawa utawala na kugharamia uovu wake. Kwa mujibu wa mtandao foreignaffairs.com, mashirika ya UN kama Shirika la Afya Duniani limemruhusu Assad kudhibiti pauni bilioni 30 za msaada wa  kibinaadamu wa kimataifa kwenye mzozo wa nchi hiyo kuzitumia kwa ufanisi kusaidia vita vyake dhidi ya wasio na hatia na kutumia uzuiaji wa misaada na kusimamia usambazaji wake kama silaha ya kivita. Mnamo 2016, zaidi ya watoaji huduma za kibinaadamu 50, makundi ya haki za binaadamu na ya kiraia yaliunga mkono ripoti ambayo inaeleza kuwa UN iliridhia kutotaka kusaidia maeneo yalioshikiliwa na wapinzani nchini Syria, hali iliyopelekea vifo vya maelfu ya raia. Zaidi ya hayo, uchunguzi wa shirika la habari la Uingereza la Guardian ambao pia ulichapishwa mnamo 2016, uligundua kuwa UN ilipeana kandarasi zenye thamani ya makumi ya mamilioni ya dolari kwa watu walio na ushirikiano wa karibu na raisi wa Syria kama sehemu ya mpango wa msaada, zikiwemo dolari milioni 4 kwa msambazaji wa serikali wa mafuta na dolari milioni 8.5 kwa shirika lililoanzishwa na kuongozwa na mke wa Assad Dkt. Reinoud Leenders, mtaalamu katika masomo ya kivita katika Chuo cha King’s College jijini London, ameeleza kuwa mashirika ya UN yamelipa “kandarasi za uagizaji zenye faida kubwa ya mauzo kwa marafiki wa utawala wa Syria wanaojulikana kusaidia kifedha ukandamizaji na ukatili ambao unasababisha mengi ya mahitaji ya kibinaadamu”.

Ni uwazi unaoonekana kuwa Umoja wa Mataifa si tu ni taasisi tiifu, ikitazama umwagikaji damu nchini Syria, Palestina, Myanmar, Kashmir na biladi nyenginezo yakifanyika machoni mwake bila ya utashi wa kisiasa kumaliza maovu haya dhidi ya ubinaadamu kwa matendo yafaayo badala ya maneno matupu…, lakini sera zake na matendo pia yamesaidia na kuchochea uonevu, mauwaji au kuchinja wasio na hatia. Mwaka uliopita, mwanasheria wa haki za binaadamu anayelifanyia kazi Baraza la Haki za Binaadamu la UN (UNHCR), ameeleza kuwa wakuu katika UNHCR walishiriki kikamilifu kuwapatia majina ya Wauyghur walio wapinzani wa utawala wa China kwa ajili ya kujipendekeza na kuendeleza mahusiano ya karibu ya kisiasa na utawala huo wa kidikteta, licha ya China kufuata sera ya mauwaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa Uyghur wa Turkistan Mashariki. Taarifa hizi baadaye zilitumiwa na utawala huo kuwahangaisha, kuwakamata, kuwafunga na kuwatesa wanafamilia wa wapinzani katika kambi mbaya za mateso kuwanyamazisha wanaharakati wa Uyghur kutokana na kuzungumzia juu ya sera zilizo dhidi ya Waislamu za Chama cha Kikomunisti katika eneo hilo. Mnamo 2018, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) yalitia saini makubaliano na serikali ya Myanmar juu ya hatua za mwanzo za kuwarejesha wakimbizi 700,000 wa Rohingya waliokimbia vurugu za kikatili za wanajeshi na kuelekea Bangladesh – wameshirikiana na wachinjaji wa Burma kuwarejesha Warohingya mikononi mwa wauwaji wao na kwa wale waliotekeleza maovu yasiosemeka dhidi yao. Na mnamo miaka ya tisiini, sera za UN ziliupa nguvu mkono waa Waserbia dhidi ya Waislamu katika Vita vya Bosnia, na shirika hilo lilikula njama za mauwaji ya Srebrenica mwaka 1995 ambapo Waislamu 8000 wanaume na wavulana waliuawa kinyama.

UN ni shirika ambalo halina ilichokitoa isipokuwa matumaini na ahadi za uwongo kwa wanaodhulumiwa na kuwepesisha maovu ya madikteta na tawala na serikali za mauwaji. Linatumika pia kama ubabaishaji na ukengeushaji mkuu katika kutatua majanga ya kibinaadamu ya dunia, linaendesha mapatano ya amani yasiokwisha ambayo hayaongozi kokote. Kwa kweli, limekuwa ni bingwa wa kubeba jukumu la hila la ‘wawekaji amani’, wakati kiuhalisia ni kuwa linasimamia uimarishaji wa nguvu za wavamizi na madhalimu kupitia ‘mikataba yao ya amani’, na kurefusha mashaka ya wanaodhulumiwa. Hili halishangazi kwa kuwa UN imekusudiwa muda wote kutumikia maslahi ya sera za kigeni za mataifa matano makuu yenye nguvu na wanachama wa kudumu wa baraza lake la usalama, hasa kwa Amerika.

Huu ni ukumbusho wa wazi kwa Waislamu kuwa hatuwezi kutegemea vyombo vya kigeni kutatua matatizo yetu au kuhifadhi damu zetu, ardhi na heshima, kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyosema:

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَتَّخِذُواْ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاء مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ أَتُرِيدُونَ أَن تَجْعَلُواْ لِلّهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا مُّبِينًا]

“Enyi mlioamini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio marafiki badala ya Waumini. Je mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyo wazi juu yenu?” [An-Nisa: 144]. Na amesema (swt):

[مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِنْ دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاءَ كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنْكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ]

“Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.” [Al-Ankabut: 41].

Tukiwa Waislamu, lazima tuyaweke mambo yetu mikononi mwetu wenyewe na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu na uhifadhi wa damu zetu kutoka kwenye Dini yetu – Uislamu – pekee, kwani kwa chengine chochote huwa ni kurefusha tu maafa ya ndugu zetu wanaodhulumiwa waume na wake kote duniani. Na Dini yetu imeainisha wazi na dhahiri kuwa ni kwa kusimamisha uongozi wa Uislamu pekee, Khilafah kwa njia ya Utume, ambayo ndio njia pekee ya kuhifadhi maisha ya Waislamu dunia kote, kuzikomboa ardhi zetu kutoka kwa madhalimu, madikteta na wavamizi, kuihifadhi Dini yetu kutokana na uingiliaji na mashambulizi ya maadui zake na kuhakikisha usalama na amani katika ardhi zetu. Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

[وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُم فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَى لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ]

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya Makhalifah katika ardhi kama alivyowafanya Makhalifah wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.” [An-Nur: 55].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Dkt. Nazreen Nawaz

Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu