Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali

Amerika na Mabadiliko katika Mawakala wake nchini Pakistan

(Imetafsiriwa)

Swali:

Al Jazeera English iliripoti mnamo tarehe 28/04/2022 kwamba, “Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amemteua Bilawal Bhutto-Zardari, mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani Benazir Bhutto, kama waziri wa mambo ya nje... Akiwa na umri wa miaka 33 tu, Bhutto-Zardari anakuwa mmoja wa mawaziri wa mambo ya nje wenye umri mdogo zaidi duniani... Sharif alitangaza baraza la mawaziri la watu 41 baada ya kuchukua nafasi ya waziri mkuu aliyeondolewa Imran Khan mapema mwezi huu......” Serikali ya Shebaz Sharif, ambaye alimrithi kaka yake Nawaz kama rais wa PML-N, aliapishwa mnamo tarehe 19/4/2022, yaani zaidi ya wiki moja baada ya kuondolewa kwa Imran Khan.

Swali ni nini kilisababisha mabadiliko haya? Kumbuka kuwa Bunge kwa kuungwa mkono na jeshi lilimpa imani Imran wakati anateuliwa, huku jeshi likiwa na hasira na pande mbili za PML-N na PPP wakati huo. Kwa hiyo nini kimetokea tangu hapo? Je, Marekani ina mchango katika suala hilo, ikijua kwamba imekuwa nyuma ya utawala wa Pakistan kwa miaka mingi?

Jibu:

Ili kufafanua majibu ya maswali haya, tunahakiki yafuatayo:

Kwanza, Je, Imran Khan alifikiaje utawala?

1- Jeshi ndilo lililompa Imran Khan madaraka. Imran Khan aliendesha serikali ambayo haikuwa na kifani kuhusiana na majenerali. Amelaumiwa kwa kuwa karibu sana na jeshi tangu alipoahidi kuunda "Pakistan Mpya," kuondoa ufisadi na upendeleo, baada ya kushinda uchaguzi wa 2018. Hadi hivi majuzi, Imran Khan alielezewa kama mmoja wa washirika wa karibu wa jeshi la Pakistan, kati ya wakuu wa serikali. Imran alishutumiwa hata kuwa chini ya jeshi.

Lau isingekuwa msaada wa jeshi kwake, Imran Khan asingepata imani yoyote ya kutawala! Mnamo 1996, alitangaza kuunda chama chake cha kisiasa cha Pakistan Tehreek e Insaf (PTI). Mnamo 1997, Imran Khan alishindwa kushinda hata kiti kimoja katika Bunge la Kitaifa wakati wa uchaguzi mkuu. Ilikuwa ni mwaka wa 2013 tu ambapo chama chake kiliweza kuleta athari katika siasa za Pakistan, kutokana na kuungwa mkono na Jeshi la Pakistan. Chama chake kilifanikiwa kushinda viti 30 katika Bunge la Kitaifa. Kilikuwa chama cha tatu kwa ukubwa cha upinzani, baada ya Pakistan Muslim League-Nawaz na Pakistan People's Party. Jeshi lilichagua kumpa Khan nafasi ya kushinda uchaguzi wa 2018. Hata hivyo, hiyo ilikuwa ni baada ya Imran Khan kukubaliana na Mkuu wa Majeshi, Qamar Bajwa, kuendesha uchaguzi mkuu.

2- Jeshi, pamoja na ujasusi chini ya uongozi wa Luteni Jenerali Faiz Hameed, walifanya kazi bila kuchoka kuboresha matarajio ya kisiasa ya Khan. ISI ilisaidia kupanga mikusanyiko yake kote nchini, na kumfanya kuwa mgombea aliyeshinda. Huku wakitishia wanahabari kuhusu kutoa utangazaji mzuri wa PML-N, huduma za usalama zilishambulia PML-N, kuwakamata, kuwaweka kizuizini na kuwanyanyasa wafanyakazi wa PML-N - mrengo wa Nawaz. Wanajeshi pia walifanya kazi nyuma ya pazia kuwanyima wagombea wa PML-N kugombea...

3- Ingawa chama cha Imran Khan kilishinda viti 149 katika Bunge la Kitaifa, bado kilikuwa chini ya viti 172 vinavyohitajika kuunda serikali ya wengi. Walakini, iliweza kufanya hivyo katika mfumo wa serikali ya mseto, kwa mpangilio wa jeshi. Serikali ya mseto ilikuwa ni mpango wa Jeshi la Pakistan kuhakikisha kuna njia ya kurudi nyuma, ikiwa Imran Khan atabadilisha mawazo yake na kuchukua hatua dhidi ya jeshi. Ujasusi pia ulifanikiwa kuwashawishi wanachama wa Pakistan People's Party katika serikali ya Imran Khan. Kwa hivyo, jumla ya wanachama 17 wa timu ya Imran Khan waliteuliwa chini ya ushawishi wa ISI. Ni wajumbe watatu pekee wa baraza la mawaziri ndio waliokuwa wafuasi wa PTI ambao hawakuwahi kuwa katika chama chengine chochote hapo awali!

Pili: Baada ya Imran Khan kuwa Waziri Mkuu, alitoa huduma nyingi kwa Amerika,

1- Idhaa ya TV ya Geo News ya Pakistan iliripoti kuhusiana na Khan kwamba, "Alipokea barua kutoka kwa Rais Trump wa Marekani mapema leo 3/12/2018, ambapo aliiomba Pakistan kuchukua nafasi katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan na kusaidia kuleta harakati ya Taliban katika meza ya mazungumzo,” kama ilivyoripotiwa kimataifa na Sputnik ya Urusi mnamo tarehe 3/12/2018. Kisha Imran Khan alikutana siku mbili baadaye na Mjumbe Maalum wa Marekani Khalilzad mjini Islamabad, akithibitisha maendeleo ya Pakistan kuhusiana na mpango wa Marekani kwa Afghanistan!

2- Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Asif, alithibitisha usaliti wa watawala wa Pakistan, wakati yeye ni mmoja wao. Katika mfululizo wa nukuu za tweets, Khwaja Asif alisema mnamo 3/1/2018, "Umeuliza tulifanya nini? Dikteta amesalimu amri kwa simu moja, nchi yetu ilishuhudia umwagaji damu mbaya zaidi, ulifanya mashambulizi 57,800 dhidi ya Afghanistan kutoka kwa vituo vyetu, majeshi yako yalipewa silaha na vilipuzi kupitia ardhi yetu, maelfu ya raia na askari wetu wakawa wahanga wa vita vilivyoanzishwa na wewe... Tulimwona adui yako kuwa ni wetu, tuliijaza Ghuba ya Guantanamo, tulikutumikia kwa shauku kubwa kiasi kwamba tuliiacha nchi yetu na shehena ya mizigo na uhaba wa gesi. Tulijaribu kukufurahisha kwa gharama ya uchumi wetu, tulitoa makumi ya maelfu ya visa kama matokeo ambayo mitandao ya Black Water ilienea katika nchi yetu. Hakuna jambo lililo wazi zaidi kuliko hili: Pakistan ilipigana vita ambavyo havikuwa vita vyake... Ilimwaga damu ya watoto wa Kiislamu kwa ajili ya Marekani... Na ilifuja maadili ya Dini yake ya Kiislamu, ili kutumikia maslahi ya Marekani…

3- Kadhalika kuhusu India, kama alivyoshindwa hapo awali, Imran alinyamaza kuhusu unyakuzi wa India wa Kashmir, isipokuwa kwa misimamo ya kupiga domo tupu. Kwa hivyo tulisema katika swali na jibu la 8/8/2019, "Wakati India ilipotangaza uamuzi wake wa hivi karibuni wa kubatilisha hadhi maalum ya Kashmir, msimamo wa Pakistan pia ulikuwa wa kuvunja moyo, haukupita zaidi ya kulaaniwa pekee, ili kuondoa lawama. Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilitoa taarifa ikisema, ‘Pakistan inalaani vikali na kukataa matangazo yaliyotolewa leo (Jumatatu 5/8/2019) na New Delhi. Hakuna hatua ya upande mmoja ya Serikali ya India inayoweza kubadilisha hali hii yenye mzozo, kama ilivyoainishwa katika maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), Pakistan itatumia machaguo yote yanayowezekana ili kukabiliana na hatua hizo zisizo halali.' (AFP 5/8/2019)... Kwa maana nyengine, mithili ya Mamlaka [ya Palestina] ya Abbas na nchi za Kiarabu zinazowazunguka, wanashutumu na kupinga ukiukaji wa umbile la Kiyahudi wa Ardhi Tukufu ya Palestina bila kuhamasisha majeshi kupigana. Pakistan inarudia dori lile lile na kushutumu bila ya kuhamisha jeshi kupigana! [Mwisho wa Nukuu]

4- Imran Khan aliamiliana na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), wakati mfuko huu uko chini ya udhibiti wa Marekani. Imran Khan alitekeleza sera zake, baada ya kuzungumza dhidi ya kukabiliana na IMF katika kampeni yake ya kuwania madaraka. Hakika, Imran alikuwa amesema kabla ya kuingia madarakani, katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la Uingereza, ‘The Guardian,’ mnamo tarehe 18 Septemba 2011, kwamba, “Nchi inayotegemea misaada? Mauti ni bora kuliko hayo. Inakuzuia kufikia uwezo wako, kama ukoloni ulivyofanya. Msaada ni udhalilishaji. Kila nchi ninayoijua ambayo imekuwa na mipango ya IMF au Benki ya Dunia imefukarisha tu maskini na kuwatajirisha matajiri.” Hata hivyo, alipoingia madarakani alikanusha ahadi yake! Mazungumzo na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yalianza kwa dhati. Kisha, mnamo tarehe 3 Julai, 2019, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulikubali kupanga mkopo wa dolari bilioni 6 kwa Pakistan chini ya Mpango wa Hazina ya Muda wa Miezi 39 (EFF)...

5- Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan, alikumbuka huduma kwa Amerika, katika mahojiano na Fox News mnamo Jumatatu 22/7/2019, akisema, "Sisi Pakistan kila wakati tulihisi kuwa sisi ni mshirika wa Amerika na ikiwa tulikuwa tumepewa taarifa kuhusu Osama bin Laden, tulipaswa kumtoa nje. Na bado ISI ndiyo iliyotoa taarifa iliyopelekea kulitambua eneo aliko Osama bin Laden. Ukiiuliza CIA ilikuwa ni ISI ndiyo iliyotoa eneo la awali kupitia unganisho la simu." Alisema hayo "katika ziara ya kwanza ya shujaa wa zamani wa kriketi katika Ikulu ya White House, tangu kuchaguliwa kwake mwaka mmoja uliopita nchini Pakistan, ambapo alikutana na Rais wa Marekani Donald Trump," kama ilivyoripotiwa na Al-Quds Al-Arabi mnamo 23/07/ 2019.

Tatu: Uhusiano wenye mvutano kati ya Imran na uongozi wa jeshi, na kisha Marekani:

Imran Khan aliendelea kuwa chini ya udhibiti wa jeshi, na Marekani nyuma yake, kwa takriban miaka mitatu ya utawala wake. Mwishoni mwa mwaka wa tatu, uhusiano wake na Mkuu wa Jeshi Bajwa ulizidi kuwa mbaya, kama ilivyokuwa baadaye na Amerika kwa kuunga mkono msimamo wa jeshi. Imran alikataa kumkubali mgombea wa jeshi kwa nafasi ya mkuu wa ISI. Luteni Jenerali Anjum Nadeem aliposimamishwa katika uteuzi huo, jambo ambalo lilisababisha hali ya wasiwasi katika jeshi... Kama ilivyoripotiwa na tovuti ya Al-Manar TV mnamo tarehe 27/10/2021, “Anjum atachukua wadhifa wake mpya mnamo tarehe 20 Novemba. Mnamo tarehe 6 Oktoba, Bajwa alimteua Anjum kuchukua nafasi ya mkuu wa ISI, Luteni Jenerali Faiz Hameed. Anjum alikuwa akichukua nafasi ya Kamanda wa Kikosi katika mji wa bandari wa kusini wa Karachi. Bajwa alimteua Hameed kama Kamanda wa Kikosi huko Peshawar mwezi huu. Imran Khan amekuwa akitangaza hadharani kumuunga mkono Faiz Hameed kama kiongozi wa ujasusi wa ndani. Kwa hivyo, uhusiano wa serikali ya Imran Khan na jeshi uliharibiwa na mivutano, kufuatia kuteuliwa kwa Nadeem Anjum mahali pa Faiz Hameed. Hii ilikuwa hasa miongoni mwa uvumi ulioenea kwamba Khan angemteua Hameed kuchukua nafasi ya Qamar Javed Bajwa, ambaye muhula wake wa pili madarakani unamalizika Novemba 2022.

Kwa kweli, Amerika inasimama nyuma ya mkuu wa jeshi. Kwa hivyo, uamuzi ulifanywa ili kuandaa njia ya kuondolewa kwa imani kutoka kwa Imran Khan, sambamba na kutafuta mbadala wake. Imran Khan alipokea baadhi ya taarifa hizi. Kwa hiyo, Imran alijaribu kufanya upatanishi na uongozi wa jeshi. Alikubali kumteua Nadeem Anjum mahali pa rafiki wa Imran, Faiz Hameed. Hata hivyo, uongozi wa jeshi ulisisitiza, kwa msaada wa Marekani, kwamba Imran lazima aondolewe katika nafasi ya uwaziri mkuu, kwa kuteuliwa mtu mwingine! Jeshi na Amerika ziliogopa kwamba ukiukaji huu wa uamuzi wa jeshi ungesababisha kudhoofisha maamuzi ya jeshi, linaloungwa mkono na Amerika. Hivyo msisitizo wa kumuondoa Imran...

Nne: Imran Khan alifazaika, haswa kwa vile alitoa huduma kubwa kwa Amerika kama tulivyotaja, wakati vivyo hivyo, alitii uongozi wa jeshi ... ni kana kwamba aliamuru kwamba jeshi na Amerika zitafanya kazi ya kumtenga, baada ya huduma alizowapa. Hata hivyo, alisahau au kujisahaulisha kwamba nchi za makafiri haziruhusu mawakala wao kupata nafasi ya kupumua! Kwa vyovyote vile, alikasirishwa na jambo hili na akatoa kauli kuhusu Amerika, lakini wakati huo alikuwa amechelewa! Miongoni mwa kauli zake:

1- Kama ilivyoripotiwa na Euro News Arabia mnamo 4/2/2022, "Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan aliambia kundi la waandishi wa habari wa kigeni leo, Jumamosi, 'Hatua ya kuniondoa ni kuingiliwa kwa wazi kwa siasa za ndani na Marekani." Gazeti la Arab Post la tarehe 3/4/2022 lilisema kuwa, "vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba Khan alipokea ujumbe kutoka kwa balozi wa Islamabad jijini Washington ambao ulijumuisha rekodi ambayo afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani, anayesemekana kuwa Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa Masuala ya Kusini na Kati ya Asia, Donald Lu, akitangaza kwamba Amerika ilihisi kuwa uhusiano unaweza kuwa bora ikiwa Khan ataondoka.

2- Katika hali inayotofautiana na msimamo wa Washington kuhusu Urusi kuhusiana na shambulizi lake dhidi ya Ukraine, Imran Khan alikataa kulaani shambulizi hilo na hata alitembelea Moscow, akitokea karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin, mnamo tarehe 24/2/2022, yaani siku ya kwanza ya vita vya Urusi dhidi ya Ukraine. Hii ni wakati ambapo mkuu wa jeshi la Pakistan, Qamar Bajwa, alilaani shambulizi hilo kwa uwazi, akiunga mkono msimamo wa Marekani na kupinga kauli za hivi karibuni za Khan. Al Hurra iliripoti mnamo 2/4/2022 kwamba, "mkuu wa jeshi la Pakistan alikosoa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, akitaka kusitishwa mara moja kwa kile alichoelezea kama "janga kubwa," lililoathiri nchi ndogo. Ni vyema kutambua kwamba ukosoaji wa Jenerali Qamar Javed Bajwa dhidi ya Moscow unakinzana na Waziri Mkuu wa nchi yake, Imran Khan. Imran Khan alitetea haja ya kutoegemea upande wowote kwa Islamabad, akiielekeza kwenye kile kinachotokea nchini Ukraine. Pia alikataa kukosoa vitendo vya Rais wa Urusi Vladimir Putin.

3- Katika hali nyingine, kama ilivyoripotiwa na 'The New Arab,' mnamo tarehe 7/3/2022, "Imran Khan alizungumza kuhusu mabalozi wa Muungano wa Ulaya kuandika barua ya kumtaka alaani operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine... Imran alisema. , ‘Nataka kuwauliza mabalozi wa Muungano wa Ulaya: Je, mliiandikia India barua kama hiyo?’ Akaongeza, ‘Mnaonaje kutuhusu? Je, sisi ni watumwa wenu...kwamba chochote mtakachosema, tutafanya?’ Mpakistani huyo aliamua kuendelea, “Wakati India ilipokiuka sheria za kimataifa huko Kashmir na Maazimio ya Baraza la Usalama la Marekani, je, yeyote kati yenu [mabalozi wa EU] aliikosoa India. Je, mulivunja uhusiano na India? Au kusimamisha biashara nao?”

Tano: Kama tulivyosema hapo juu, Imran Khan hakutarajia kwamba utumishi wake wote kwa jeshi, na nyuma yake, Amerika, haungekuwa na manufaa kwake! Ni kana kwamba hakutambua kwamba yeyote anayeingia madarakani kwa kuungwa mkono na makafiri wa kikoloni, kama wakala wao, anakuwa kama kipande cha chesi kwao. Wanamwendesha wapendavyo. Zaidi ya hayo, wanamtoa kama wapendavyo, bila kusita, ikiwa hatafikia masilahi yao. Hiki ndicho kilichotokea kwa Imran Khan! Mnamo tarehe 7/4/2022, uamuzi wa Naibu Spika ulikataa kura ya hoja ya upinzani ya kutokuwa na imani dhidi ya serikali ya Imran Khan. Pia ulibatilisha uamuzi wa Rais wa Jamhuri wa kulivunja Bunge tarehe 3/4/2022 na kuelekea kwenye uchaguzi wa mapema, kwa ushauri wa Waziri Mkuu Imran Khan. Mahakama iliamua kuwa hatua hii ni kinyume na katiba na hivyo kuwa batili. Mahakama kuu pia ilimuamuru spika wa bunge kufanya kikao cha Bunge tarehe 10/4/2022, ambapo Bunge la Pakistan lenye viti 342 lilipiga kura 174 za kutokuwa na imani na Imran Khan... Ni wazi kuwa katika matukio haya, jeshi lilikuwa likiendesha mambo nyuma ya pazia. Majaji wakuu hawangeweza kamwe kuchukua uamuzi kama huo bila kuungwa mkono kikamilifu na mkuu wa jeshi...

Sita: Siku iliyofuata, 11/4/2022, Bunge lilimchagua Shehbaz Sharif kuwa Waziri Mkuu, hadi tarehe ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2023. Kuhusu Shehbaz, yeye ni kaka mdogo wa Nawaz Sharif, ambaye alikuwa wa kwanza. Waziri Mkuu wa Pakistan. Shehbaz amekuwa kiongozi wa upinzani katika Bunge la Pakistan tangu 2018. Shehbaz alichukua uongozi wa Pakistan Muslim League baada ya kaka yake Nawaz, ambaye alianzisha chama. Shehbaz alijitolea kuwa mtiifu kwa jeshi na Marekani... na kisha jeshi likamuunga mkono katika uchaguzi wa kuchukua nafasi ya Imran Khan na akafanya yafuatayo:

1- Shehbaz alianza muhula wake wa kisiasa kulingana na Amerika inavyotaka... Alianza kwa sauti ya maridhiano na India, akisema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo badala ya makabiliano. Sky News kwa Kiarabu iliripoti mnamo 14/4/2022 kwamba "Katika hotuba yake ya kwanza, Shehbaz Sharif alisema, 'Tunataka uhusiano mzuri na India lakini hakuwezi kuwa na amani endelevu isipokuwa suala la Kashmir litatuliwe,' huku akitoa wito kwa Waziri Mkuu wa India kuruhusu utatuzi wa suala la Kashmir na hivyo nguvu zitolewe kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo mbili. Waziri Mkuu wa India Modi alimjibu kwa kutuma barua pepe, "Hongera H.E. Mian Muhammad Shehbaz Sharif kwa kuchaguliwa kwake kama Waziri Mkuu wa Pakistan. India inatamani amani na utulivu katika eneo lisilo na ugaidi, ili tuweze kuzingatia changamoto zetu za maendeleo na kuhakikisha ustawi wa watu wetu. Kumbuka kuwa Waziri Mkuu wa India anachukia Uislamu na Waislamu. Modi anawachochea wafuasi wake wa Kibaniani dhidi ya Waislamu nchini India. Wafuasi wake wanawawekea vikwazo Waislamu na hawakubali Waislamu waishi katika nchi yao ya India. Wanawawekea vikwazo mabinti wa Kiislamu shuleni katika suala la kanuni za mavazi ya Kiislamu.

2- Ripoti za habari zinataja kwamba Shehbaz Sharif alijitolea kufanya kazi na majenerali, ikiwa atachaguliwa. Alisema nchi hiyo ilihitaji kusonga mbele na kuondokana na tofauti na jeshi. Hapo awali alikuwa amelikosoa jeshi katika mapinduzi yake dhidi ya kaka yake mkubwa, Waziri Mkuu wa zamani, Nawaz Sharif, mwaka wa 1999. Shehbaz Sharif alishiriki katika uchaguzi wa 2018 lakini alishindwa na Imran Khan. Mnamo Disemba 2019, Afisi ya Kitaifa ya Uwajibikaji ilizuia mali 23 zinazomilikiwa na Shehbaz na mwanawe, na kuwashtaki kwa ulanguzi wa pesa. Mnamo Septemba 2020, Shehbaz alikamatwa kwa tuhma za kuhusika na ulanguzi wa pesa, lakini aliachiliwa mnamo Aprili 2021 kwa dhamana. Kwa hivyo, maridhiano yake na jeshi ilikuwa moja ya sababu zilizomruhusu kushika madaraka.

3- Hebu turegelee hapa pongezi za haraka za Amerika kwa Shehbaz Sharif, kama Waziri wake wa Mambo ya Nje, Blinken, alisema, "Marekani inampongeza Waziri Mkuu mpya wa Pakistan Shehbaz Sharif na tunatarajia kuendeleza ushirikiano wetu wa muda mrefu na serikali ya Pakistan...” (Sky News 4/14/2022). Hii inathibitisha kwamba Marekani imekubali maridhiano ya Shehbaz na jeshi, pamoja na ahadi yake ya kutekeleza sera ya Marekani. Ilikubali kupanga mafanikio yake ya kuingia madarakani, baada ya kuwazuia yeye na kaka yake Nawaz hapo awali. Sasa Marekani imekubali tu baada ya Shehbaz kuwa tayari kabisa kufanya kazi na Marekani, wakati yeye ameshapatana na jeshi ambalo ni tiifu kwa Marekani!

4- Sauti ya Amerika (VOA) iliripoti mnamo tarehe 12/4/2022, kwamba "serikali mpya ya Pakistan ilisema Jumanne "itazungumza kwa njia ya kujenga na chanya" na Marekani ili kukuza "malengo ya pamoja" ya amani ya kikanda, usalama na maendeleo... "Tunakaribisha uthibitisho wa Marekani wa uhusiano wa muda mrefu na Pakistan," afisi ya Sharif ilisema katika kujibu matamshi ya mwandishi wa habari wa White House Jen Psaki siku ya Jumatatu ambapo alisisitiza ukosoaji wa uhusiano wa Washington na Islamabad bila kujali kiongozi wake. "Tunatazamia kuimarisha uhusiano huu muhimu juu ya kanuni za usawa, maslahi ya pande zote na manufaa ya pande zote," taarifa ya Pakistan ilisema. Siku ya Jumatatu, Psaki alisema utawala wa Biden unaunga mkono "kudumishwa kwa amani kwa kanuni za kidemokrasia za kikatiba" na hauungi mkono chama kimoja cha kisiasa dhidi ya kingine nchini Pakistan. "Tunathamini ushirikiano wetu wa muda mrefu na Pakistan, siku zote tumeiona Pakistan yenye ustawi na ya kidemokrasia kama muhimu kwa maslahi ya Marekani," alisema. Psaki alisema uhusiano "wa muda mrefu, wenye nguvu na wa kudumu" utaendelea chini ya viongozi wapya jijini Islamabad."

Hii inathibitisha kwamba Amerika ilikuwa nyuma ya anguko la wakala wake wa zamani, Imran Khan, na kupandishwa cheo kwa Shehbaz Sharif, ambaye anatangaza waziwazi nia yake ya kufanya kazi na Marekani, kwa nguvu zaidi kuliko Imran Khan alivyofanya!

Saba: Mawakala hawa hawajifunzi wala hawafikirii. Iwapo Marekani itampindua mmoja wao, wanakimbilia kusuhubiana na Marekani na kujiandaa kutoa huduma kwa Amerika, hadi wafikie kutawala. Inawafafanua kuwa ni duni kuliko viongozi halisi wa kisiasa wa kimfumo, wanaotafuta nyadhifa pekee. Shehbaz Sharif hakujifunza kutoka kwa Amerika kumpindua kaka yake zaidi ya mara moja, wakati yeye pamoja naye waliadhibiwa kwa kupelekwa uhamishoni. Ummah unahitaji wanasiasa wenye maadili wanaoshikamana na mfumo, ambao ni mfumo wa Umma, Uislamu. Uislamu pekee ndio unaoyachukulia mambo yote kwa njia kimsingi na sahihi, huku wanasiasa wake pekee ndio wanaoweza kuuokoa Ummah, kuuhuisha na kuufanya kuwa na dola kuu, sio nchi inayonyenyekeshwa chini ya Amerika.

Kwa hakika, Pakistan inastahiki kuwa nukta ya nusra kwa dola hii tukufu, dola ya Khilafah Rashida, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt).

[إِنَّ فِي هَذَا لَبَلَاغاً لِقَوْمٍ عَابِدِينَ]

“Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.” [Sura Al-Anbiyyah 21:106]

5 Shawwal 1443 H

5/5/2022 M

 

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu