Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ukanushaji wa Uislamu Juu ya Nadharia ya Usawa wa Kijinsia

(Imetafsiriwa)

Tunapo jadili juu ya mada ya nadharia ya usawa wa kijinsia na vipi inaangaliwa na Uislamu, tunaona kuwa kuna masuala mawili ya kimsingi ambayo lazima tuyazungumzie. Nayo ni:

1. Kukosekana kwa ufahamu kuhusiana na hadhi ya wanawake katika Uislamu na majukumu yaliowajibishwa kwao na Shariah.

2. Mkanganyiko kuhusiana na haki za wanawake na kukosekana kwa nidhamu inayowatetea.

Kwa hivyo, kama jaribio lolote lingefanywa kuelezea msimamo wa Uislamu kuelekea nadharia ya usawa wa kijinsia, masuala haya mawili lazima yaelezwe. Lazima kwanza tuangalie Uislamu unasema nini juu ya wanawake, haki gani wamepatiwa, na majukumu gani waliopewa na Shariah. Yatakapowekwa wazi haya ndipo tutapoweza kulinganisha Uislamu na nadharia ya haki za kijinsia na kufanya hitimisho juu ya ima nadharia hii ina afikiana na Uislamu ama la. Hivyo, hebu tuanze, insha’Allah.

Hadhi ya wanawake katika Uislamu na majukumu yao kwa mujibu wa Shariah

Dhana ya kuwa wanaume ni sawa na wanawake, kwa namna yoyote, haipo katika Uislamu. Ndio, wao ni sawa kwa kuwa wote ni wanaadamu, wote ni waja wa Muumba wao, Mwenyezi Mungu (swt) na wote wanawajibika kumuabudu Yeye (swt).

Kilicho wazi, hata kwa mtoto mdogo ni kuwa wanaume na wanawake ni aina mbili tafauti. Wao ni tafauti katika namna ambayo Mwenyezi Mungu (swt) amewaumba na akaisadikisha tafauti hii. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

[وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنثَى]

Na mwanamume si sawa na mwanamke.” [Surah Aali Imran 3:36].

Uwepo wa wenye jinsia mbili, wanaojulikana pia kama khuntha, hakupingi ukweli kwamba wanaume na wanawake ni watu wa jinsia tafauti. Hii ni kwa sababu kukinzana na sheria hakupelekei kutofaa kwa sheria. Kwa hakika, ni kuwa kukinzana kunakuwepo kwasababu ya hiyo sheria.

Wanaadamu huzaliwa na vidole vitano, japokuwa kunakuwepo na hali zisizo za kawaida za watoto kuzaliwa na zaidi au pungufu ya hivyo. Vivyo hivyo, kuna jinsia mbili za watu, japokuwa jinsia za baadhi ya watu zinakuwa katika hali ya utata.

Bila shaka, tunayapatia nafasi mambo ya upekee na Shariah inawapatia hasa nafasi wenye jinsia mbili. Hata hivyo, hiyo sio mada inayozungumziwa hapa.

Kile kinachozungumzwa ni hadhi ya wanawake katika Uislamu. Qur’an inawatafautisha kwa uwazi na wanaume juu ya msingi wa kuwa ni jinsia tafauti. Swali lifuatalo je, ni tafauti zipi nyengine zinazopo baina ya wanaume na wanawake?

Tunapochunguza Shariah na majukumu ambayo Mwenyezi Mungu (swt) amewapatia waumini, tunaona katika baadhi ya hali, wanaume na wanawake wanapewa majukumu sawa, katika hali yao kama wanaume, na katika hali nyengine, wanakuwa na majukumu tafauti, katika hali zao wakiwa ni watu wa jinsia tafauti. Katika hali ambapo kuna majukumu yanayolingana, tuna mifano ya wao wote wawili kutakiwa kutekeleza swala tano kila siku na katika kuamrisha mema na kukataza maovu. Tena kuna hali ambapo katika vipengele vyote vya Shariah ambapo wanaume na wanawake wanapatiwa majukumu tafauti. Katika ibadat, tuna mfano wa mwanamume anawajibishwa kutekeleza swala ya Ijumaa ambapo mwanamke hawajibishwi. Katika munakahat, tuna mfano wa mwanamume kupewa jukumu la kuwa msimamizi kwa mkewe na mke kutakiwa kumtii yeye.

Hivyo, kile tunachokisema ni kuwa katika baadhi ya hali majukumu ya waumini wanaume na wanawake ni sawa na katika baadhi ya hali ni tafauti. Mwenyezi Mungu (swt) ni Yule aliyeyaweka majukumu haya na sisi tukiwa waja Wake, tunawajibika kuyatekeleza kwa kadiri ya uwezo wetu. Yeye (swt) ni Al-Hakiim, Mwenye Hekima na ni Mwenye Busara na kwa sheria zake pekee tunanyenyekea. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

[إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]

“Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia na tunatii! na hao ndio wenye kufanikiwa.” [Surah An-Nur 24:51].

Haki za wanawake katika Uislamu na nidhamu inayowahifadhi

Kama tunavyofahamu kuwa ni Shariah ndio inayoweka wajibu na majukumu ya waumini, pia vile vile tunafahamu kuwa haki za waumini zinapatikana kutoka kwenye sheria za Mwenyezi Mungu (swt). Hii ni kwa sababu haki za mja zinapatiwa wao kutoka kwa bwana wao na Mwenyezi Mungu (swt) ni As-Sayyid, Bwana, na sisi ni waja Wake wanyenyekevu.

Kwa hivyo, ili kuona haki gani mwanamke anazo katika Uislamu, tunageukia kile ambacho Mwenyezi Mungu (swt) amekiteremsha na kupitia kwa Mtume wa mwisho, Muhammad (saw). Mwenyezi Mungu anasema,

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا]

“Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho. Hayo ndio bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.” [Surah An-Nisaa 4:59].

Tatizo, hata hivyo, sio kuwa Shariah haikuwapatia haki wanawake. Lakini, tatizo lililopo ndani ya Ummah hivi leo ni kuwa haki za wanawake hazijahifadhiwa.

Na hapa tunageukia katika suala kubwa zaidi.

Kukosekana kwa Khilafah na utabikishaji wa Shariah

Ilikuwa mnamo mwaka 1924 Miladi ambapo wakala wa Magharibi, Mustafa Kamal, alifanikiwa kuivunja Khilafah Uthmaniya na, chini ya Mkataba wa Sykes-Picot, mataifa ya Magharibi yaliigawa ardhi ya Waislamu miongoni mwao.

Kilichofuatia ilikuwa ni kuin’goa kabisa Shariah kutoka kwenye jamii ambazo Waislamu wanaishi. Sheria zinazotawala ardhi zao zilibadilishwa kutoka kwenye Shariah hadi zile za Magharibi. Mamlaka ya mahakama za Shariah mwanzoni ziliwekewa kikomo kabla ya kuondolewa kabisa. Mageuzi yalifanyika katika taasisi za elimu ili watu wasiendelee kufundishwa Dini yao badala yake wafundishwe kwa mitaala ya Kimagharibi. Kila mahali, katika nyanja zote za jamii, Shariah iliwindwa na wakoloni na kun’golewa kwa nguvu.

Matokeo ya haya ilikuwa ni kwamba Ummah ulikumbana na matatizo makubwa sana. Kukiwa hakuna dola ya Khilafah inayoamrisha mema juu ya watu na kutabikisha Shariah, ulimwengu wa Kiislamu ukawa umegubikwa na kila aina ya uovu na udhalimu.

Katika suala la wanawake, udhalimu ulikuwa, na bado umekuwa mkubwa na mbaya zaidi.

Ndoa za kulazimishwa, ukiukwaji wa haki ya mwanamke ya kuachwa, na ulaji wa mali ya mwanamke kwa dhulma, kwenye mikono ya mume wake au jamaa wa mume, ikiwa ni mifano michache tu inayojulikana zaidi na mifano ya wazi.

Dhulma inayowakumba wanawake inafanywa iwe wazi zaidi wakati dini inapochafuliwa kwa makusudi na kutumiwa kama kisingizio. Hivyo, hukm ambayo mwanamke lazima amtii mumewe inatumika kuwa ni kinga ya mume wakati anapombughudhi mkewe au anaposhindwa kumpatia haki zake zilizo juu yake na hukm ambayo ni dhambi kwa mwanamke kukataa jimai na mumewe, isipokuwa atapokuwa na dharura ya kisheria, inatumika na mume kuhalalisha kila aina ya machukizo yanayofanywa dhidi ya mke. Tunafahamu kadhia ambapo mwanamume anambaka mwanamke, ambaye sio mke wake, kisha anamlazimisha kufunga naye ndoa, ili kukwepa adhabu!

Kadhia kama hizi zinaonyesha hali ya masikitiko ambapo Ummah unajikuta hivi leo. Kwa kukosekana Khilafah, hakuna mfumo unaofundisha watu kwa upana juu ya Dini yao, unaoamrisha watu tabia njema na uchamungu, na kuchukuliwa hatua walio waovu. Sio tu haki za wanawake ambazo hazihifadhiwi, bali pia haki za kila mtu kila mahali.

Nadharia ya usawa wa kijinsia sio suluhisho                                          

Kufahamu kuwa kukosekana kwa Khilafah na utabikishaji wa Shariah ndio sababu za kweli za kutopatikana uadilifu kwa wanawake katika Ummah huu ni jambo muhimu katika mjadala wetu wa nadharia ya usawa wa kijinsia.

Hii ni kwa sababu hivi sasa kuna imani inayoongezeka miongoni mwa pote la Ummah huu kuwa njia sahihi ya kupata haki za wanawake ni ulinganizi wa fikra ya usawa wa kijinsia.

Hata hivyo, kile ambacho lazima kifahamike na waumini wa Ummah huu ni kuwa usawa wa kijinsia sio suala la njia fulani. Bali ni fikra, iliyozalikana juu ya imani ya kikafiri inayotoka kwa Wamagharibi. Ili kufahamu kwa upana nini kinakusudiwa kwa hili, tutachunguza historia ya fikra hii kwa Wamagharibi.

Maendeleo ya nadharia ya usawa wa kijinsia katika nchi za Magharibi na ukafiri wake wa asili

Fikra ya kuwa wanawake kiasili ni duni kuliko wanaume ni dhana iliyopatikana zamani wakati wa wanafalsafa wa Kigiriki wa zamani. Aristotle alisema kuwa, “Wanawake mbele ya mwanamume ni kama mtumwa mbele ya bwana, mfanyikazi za mikono mbele ya mfanyikazi za kiakili, mshenzi mbele ya Mgiriki. Mwanamke ni mtu asiyekamilika, anayeachwa katika hatua ya chini ya maendeleo.”

Baadaye, wakati Wakristo walipoidhibiti Ulaya, uoni wao juu ya wanawake haukuwa bora hata kidogo. Maelezo ya Biblia juu ya Bibi Hawa kuwa amedanganywa na Ibilisi akala tunda na kumpatia sehemu yake Adam, na kupelekea wote wawili kuhamishwa Peponi, yamezua hisia katika thaqafa ya Kimagharibi kuwa wanawake kiakili ni duni kuliko wanaume, watukutu, na wasumbufu kwa wanaume.

Kutokana na uoni huo ndio kumepelekea kubughudhiwa na kukandamizwa kwa wanawake katika jamii za Wamagharibi kwa karne nyingi. Walikoseshwa haki ya kuvunja ndoa na, kutokana na imani kuwa wanawake hawakuwa wenye kuaminika na hawakuwa waungwana, hawakuruhusiwa kusimamia mali zao wenyewe. Badala yake, mali ya mke ikawa ni mali ya mumewe na akaweza kuitumia apendavyo lakini yeye mke akinyimwa haki hiyo. Haki zote hizi, ile ya kuvunja ndoa na ya kusimamia mali, walikwisha patiwa na Mtume wetu Mtukufu (saw) takriban karne saba kabla ya Mwamko wa Ulaya kujitokeza.

Imani ya Wakristo kuwa Bibi Hawa alimshawishi Adam kumega tunda, pia imepelekea imani kuwa wakati wanawake wanaporuhusiwa kuzungumza, ni shetani tu ndiye hufuatia na hivyo ni bora kuwanyamazisha. Katika nchi nyingi za Ulaya wakati wa Zama za Kati, kigwe cha makaripio, aina ya kizibo cha mdomo, kiliwekwa kupitia juu ya vichwa vya wanawake, wanaonyanyua sauti au kukasirisha waume zao.

Ilikuwa ni baada ya karne kadhaa za manyanyaso kama hayo na uonevu ambapo wanawake walijipanga na kuanza kudai haki kwa uwazi. Hivyo, katika karne ya kumi na tisa, likaja wimbi la kwanza la nadharia ya usawa wa kijinsia, ambalo lilitafsiriwa kwa juhudi za wanawake wa Kimagharibi kuhifadhi haki za msingi kama haki ya kupiga kura na haki ya kumiliki mali.

Juu ya hivyo, hata baada ya haki hizi kupatiwa, Wamagharibi bado wamejaa pomoni fikra zinazotumiwa kuwanyanyasa wanawake. Chukua kwa mfano, dhana ya Kimagharibi ya “upambanuzi wa kibaiolojia”.

Fikra iliyowekwa na wanafikra wa Kimagharibi ni kuwa majukumu ya mwanamume na mwanamke katika jamii yanapambanuliwa kwa baiolojia yao. Baiolojia yao, inafahamika, imewafanya kimsingi kuwa ni tafauti. Fikra hii, ya kuwa mwanamume na mwanamke ni viumbe tafauti kibaiolojia, pia inafahamika katika Dini yetu, kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa mjadala huu.

Hata hivyo, pale ambapo Wamagharibi wamekosea ni kuwa wameifanya akili ya mwanaadamu kuwa msingi wa kupangilia majukumu ya kijinsia badala ya Shariah. Akili ya mwanaadamu, kama tunavyoifahamu, haijakamilika na inaweza kukosa. Haya yamepelekea kwenye hatua za aina zote hizi zilizoenea kote kuhusu wanawake.

Kwa mfano, katika karne ya kumi na tisa, madaktari wa Kimagharibi walitunga wazo la kuwa mwili wa mwanamke ni “anabolic” yaani unahifadhi nishati badala ya kuitumia nishati. Wanatoa sababu ya kuwa hii inawafanya wanawake kuwa magoigoi na wapo baridi na kwa hivyo, hawastahiki kuwa katika wigo wa kisiasa. Kwa hivyo fikra kama hizi zilitumika kuhalalisha kuwanyima wanawake haki ya kuchagua na kuwatenga kutoka katika siasa.

Fikra hii isiyoeleweka ya “utambuzi wa kibaiolojia” ndio iliopelekea wimbi la pili la nadharia ya usawa wa kijinsia. Wanafikra wa nadharia hii kama Simone de Beauvoir na Betty Friedan walianza kupingana na fikra kuwa baiolojia inaamua dori ya mwanamke katika jamii na kuanza kushajiisha fikra ya kuwa mwanamke anaweza kuwa sawa na mwanamume kwa upande wa utendaji wake katika jamii.

Juhudi hii ya nadharia ya usawa wa kijinsia kuwakomboa wanawake kutokana na vikwazo vya vizuizi vya kibaiolojia imekuwa na matokeo yasiotarajiwa. Huku fikra ya nadharia hii ikiendelea kukua na mawimbi ya tatu na nne yakianza, wanafikra kama Judith Butler alichukua fikra za mfuasi wa nadharia hii ya wimbi la pilli kama Simone de Beauvoir katika kiwango kipya cha juu zaidi.

Kile kilichoanza kusemwa ni kuwa sio tu dori ya mwanamke katika jamii haisitambuliwi kwa baiolojia yake bali pia jinsia yake isitambuliwe kwa baiolojia yake. Fikra hii ya kuwa jinsia ni “muundo wa kijamii” tu na kuwa mwanamke hakufasiriwa kwa baiolojia yake ndio iliopelekea maendeleo ya harakati za wenye jinsia mbili.

Hivi sasa, dhana iliyopo kwa Wamagharibi ni kuwa mwanamume na mwanamke wanaweza kuchagua jinsia zao wenyewe. Mwanamume anaweza kuvaa nywele bandia na sketi na kuanza kujiita mwanamke. Hii ni dhambi nyengine kubwa zaidi, kwani imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas (ra) kuwa,

وَالْمُتَشَبِّهِينَ بِالنِّسَاءِ مِنَ الرِّجَالِ» «لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم الْمُتَشَبِّهَاتِ بِالرِّجَالِ مِنَ النِّسَاءِ

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amewalaani wanawake wenye kujishabihisha na wanaume na wanaume wenye kujishabihisha na wanawake.” (at-Tirmidhi).

Hivyo, kinachooneka hapa ni kuwa kutabanni ukafiri moja kunapelekea kupatikana ukafiri mwengine. Katika mapambano ya Wamagharibi ya “wenye mwamko” kuhifadhi haki za wanawake wao, waliishia kuvunja kile kilichomfafanua kuwa mwanamke.

Hii ni hadhari kwa waumini. Watu wema waliopita walikuwa wakiuonya Ummah kuwa kama ambavyo malipo ya kutenda mema, Mwenyezi Mungu (swt) humuongoza mtu kuelekea kwenye jema jengine, basi adhabu ya kutenda ovu ni kuwa mtu atazongwa na maovu mengine. Vivyo hivyo, wakati muumini atakapojiweka mbali kutokana na sheria za Quran na Sunnah na kuanza kuchukuwa fikra za kikafiri, hatofanikiwa nazo. Atazama kwenye dimbwi la dhambi ambapo njia pekee ya kuokoka ni kuregea kwenye kile ambacho Shariah imekiweka.

Hili linazidi kupigiwa mfano kwa kujipenyeza kwa usoshalisti kwenye harakati za fikra ya utetezi wa wanawake.

Wakati sehemu ya mwanzo ya fikra ya usawa wa kijinsia ilipoanza kuibuka mwishoni mwa karne ya 19, ilipenyezwa kwa haraka kwenye falsafa ya kiujamaa. Ilikuwa ni wanafikra wa kiujamaa kama Friedrich Engels ambao walifafanua ndoa kuwa ni mapambano ya kitabaka baina ya wanaume na wanawake, sawa na mapambano ya kitabaka yaliotokea baina ya mabwanyenye na tabaka la wafanyikazi. Hii imedhoofisha thamani ya jamii iliyowekwa kwenye ndoa. Baadaye, katika karne ya 20, Simone de Beauvoir alijenga fikra za kiujamaa za mapambano ya kitabaka na akahitimisha kuwa mwishowe, wanawake na wanaume watakuwa katika mapambano ya kitabaka. Hali ambayo ni kinyume na ufahamu wa Kiislamu kuwa wanaume na wanawake ni vipenzi (awliyaah) wao kwa wao. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

[وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ]

Waumini wanaume na waumini wanawake ni vipenzi (‘awliyah) baina yao…[Surah At-Tawba 9:71].

Kuwapambanisha wanaume na wanawake baina yao haipelekei chochote isipokuwa madhara tu. Zingatia hivi sasa, kwa kutanda fikra ya usawa wa kijinsia katika nchi za Wamagharibi, jinsi gani viwango vya talaka vinaongezeka na watoto zaidi na zaidi wanalelewa na kina mama pekee wanaolazimika pia kufanya kazi. Haya hayahusishwi pekee na fikra ya usawa wa kijinsia bali pia kuongezeka kwa maisha ya anasa na ubinafsi. Watu hawathamini tena ndoa au muundo wa familia bali hutaka starehe za muda mfupi na uzoefu wa kuwahakikishia hali yao ya ubinafsi. Kutokana na hayo, watu wachache katika Wamagharibi ndio wanaofunga ndoa, viwango vya uzinifu vinaongezeka, idadi ya watoto wanaozaliwa inapungua, uavyaji mimba unazidi, na, kutokana na watu wengi kujiingiza kwenye zinaa, viwango vya maradhi ya yanayoambukizwa kupitia ngono vinaongezeka.

Hii ndio sababu ya kwa nini fikra za makafiri lazima zichunguzwe kwa makini. Kile kinachoonekana kuwa hakina madhara kwa kuangaliwa juu juu tu kinaweza kusababisha kuangamia kwa Ummah. Nadharia ya usawa wa kijinisa inaonyeshwa kwa waumini kuwa ni njia ya kuhakikisha haki za wanawake lakini misingi yake si chochote bali ni muozo na ukafiri.

Haki za wanawake na ajenda za kikoloni

Kuna nukta nyengine ambayo lazima tuifahamu kuhusiana na fikra ya usawa wa kijinsia. Nayo ni, fikra hii haikuletwa katika ulimwengu wa Kiislamu na Wamagharibi kwa nia njema ya “kuwakomboa” wanawake. Bali, imeletwa ili kuihujumu Shariah na kuongeza kampeni ya wakoloni kuwatawala Waislamu.

Wakoloni walipoingia katika ulimwengu wa Kiislamu, walitekeleza kupitia njia kadhaa kuin’goa Shariah na kuweka badala yake nidhamu nyengine za kisheria. Moja ya njia zao za kutekeleza hayo ni kudhamini mpango wa Orientalisti; taasisi za Ulaya zilianza kutoa vikundi vya wasomi wanaosoma Shariah kwa undani na kuanza kupotosha mafundisho yake na kueneza uongo juu yake. Moja ya masimulizi hatari zaidi yanayotolewa na Ma-orientalisti ni kuwa Shariah ni mfumo wa kisheria usiobadilika unaopelekea mkwamo wa kijamii. Watu wa Ulaya wanajiona wao kuwa ni mawakala wa mabadiliko na maendeleo na kudai kuwa shule zao za sheria ni bora kuliko Shariah.

Wanadai kuwa Shariah imepitwa na wakati na haimo katika ulimwengu mpya. Moja ya hoja wanazozitumia ni kudai kuwa Shariah inawakandamiza wanawake na haiwapi haki zao. Ili kujenga hoja yao hii, kwa makusudi wanaipotosha Shariah na kueneza uongo kuhusu Waislamu.

Kwa mfano, Wazungu walipowasili nchini Uturuki, walijifunza kuhusu harem za sultani wa Kiuthmani. Harem zilitumika kama makaazi ya wanawake kwenye nyumba ya mfalme na ambapo wanawake walipewa darsa na kuelimishwa. Hakuruhusiwa mwanamume kuingia harem. Wazungu wa kiume waliochukizwa na hili, walianza kueneza uongo kwa makusudi kuhusu harem. Wakadai kuwa harem ilikuwa ni gereza la masuria wa sultan na hawakupewa chochote kufanya kwa kuwa walikuwa wakisubiri siku nzima kuitwa na sultan. Kuufanya utungo huu kuwa kweli, Ma-orientalisti walitengeneza filamu nyumbani kwao Ulaya iliyoigiza harem ya Kiuthmani na kuwakodi waigizaji wa kike ambao sura zao zinalingana na wanawake wa Mashariki. Waigizaji walipangiwa wajionyeshe kuwa waliochoshwa na kukata tamaa. Picha zao zikachukuliwa na kusambazwa kote Ulaya kusaidia kujenga mtazamo wa watu jumla kuwa dhidi ya Waislamu na Shariah.

Walikwenda mbali zaidi na kutoa picha za kuchora za kuonyesha kile wanachodhania kuwa ni muonekano wa ndani ya harem. Katika michoro hiyo, wameonyesha wanawake wa harem wakiwa uchi, na hivyo ipelekee kwa thaqafa nzima kuwa wanawake wa Kiislamu walikuwa wakiingiliana na Wazungu. Picha za ngono, zinazoonyesha waigizaji wa kike wakijifanya kama ni wanawake wa Kiislamu, zilisambazwa sana Ulaya.

Shauku ya Wazungu kwa wanawake wa Kiislamu imeonyesha uovu wao mkubwa. Nchini Algeria, Wafaransa walianzisha kampeni kuwashawishi wanawake wa Kiislamu kuzivua hijabu zao. Waliwavisha wanawake wao mashungi na kuwasimamisha mbele ya hadhara, kwa kujidai kuwa ni wanawake wa Kiislamu, na baadaye kuzivua shungi zao. Wakitarajia kuwa hiyo itawashawishi wanawake wa Kiislamu kuachana na shungi zao. Juhudi hizi zilishindwa, na katika mapinduzi ya Algeria dhidi ya Ufaransa, hijab ikawa ndio alama ya ukombozi wa Waislamu.

Kampeni ya wakoloni kuwataka wanawake wa Kiislamu kuvua hijabu zao ilikuwa ni sehemu ya mpango wao kuwatawala Waislamu. Frantz Fanon aliielezea kanuni yao katika Algeria Unveiled kuwa: “…kama tunataka kuvunja muundo wa jamii ya Kialgeria, uwezo wake wa upinzani, ni lazima kabla ya yote, tuwavamie wanawake; lazima tuende na kuwatafuta nyuma ya pazia ambako wanajificha na katika majumba ambamo wanaume wanawaweka wasionekane.”

Aliendelea kufafanua kwa kuandika: “Waalgeria, ilihakikishwa, hawatotingishika, watatoa upinzani kwa uvunjaji wa thaqafa unaofanywa na mvamizi, watapinga sera ya kugeuzwa, muda wa kwamba mwanamke wao hajageuza mkondo. Katika programu ya mkoloni, ilikuwa ni mwanamke aliepewa mpango wa kihistoria wa kumtingisha mwanamme wa ki-Algeria. Kumgeuza mwanamke, kumvutia kwenye maadili ya kigeni, kumvuta atokane na hadhi yake, ilikuwa wakati huo huo akipata nguvu muhimu dhidi ya mwanamume na kupata njia za wazi na bora za aibomoa thaqafa ya wa-Algeria.”

Nchini Misri, mtawala maalum aliyewekwa na Uingereza, Evelyn Baring, alianzisha kampeni kadhaa za kuvua hijab sawa na zile walizoanzisha Wafaransa Algeria. Hata hivyo, wakati huo huo anapo kashifu shungi kuwa ni ukandamizaji, alikuwa anatumika kama raisi wa mwanzo wa Jumuiya ya Wanaume kwa ajili ya Kupinga Haki ya kupiga kura Wanawake. Unafiki mtupu ulioonyeshwa na Baring umefichua kile ambacho ni lengo halisi la wakoloni. Hawakuwa na hamu katika “kuwakomboa” wanawake Waislamu. Lengo lao lilikuwa ni kuiondoa Shariah kama mfumo kamili wa Maisha kupitia kwanza kwa kuihafifisha.

Hitimisho

Kufikia hivi sasa inapaswa kuwa dhahiri kwa msomaji ni wapi Uislamu unasimama kuhusiana na nadharia ya usawa wa kijinsia. Ambapo Uislamu ni Dini kamilifu ya Mwenyezi Mungu (swt), nadharia ya usawa wa kijinsia si chochote isipokuwa ni fikra iliyotungwa na mwanaadamu iliyojengwa juu ya ukafiri.

Ni kwa bahati mbaya sana kwamba kwa kukosekana Khilafah, Ummah hauwezi kufikia wema kamili wa Dini yao na hivyo kuhisi haja ya kugeukia kwenye fikra za kikafiri ili kuendesha mambo yao.

Hivyo basi, imekuwa wazi kwetu sote umuhimu wa kufanya kazi ya kuregesha tena Khilafah. Ni kwa kuiregesha tu Khilafah kwa njia ya Mtume (saw) pekee ndio Shariah inaweza kutekelezwa na haki za wanawake kuregeshwa.

Basi na tujitahidi kwa nguvu zote, insha’Allah, kwenye lengo hili. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

[وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ]

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifah katika ardhi kama alivyowafanya makhalifah wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.” [Surah An-Nur 24:55].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Khalil Musab – Wilayah Pakistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu