Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Vijana wa Ummah Huu Waweza Kupatiliza Fursa ya Udhaifu wa Amerika na Kuurudisha Katika Nafasi Inayostahiki

Miaka michache iliyopita, ilikuwa ni nadra sana kupata makala juu ya kuporomoka kwa Amerika. Leo, kufifia kwa nguvu za Amerika kumekuwa ndio mada maarufu. Vichwa vya habari kama “Je, Amerika Iko Katika Mporomoko?”, “Amerika Iko Katika Kasi Kubwa ya Kuporomoka…”, “Mustakbali: Kuinuka kwa China, Kuporomoka kwa Amerika”, na “Mporomoko Mkuu wa Amerika Huenda Ikawa ni Matumaini Bora ya Kuiokoa Demokrasia” vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara pasi na utata. Kuingia kwa Trump ikuluni Whitehouse na wimbo wake wa “Amerika Kwanza” hakukufelisha tu kuzuia dhana kuhusu kuporomoka kwa Amerika, bali kumechochea zaidi dhana hii. 

Mnamo Januari 2018, Gallup ilifanya utafiti wa kimaoni katika nchi 134 na kupata kuwa viwango vya uidhinishaji dori ya Amerika ulimwenguni, vimeshuka kutoka asilimia 48% chini ya Obama hadi asilimia 30% punde tu baada ya mwaka mmoja wa utawala wa Trump. Hiki ndicho kiwango cha chini zaidi kuwahi kunakiliwa na Gallup juu ya uongozi wa kiulimwengu.  

Miongo michache tu iliyopita, Amerika ilikuwa ikijigamba kwa ushindi dhidi ya ufalme mwekundu – Umoja wa Kisovieti – pasi na kurusha risasi hata moja, na taarifa za kifahari mithili ya “nguzo pekee ya Amerika” na “nguvu ya hali ya juu” ziliviteka vichwa vya habari. Siku hizo ni tofauti mno na hali ya sasa ya Amerika.  

Jeshi lenye nguvu zaidi duniani limeshindwa kuwashinda wapiganaji limbukeni wa Afghanistan wenye silaha na mafunzo duni wanaojulikana kama Taliban. Vita vya muda mrefu vya Amerika vimedhoofisha motisha ya watu wake na kuvunja migongo ya wanajeshi wake. Baada ya kupigana kwa zaidi ya miaka kumi na sita na kutumia mabilioni ya dolari, suluhu ya kisiasa nchini Afghanistan ingali imesalia gizani. Uko uwezekano mkubwa wa Amerika kupoteza serikali ya Ashraf Ghani kuliko kuishinda Taliban.

Ripoti ya hivi majuzi ya shirika la habari la BBC imedunisha utendakazi wa serikali kibaraka wa Amerika jijini Kabul na kueleza kinaganaga kuwa ushawishi wa Taliban unapatikana kwa asilimia 70% nchini Afghanistan. Ni jambo lisiloshangaza basi, kwa Wizara ya Ulinzi ya Amerika imemzuia Mchunguzi Jumla Maalumu kwa Maridhiano ya Afghan (SIGAR) kutokana na kuchapisha takwimu juu ya kiwango cha udhibiti wa maeneo ya Taliban.

Dalili nyengine ya udhaifu wa Amerika ni rekodi yake mbaya ya kukabiliana na matamanio ya kinuklia ya Korea Kaskazini. Tangu 1994, Washington imefanya kazi kwa nguvu kuizuia Pyongyang katika jaribio lake la kupata mustawa wa nguvu za kinuklia, na ilipata pigo kubwa mnamo 2006 pindi Korea Kaskazini ilipotegua kifaa cha kinuklia na kujiunga na klabu ya nuklia. Kizingiti kilichoko sasa baina ya Korea Kaskazini na Amerika kinaonekana kuelekea njia hiyo hiyo. Mbali na tangazo lake la vikwazo zaidi na kuhatarisha kutokea kwa vita vya kinuklia na China, nafasi ya kupiga hatua ya Amerika ni ndogo. Pyongyang imechukua fursa ya upungufu wa machaguo ya Amerika na kuhujumu juhudi za Washington kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa kumwalika Raisi wa Korea Kusini kwa mazungumzo baina ya nchi mbili hizi nchini Pyongyang.

Kama itokeavyo mara nying, malengo ya kisiasa hupatikana ima kupitia vita au kupitia kuonesha nguvu za kijeshi ili kumlazimisha mpinzani kukubali suluhu. Ilhali katika kesi ya Afghanistan na Korea Kaskazini kufeli kwa Amerika katika hali zote mbili kunahisika. Umilikaji wa ubwana wa kijeshi hupelekea uhuni endapo dola kuu pekee duniani haitatafuta suluhisho la kisiasa kwa kadhia za muda mrefu. Kadhia mbili hizi za muda mrefu zinafichua kiwango cha hali ya mporomoko wa Amerika. Ikiwa Washington haitatafuta suluhisho la kisiasa la kudumu nchini Afghanistan au kuizuia Korea Kaskazini kutokana na kuunda kombora la kinuklia lenye uwezo wa kufika hadi Amerika, basi ina nafasi gani ya kuzizuia dola nyengine kuu kama China na Urusi au dola zenye nguvu kiasi yazo kama Pakistan na Uturuki kutokana kuyatishia maslahi yake.  

Pakistan inawakilisha changamoto muhimu kwa ubwana wa Amerika. Ni maarufu kuwa upinzani wa Afghan – unaojumuisha Afghan Taliban, mtandao wa Haqqani na makundi mengine ya wanamgambo – unalizunguka jeshi la Pakistan, na kila Amerika inapokuwa na hamu ya kufanya majadiliano ya mkataba wa amani na uongozi wa upinzani huu, Washington uhitaji usaidizi wa Islamabad ili hilo liweze kufanyika. Kwa Pakistan kushinikiza ushawishi kama huo juu ya upinzani wa Afghan, licha ya kupoteza kina cha mikakati yake, inazungumza kwa kinywa kipana kuhusu uwezo wa Pakistan wa kuidhuru Amerika – ikiwa tu Islamabad itachagua kufanya hivyo. Kisha kuna kadhia ya mabomu ya Pakistan – makadirio yanadokeza kuwa zana za kinuklia za nchi hii karibuni zitafikia 240. Ikiwa Korea Kaskazini tu yenye mabomu machache inaonesha kuitishia Amerika, sasa tafakari ni matatizo kiasi gani ambayo Pakistan yaweza kuisababishia Washington. Chini ya uongozi sahihi, inawezekana kikamilifu kuunganisha Pakistan na Afghanistan, kuifurusha Amerika kutoka katika eneo hili na kuzima vitisho vyote vya kawaida kutoka India kwa mikakati ya mabomu ya kutisha kutoka katika ghala lake la zana za kinuklia.     

Vile vile, Uturuki – dola isiyokuwa na nuklia – inaonyesha kuwa changamoto dhidi ya uongozi wa Kiamerika barani Ulaya. Uturuki kwa kiasi kikubwa ndio nchi ya NATO iliyo na ushawishi mkubwa juu ya bara la Ulaya, na jeshi lake laweza kuuharibu vibaya ushawishi wa Kiamerika. Kwa mujibu wa George Freidman wa Stratfor, majeshi ya Uturuki yana uwezo wa kufika Ujerumani kwa muda wa saa moja na Ufaransa kwa muda wa nusu siku bila ya kuzuiwa. Dola nyengine pekee ya NATO kando na Amerika ambayo yaweza kuisitisha Uturuki kusonga upande wa magharibi ni Uingereza.

La kusikitisha, uongozi wa kinafiki wa nchi zote hizi ndio kitu pekee kinachoizuia Pakistan na Uturuki dhidi ya kupambana na Amerika. Uongozi wenye ikhlasi unaofanya kazi chini ya kivuli cha bendera ya Kiislamu ya Khilafah utaung’oa mfumo wa Amerika katika bara hili na Ulaya, na kukaribisha mfumo mpya wa Kiislamu kwa ulimwengu. Lakini je, yuko yeyote katika wanajeshi anayeweza kutekeleza ombi hili kupitia kusimamisha Khilafah?

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَجِيبُواْ لِلّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُم لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ}

“Enyi mlioamini, muitikieni Allah na Mtume wanapokuiteni jambo la kukupeni uhai wa milele. Na jueni kwamba Allah huingia kati ya mtu na moyo wake na kwamba kwake Yeye mutakusanywa.” [8:24]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Abdul Majeed Bhatti

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:24

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu