Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ijtihadi Zinazohusiana na Mabadiliko

Tofauti Baina ya Matendo ya Dola na ya Mtu Binafsi

Baada ya Waislamu kuihisi hali mbaya waliokuwa wakiishi, utambuzi wa baadhi yao ukaanza kupata nguvu kuelekea kwenye kubadilisha ukweli huu. Maono ya mwamko juu ya msingi wa Uislamu yameanza kutambaa miongoni mwao na matokeo yake vyama vya kisiasa na vikundi vimeanza kuundwa kwa lengo la kuleta mabadiliko. Hata hivyo, vimeanza kuelekea kwenye njia tofauti na kukiuka nyingi ya njia za Hukmu za Kisheria. Tofauti hii na migongano imetokana na Ijtihadi za kimakosa walizozifikia. Baadhi yao waliona kuwa jamii ni jamii ya Kiislamu ambayo ina makosa. Kwa hivyo inahitaji marekebisho na sio mabadiliko (uhuishaji). Wao, kwa hiyo, wakaanza kufanya matendo ya kurekebisha kama kutoa usaidizi na misaada kwa masikini, mayatima na wale wenye mahitaji, kujenga maskuli, hospitali, kulingania urekebishaji wa tabia za watu, kulingania watu katika ibadati na kushikamana na Sunnah, kuandika na kuchapisha vitabu vya Kiislamu na thaqafa za Kiislamu na kuwahubiria na kuwaongoza watu kwenye haki. Wamekosea na wamewafanya wengine kukosea wakiwaweka mbali na njia ya sawa (ya mabadiliko).

Kufahamu tofauti baina ya kufanya matendo ambayo ni maalum kwa Dola kama Dola na kufanya matendo ambayo ni maalum kwa mtu binafsi kama mtu binafsi itapambanuka kuwa matendo hayo yaliotajwa hapo juu yanatokana na Ijtihadi za kimakosa ambazo hazina mahusiano na suala la msingi la Waislamu, na hatimaye hawatoweza kufikia lengo ambalo Waislamu lazima walifanyie kazi ili kulifikia, yaani kusimamisha Khilafah na kurejesha hukumu kwa kile alichoteremsha Mwenyezi Mungu (swt).

  1. II) Kufanya matendo maalum kwa Dola kama Dola:

Vyama vingi vya kisiasa, vikundi na taasisi vinawataka walinganizi (wa Da’wah) kuwaendea watu kwenye maeneo yao na kushiriki katika kazi za kufundisha wasiojua kusoma, kuwatibu wagonjwa ili wapate uzima, kuwatia nguvu wale wote waliokwama hadi waweze kusimama sawa sawa, kuwasaidia wasio ajiriwa ili wawe na kazi, kuwasaidia wenye shida hadi waweze kujisimamia wenyewe na kuweka ufahamu kwa wale walio nyuma ili wasonge mbele na kuendelea. Kwa msingi huo, wanahitajika kuweka kamati ili kuondoa kutojua kusoma na kukusanya Zakaah na kuzisambaza, na wajishughulishe kwa hayo ambayo yako ndani ya uwezo wao kama kuweka masanduku ya kukusanyia Zakaah, zahanati za ummah, hospitali za misaada na mfano wa matendo kama hayo.

Mengi ya matendo ya namna hii ni kutokana na kazi maalum za Dola na kutokana na majukumu yake kwa raia wake. Hii ni kwa sababu jukumu la kivitendo la usimamizi wa masuala ya watu katika maeneo hayo yenye mahusiano na maisha ya watu, ndani ya Dola, yanaangukia kwenye majukumu ya mtawala na sio Chama au watu binafsi. Kujiingiza kwa Chama au Jumuiya katika matendo ambayo ni majukumu ya mtawala inaonyesha kujiingiza kwenye majukumu ambayo sio yao kwa mujibu wa Sharia. Hii ni kwa upande mmoja na kwa upande mwengine inaashiria kumsaidia mtawala ambaye imedhamiriwa kuepukana naye na kuleta mabadiliko. Hii ni kwa sababu Chama kinashughulika na usimamizi ambao ni wajibu juu ya mtawala kuutekeleza ambapo watu hukosa hamasa na kutulia (kutokana na kutatuliwa shida zao), kuyapa nguvu mamlaka ya utawala na matokeo yake ni kuongeza uhai wa utawala wake. Haijahusishwa kuhusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ambaye ni kiigizo chema kwetu, kuwa alijishughulisha na tendo lolote la watawala na jukumu la mtawala wakati yupo Makkah katika kipindi cha Da’wah yake. Alipoipitia familia ya Yaasir (ra) ilipokuwa ikiteswa aliwaambia:

«صبرا ال ياسر فان موعدكم الجنة»

“Subirini enyi familia ya Yasir kwani ahadi yenu ni Pepo” (Ibn Is-haaq /Ibn Hishaam).

Yeye (saw) hakukusanya fedha kutoka kwa Masahaba (ra) kwa kutaka kuwakomboa na hakuamrisha haya kufanywa. Bali Abu Bakar (ra), miongoni mwa wengine katika Masahaba (ra), alitekeleza jambo hili lililopendekezwa kama mtu binafsi katika uwezo wake ili kupata malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). Vivyo hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) hakuweka kamati kuondoa udhalimu au umasikini kutoka kwa watu wala kutoka kwa Sahaba wake (ra) bali, aliwataka Masahaba kuwa na subra katika kukabiliana na madhara wanayokumbana nayo na kuwa imara juu ya Da’wah hadi ushindi wa Mwenyezi Mungu utakapokuja.

Makusanyo ya Zakkah na kuzisambaza, kwa mfano, ni katika matendo ya Dola na sio miongoni mwa matendo ya Chama. Kama Dola haipo, ambayo ndio chombo chenye jukumu hilo, ni wajibu juu ya kila Muislamu anayemiliki Nisaab kutoa Zakaah mwenyewe kwa wahitaji. Kamati za Zakaah haziingii chini ya Qaida ya: ‘Kile ambacho hakikamiliki bila yake, nacho ni Wajib’ kwa sababu kinakamilishwa bila ya kamati. Kitu pekee kinachohusiana na Zakaah ambacho kinaangukia chini ya qaida hii ni wajibu wa kusimamisha Dola ya Kiislamu, kwa sababu kuchukua Zakaah kutoka kwa wote wanaowajibika kutoa hakuwezi kukamilishwa bila yake. Haiwezi kusambazwa juu ya wote wanye mahitaji nayo, na wale wanaoizuia hawawezi kuadhibiwa kwa mujibu wa Sheria isipokuwa kwa kuwepo Dola ya Kiislamu.

Vivyo hivyo kuwasaidia wale wenye mahitaji, kuwatibu wagonjwa na kutoa msaada kwa masikini na mayatima na miongoni mwa matendo mengine ya aina hiyo, yote ni majukumu ya Dola na sio majukumu ya Chama au watu binafsi. Hata hivyo ikiwa mtu binafsi atatekeleza baadhi ya matendo haya bila kujihusisha kwake na Chama basi tendo lake hilo huwa ni Manduub (Sunnah) na linastahiki thawabu. Matendo haya, hata hivyo, hayaondoi wajibu wa kufanya kazi ya kusimamisha Dola ambayo ni Faradhi ambapo mtu hupata dhambi pindipo lengo halijafikiwa.

Chama au Jumuiya ambayo hufanya kazi kurejesha maisha ya Kiislamu haitakiwi kujihusisha na kujishughulisha na majukumu ya Dola na ambayo sio majukumu yake. Hii ni kwa sababu matendo ya Twariqa (Njia) ya kurejesha utaratibu wa maisha ya Kiislamu lazima ichukuliwe kutoka vyanzo vya kisheria vya Kiislamu ambavyo vinahusiana moja kwa moja na matendo ya ubebaji Da’wah kwa ajili ya kukamilisha lengo ambalo kazi yake imefanywa kuwa wajibu. Vyenginevyo, kujishughulisha kwa wabebaji Da’wah kwenye mambo yasio hakikisha lengo lake itapelekea kufeli kwake. Hii ni kwa kuwa hili ni sharti la msingi miongoni mwa masharti ya ushindi kwa ajili ya wabebaji wa Da’wah kujifunga na hukmu za Sheria juu ya Njia (Twariqa).

Mwenyezi Mungu (swt) asema,

[يَـٰأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا إِن تَنصُرُوا ٱللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ]

“Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu” [Surah Muhammad 47:7]

Kwa hiyo, Nusura yetu katika njia ya Mwenyezi Mungu (swt) inatutaka na kutuamuru tufuate maamrisho Yake (swt) kwetu na kwa namna aliyotuamrisha kuyatekeleza.

Kwa hivyo, matendo ambayo yanatakiwa kutoka kwenye Chama kwa kuyarejesha maisha ya Kiislamu sio matendo yale yanayotakiwa na kuhitajiwa na Dola, na pia sio matendo sawa na yale yanayohitajiwa kutoka kwa mtu binafsi.

II) Kutekeleza matendo ambayo ni maalum kwa mtu binafsi kama mtu binafsi: 

Baadhi ya vyama vya kisiasa vya Kiislamu na vikundi vimelenga juu ya matendo ya kibinafsi na vinalingania kwenye matendo haya, yanayojumuisha akhlaqi na misaada kwa lengo la kurejesha mwenendo wa maisha ya Kiislamu. Wanawalingania watu kwenye akhlaqi ambazo Uislamu umeziamrisha kama ukweli, uadilifu na uaminifu miongoni mwa nyengine na wanawalingania kuwa pamoja kuhusiana na ugumu wa maisha uliopo miongoni mwao. Hii ni kwa aliye tajiri atatoa msaada kwa masikini na mwenye nguvu atamsaidia dhaifu miongoni mwao. Kwa hakika hii itawapelekea kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia walioathiriwa na umasikini na kujenga shule, misikiti na hospitali.

Walizingatia kuwa jamii imeundwa na watu mmoja mmoja tu na kwa hiyo kama mtu atarekebishwa na kusahihishwa, basi jamii nayo itarekebishika na kusawazika. Wakati kiukweli ni kuwa jamii imeundika kwa watu mmoja mmoja, fikra, hisia na nidhamu na kuwa ni muhimu kubadilisha vijumuishi vya jamii kwa ujumla wake yaani watu, fikra, hisia na nidhamu.

Matendo haya hasa ambayo baadhi ya vikundi vya Kiislamu na vyama vinayatekeleza, ambayo yanaangukia katika kiwango na majukumu ya mtu binafsi au Dola, yanawakilisha matendo ambayo yapo kisheria na kuelekezwa kwa watu binafsi na kwa Dola. Hata hivyo, hayahitajiki kisheria kwa Chama au Jumuiya ambayo inafanya kazi kurejesha maisha ya Kiislamu. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) amekiwakilisha kila kiungo kwa jukumu maalum kulifanya.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

‏«كُلُّكُمْ رَاعٍ، وَكُلُّكُمْ مَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، فَالأَمِيرُ الَّذِي عَلَى النَّاسِ رَاعٍ، وَهُوَ مَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالرَّجُلُ رَاعٍ عَلَى أَهْلِ بَيْتِهِ، وَهُوَ مَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَعَبْدُ الرَّجُلِ رَاعٍ عَلَى مَالِ سَيِّدِهِ، وَهُوَ مَسْؤُولٌ عَنْهُ، أَلاَ كُلُّكُمْ رَاعٍ، وَكُلُّكُمْ مَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»

 “Kila mmoja wenu ni mchunga, na kila mmoja ataulizwa juu ya vichunga vyake. Kiongozi ni mchunga na ataulizwa juu ya raia wake. Mwanamume ni mchunga juu ya ahli zake na ataulizwa juu ya anaowachunga. Na mtumishi ni mchunga juu ya mali ya bwana wake na ataulizwa juu yake. Nyote nyinyi ni wachunga na kila mmoja ataulizwa juu ya vichunga vyake.” (Al-Bukhaari na Muslim).

Katika Hadithi hii, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema akiwa katika nafasi yake ya mkuu wa Dola:

«أَنَا أَوْلَى بِكُلِّ مُؤْمِنٍ مِنْ نَفْسِهِ مَنْ تَرَكَ مَالًا فَلِأَهْلِهِ، وَمَنْ تَرَكَ دَيْنًا أَوْ ضَيَاعًا فَإِلَيَّ وَعَلَيَّ»

“Mimi ninastahiki zaidi (kumsimamia) kila muumini kuliko nafsi yake. Hivyo mwenye kuwacha mali basi ni ya warithi wake, na mwenye kuwacha deni au watoto basi ni juu yangu. [Bukhari/Muslim na Tirmidhi)].

Kwa hivyo, kusimamia masuala ya walio masikini na wale wenye mahitaji ni jukumu la Dola. Hii hata hivyo, sio kuwataka watu kuachana na kutekeleza matendo ya kusaidia au kuwacha kujifunga na Hukmu za Kisharia kuhusiana na masuala ya wajibu na yaliopendezewa. Bali ni kumtaka kila mchunga achunge kile alichotakiwa na Mwenyezi Mungu kwake juu ya vichunga vyake (eneo la jukumu lake). Kwa namna hii hasa Muislamu akiwa katika nafasi yake kama mtu binafsi hutakiwa kuswali na kufunga, kutoa Zakaah na Sadaqa, kuwasaidia wale walio na shida na kuwasimamia mayatima miongoni mwa matendo mengineyo yanayoangukia kwenye Faradh, Manduub na Ibaaha (wajibu, ya Sunna na ya halali). Pia inatakiwa kwake kufanya kazi pamoja na Jamaa au Chama kurejesha maisha ya Kiislamu yanayoendana na kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):

[وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى ٱلْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِٱلْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ ٱلْمُنكَرِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ ٱلْمُفْلِحُون]

“Na uwe kutokana na nyinyi Ummah unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio waliofanikiwa” [Aal - Imraan 3:104]

Na kutokana na kauli ya Mtume (saw):

«ومن مات وليس في عنقه بيعة مات ميتة جاهلية»

“Na anayekufa hali ya kuwa hakuna bay’ah shingoni mwake, anakufa kifo cha kijahiliya” [Muslim].

Kwa hakika, Uislamu umefafanua matendo ya kisiasa na kifikra ambayo mtu binafsi huyatekeleza pamoja na Chama au Jamaa. Sio matendo yanayotakiwa kutoka kwake katika uwezo wake akiwa ni mtu binafsi nje ya Chama au Jamaa na sio matendo ambayo hutakiwa na Dola kutekelezwa. Kwa namna hii, kila moja ya haya yana majukumu yake na kila moja lina vichunga vyake (eneo la majukumu yake). Chama kwa hivyo, lazima kijifunge katika matendo yake kwa yale yenye kuzingatiwa kuwa yanayotokana na majukumu yake kulingana na Sharia kwa sababu kuingia kwenye matendo mengine humaanisha kuwa ni kuingia kwenye kile ambacho hakimo kwenye majukumu yake pamoja na kuwa matendo haya hayahitajiki kutoka kwake kwa mujibu wa njia ya Kisheria. Hii itakwamisha kazi ya Chama na kuigeuza kutoka kwenye njia yake ya Kisharia na kuiepusha na kazi yake muhimu na ya msingi.

Vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu (swt) hakulazimisha Chama katika nafasi yake kama Chama kinachofanya kazi kurejesha maisha ya Kiislamu, kutekeleza Huduud kama kumkata mwizi mkono au kuchapwa mijeledi na kupigwa mawe mzinifu. Yeye (swt) hakuyataka haya kutoka kwa wanachama wa Chama au watu mmoja mmoja katika Ummah kwa sababu kutekeleza Huduud ni jukumu la Dola na sio jukumu la Chama.

Hii ina maana kuwa mbebaji Da’wah anazuilika na kufungika na kutekeleza matendo yanayohusiana na kubeba Da’wah pekee. Bila shaka, anawajibika wakati akibeba Da’wah katika uwezo wake kama mtu binafsi kujifunga na Hukmu za Kisharia katika matendo yake yote na kauli ima ziwe zinahusiana na kuwa kwake msimamizi juu ya masuala ya familia, kama kuwalea watoto, kutafuta rizki, kumsaidia aliye na shida na kutoa msaada kwa masikini, au kuhusiana na kuwa kwake na tabia ya ukweli na uaminifu.

Kwa hivyo ni wajibu kwa Muislamu, vyama vya kisiasa na vikundi, kufanya kazi ya kurejesha maisha ya Kiislamu, kuchunguza, kwa namna sahihi, njia ambayo Mtume (saw) aliifuata kuhusiana na kusimamisha Dola ya Kiislamu. Lazima wafahamu maandiko ya Kisharia yanayohusiana na hili kwa ufahamu makini. Wasichanganye baina ya matendo ya Dola na matendo ya watu mmoja mmoja kwa upande mmoja, na matendo ya Chama kwa upande mwengine. Hii ni kwa sababu ili waweze kufikia mafanikio na ushindi kama ambavyo Yeye (saw) alifikia.

Kwa kuhitimisha, uhalisia ambao leo Waislamu wanaishi ndani yake, ambao unahitajika kubadilishwa, unashabihiana na uhalisia ambao Mtume (saw) alijikuta ndani yake mjini Makkah kutoka kipindi ambacho alitumilizwa na ujumbe. Kwa hali hiyo, ni muhimu kwa wabebaji Da’wah wanaofanya kazi kuleta mabadiliko kuufahamu vyema uhalisia huu. Hii ni ili waweze kuchunguza na kujifunza dalili na Hukmu za Kisharia ambazo zinatumika juu ya uhalisia huu na hivyo waweze kujifunga na njia ya Kisharia katika kazi ya kuleta mabadiliko. Hii ni kwa ajili ya kufanya kazi katika jamii kama ambavyo Mtume (saw) aliifanya alipokuwa Makkah kwa mujibu wa hatua alizopitia Yeye (saw) kama ifuatavyo: Nuqta-ul-Ibtidaa’ (Nukta Kianzio) ambayo ni hatua ya kujifunza thaqafa. Hii inafuatiwa na Nuqtat-ul-Intilaaq (Nukta ya kusonga mbele) ambayo inapelekea kwenye hatua ya Tafaa’ul (maingiliano). Hii tena inafuatiwa na Nuqtat-ul-Irtikaaz (nukta ya Nusra) ambayo hupelekea hatua ya kupata utawala.

Sio siri kwa Waislamu kuwa Hizb ut Tahrir ni kiongozi ambaye hawadanganyi watu wake, na inafanya kazi kufikia lengo lake la kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume. Inafanya kazi mchana na usiku kufikia lengo lake kwa imani thabiti isioyumba kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu (swt) ya ushindi kwa Ummah huu, mamlaka na khilafah haitofeli, na itakuja katika kipindi alichokiweka Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hakuna shaka kuwa ushindi una sababu moja, ambayo ni kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:

  [وَمَا ٱلنَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ ٱللَّهِ ٱلْعَزِيزِ ٱلْحَكِيمِ]

“Na msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikma” [Surah Aal-Imran 3:126].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Hameed bin Ahmad

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu