Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ugumba wa Kuweka Uaminifu Wetu kwa Umoja wa Mataifa

Srebrenica

Miaka 25 imepita sasa ambapo zaidi ya wavula na wanaume wa Kiislamu 8,000 kutoka Srebrenica, mji mdogo, ulio na wakaazi wengi mno, nchini Bosnia, waliuwawa katika yale yanayo onekana sasa kuwa ndio mauwaji mabaya zaidi katika ardhi ya Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Kuanguka kwa eneo la Waholanzi ambalo lilikuwa limetangazwa kuwa mojawapo ya "maeneo salama" sita yaliyopewa ulinzi na Dutchbat, kikosi cha Uholanzi kilicho pelekwa kule kama Jeshi la Ulinzi na Umoja wa Mataifa, ilikuwa ndio sura ya mwisho katika vita vya miaka minne katika ile iliyokuwa Yugoslavia.

Idadi ya watu eneo hilo iliongezeka kwa ghafla huku wakimbizi waliokuwa wametawanyika baada ya kimbunga cha ghasia katika kutafuta ruwaza ya Milosevic ya "Serbia Tukufu." Wakitafuta usalama kutokana na mashambulizi, mauwaji, kufurushwa kwa lazima, kambi za msongamano, mateso na dhulma za kimapenzi dhidi ya wanawake takriban 50,000 ambao walibakwa kwa mpangilio, kufanywa watumwa na kutungwa mimba kwa nguvu.

Mauwaji ya Srebrenica yanaonekana kuwa ndicho kitendo kibaya zaidi cha kuogofya wakati wa vita hivyo, haswa kwa kuwa yalifanyika chini ya jicho angalizi la Umoja wa Mataifa, ambao ulicheza sehemu katika kuwapokonya silaha wanaume wa Kiislamu kufuatia matakwa ya Serbia, ili kuunda "eneo-salama", waliwasaidia Waserbia katika kuwatenganisha wanaume na wanawake katika siku ya mauwaji hayo na wakawaruhusu wanaume waliokuwa wametafuta hifadhi katika uwanja wa Waholanzi kutolewa na majeshi ya Serbia wakijua fika hatma yao itakuwa ni ipi.

Kwamba Umoja wa Mataifa ulifeli vibaya mno kulinda maisha ya wanaume na wavulana 8,000 na kwamba walisalia kuwa watu waliosimama kando, huku wanawake wakidhulumiwa kwa kiasi kikubwa ndio ukweli. Ilhali tungali tunaona kwamba kila kadhia mpya inayoibuka ndani ya Ummah, Umoja wa Mataifa bado huonekana kama shirika lenye uwezo wa kutatua tatizo  

Kufeli kumoja huenda kusitosheleze kuukinaisha Ummah kwamba Umoja wa Mataifa kamwe hauwezi kutimiza dori yake, lakini, ili kupima fikra kama hiyo, hebu tutathmini msururu wa rekodi ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na Ummah huu. Hivyo kando na kufeli kwao katika kuwalinda Waislamu nchini Bosnia je, wamefanya lipi la maana katika kuwalinda Waislamu katika historia yake yote?

Palestina

Tangu uvamizi wa Palestina, Wapelestina wamekuwa wakipigana dhidi ya kile ambacho mchunguzi wa Umoja wa Mataifa aliwahi kukitaja kama "sifa zisizokubalika za ukoloni, ubaguzi wa rangi na mauwaji ya kimbari". (Richard Falk)

Leo licha ya maazimio ya Umoja wa Mataifa, "Israel" imeongeza udhibiti wake wa maeneo ya Palestina. Imelazimisha vikwanzo vyenye kulemaza juu ya Gaza na ingali inaendelea na ujenzi wake wa makao yasio halali juu ya ardhi zilizo kaliwa.

Historia imetufunza kwamba "Israel" hata mara moja haijawahi kutii azimio lolote la Umoja wa Mataifa ambalo haliko kwa manufaa yake kikamilifu. Vilevile usaidizi wa Amerika kwa "Israel" umekuwa dhahiri zaidi ikipinga azimio lolote ambalo halihifadhi maslahi ya umbile la Kiyahudi, hata vikwazo vya kinyama juu ya ukanda wa Gaza, kujenga makao yasiyo halali juu ya ardhi ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi, au kuwaweka kuzuizini watoto wa Palestina kwa ajili ya uchunguzi huku ikiwadhalilisha wafungwa kwa rai na maandamano.

Iraq

Uvamizi wa Amerika kwa Iraq mnamo 2003, ambao ulikuwa si halali na bila ya idhini ya Baraza la Usalama, waziwazi unamulika ukweli kwamba uwezo wa Umoja wa Mataifa una kikomo katika kudhibiti vitendo vya dola kuu.

Waundaji wa Baraza la Usalama walibuni kura ya turufu ili yeyote katika wanachama watano wa kudumu aweze kukataa azimio la Baraza hilo. Hivyo ikiwa "nguvu" za ulimwengu zinataka kuvamia, hakuna lolote la kuzizuia.

Katika kesi ya uvamizi wa Iraq, Amerika hata haikupiga kura ya turufu kwa azimio, bali ilitafuta idhini ambayo haikuipata.

Umoja wa Mataifa, ulipaswa kujibu kwa kuihami Iraq dhidi ya matumizi ya nguvu yasiyo halali. Badala yake ulisalia tasa huku uvamizi huo ukithibitisha kuwa ni janga la kibinadamu kwa potea kwa maisha zaidi ya 400,000.

Kashmir

Makabiliano yanayo endelea katika eneo la Kashmir inayozozaniwa yamekuwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya haki za kibinadamu katika historia, yakidhihirishwa na mauaji ya Wanton, ubakaji, kuwekwa kizuizini kwa viongozi na wanaharakati, mateso na kupotezwa kwa Wakashmir, yote haya yanafanyika huku kukiwa na maazimio mingi ya Umoja wa Mataifa juu ya kadhia hii.

Mnamo 1948, Amerika na Uingereza ziliahidi kuwa mustakbali wa Kashmir ni lazima uamuliwe na mapenzi ya watu wake. Matakwa yao ni lazima yaamuliwe kupitia kura ya maamuzi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Amerika ndio iliyokuwa mdhamini mkuu wa azimio nambari 47 lililotabanniwa na Baraza la Usalama mnamo Aprili 21, 1948 na ambalo liliundwa juu ya msingi huo usiopingika.

Badala yake Umoja wa Mataifa imetazama kama shabiki huku India ikiyachana maazimio yake juu ya Kashmir na kipeke yake ikifutilia mbali Kifungu 370 na 35-A cha kumaliza hadhi maalum ya Kashmir. India imeanzisha msako mkubwa katika Kashmir iliyo kaliwa. Amri ya kutotoka nje usiku iliyo lazimishwa na majeshi ya India bado ingalipo. Kuna uhaba mkubwa wa dawa na chakula bondeni humo. Watu wengi wanakabiliwa na baa la njaa. Wagonjwa wamenyima matibabu. Majeshi vamizi ya India yanawapiga na kuwadhalilisha watu wale wote wanaosubutu kutoka nje na yale yote ambayo Umoja wa Mataifa na dola za ulimwengu ziko tayari kufanya ni kutazama kimya kimya huku majeshi ya India yakitekeleza mauaji haya.

Yemen

Muungano unao ongozwa na Saudia, ambao unasaidiwa kijeshi na kisiasa na Imarati, Amerika, Uingereza, Ufaransa, "Israel", Misri, Bahrain, na mataifa mengine, ulianzisha vita juu ya Yemen mnamo 2015 ambavyo vimetajwa na Umoja wa Mataifa wenyewe kama "mojawapo ya maafa mabaya zaidi ya kibinadamu katika historia ya zama hizi." Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kufikia mwisho wa 2019, mapigano hayo yatakuwa yamechukua maisha ya watu 102,000. Zaidi ya hayo vita hivyo vimewaacha mamilioni bila ya makao, huku milioni 19 wakiteseka kutokana na umasikini na hatari ya baa la njaa.

Umoja wa Mataifa umefanya nini?

Hawajawataja majina wale ambao wanahusika waziwazi na maafa haya, na kihakika waliitisha suluhisho la kisiasa (mnamo 2016) ambalo litahifadhi kwa njia isiyo ya moja kwa moja maslahi ya Saudi Arabia huku likiitambua serikali mpya iliyoundwa mjini Sanaa. Sio Umoja wa Mataifa wala jamii ya kimataifa iliyotaja kuwa Saudi Arabia na Imarati ndizo vyanzo vya moja kwa moja vya maafa haya kwa kiwango mkubwa, kupitia usaidizi wa Amerika, "Israel", Uingereza, na Ufaransa.

Vilevile tangu kuzuka kwa vita nchini Yemen, imepokea fedha zaidi ya dolari bilioni 8 kutoka kwa makongamano ya wafadhili kwa ajili ya Yemen, huku watu wa Yemen wakiendelea kuteseka kutokana na umasikini, njaa na maradhi.

Rohingya

Katika ripoti moja iliyo chapishwa mwaka mmoja uliopita ikiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Kigeni wa Guatemala, Gert Rosenthal inatamatisha: katika upuzi wa kughadhabisha wa kidiplomasia wa taasisi, ambao mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa umekuwa ndani yake ni "utasa wa kufanya kazi inavyostahili pamoja na mamlaka za Myanmar, ili kugeuza mitindo miovu katika nyanja za haki za kibinadamu, na kumakinisha mitindo mizuri katika nyanja nyenginezo."

Kwa lugha nyepesi, Umoja wa Mataifa haukufanya lolote kuzuia Myanmar kutokana na kutekeleza mauwaji ya halaiki ya Rohingya wa jimbo la Rakhine.

Ghasia ambazo zilitumiwa ni za kushtua, hata hivyo hazikutarajiwa. Tafiti zimefafanua kwamba mapema tangu 2015 kampeni ya mauwaji ya halaiki tayari ilikuwa imeanza. Kwa viashiria vya wazi kwamba janga linakuja, kwa nini ulimwengu ulishindwa kuwalinda Rohinya? Hususan tunapogundua kuwa Umoja wa Mataifa uliidhinisha Jukumu la Kulinda (R2P) mnamo 2015, linalo wajibisha jamii ya kimataifa kulinda raia kutokana na mauwaji ya halaiki pindi serikali zao zinapokuwa "haziko tayari au haziwezi" kuwaweka katika usalama. R2P ilikubaliwa kutokana na hatia jumla juu ya uchinjaji wa halaiki wa raia nchini Rwanda na Bosnia na kuahidi enzi mpya ya majibu ya "hapo kwa hapo na makali" kwa mauwaji. Katika kulipata lengo hili, onyo la mapema la juhudi za kutambua viashiria vya mauwaji ya halaiki likawa ndio angazo la watekelezaji wa kimataifa pamoja na wa dola. Hadi sasa yote yaliyofanya ni kunakili ubakaji mkubwa wa magenge, mauaji – ikiwemo ya watoto wachanga na wadogo – kipigo cha kikatili na upotezaji watu unaofanywa na majeshi ya dola ya Myanmar. Na kuwataja Rohingya kuwa "watu wanaoteswa zaidi duniani."

Syria

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa kwa uchache watu 250,000 wameuwawa kati ya 2012 na 2017. Lakini, shirika hilo lilisitisha kujadidisha tarakimu zake mnamo 2015. Shirika la Kuchunga Haki za Kibinadamu la Syria linakiweka kiwango cha vifo kuwa zaidi ya 321,000, huku tathmini nyengine ikieleza kuwa mzozo huo umesababisha vifo 470,000, ima kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. 

Watu milioni tano – wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto – wamekimbia Syria, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Nchi jirani za Lebanon, Jordan na Uturuki zimeng'ang'ana kubabiliana na mojawapo ya uhamiaji mkubwa zaidi wa wakimbizi katika historia ya hivi karibuni.

Historia ndefu zaidi ya zama hizi imewekwa kwa kuzingirwa na kuchukuliwa tena eneo la mashariki ya Ghouta kutoka kwa uhalifu wa kivita dhidi ya ubinadamu uliochukua zaidi ya miaka mitano.

Takriban asilimia 85 ya Wasyria wanaishi katika umasikini, huku zaidi ya thuluthi mbili ya watu wakiwa ima ndani ya umasikini mbaya zaidi au uchochole. Zaidi ya watu 12.8 milioni nchini Syria wanahitaji usaidizi wa afya na zaidi ya milioni saba hawana usalama wa chakula huku kukiwa na ongezeko la bei na uhaba wa chakula. Familia hutumia hadi robo ya mapato yao kwa maji pekee. Baadhi ya watoto 1.75 milioni hawako shuleni.

Na sasa kwa mara nyengine tena – hata wakati ambapo serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali kwa raia wake wenyewe, Umoja wa Mataifa ulishindwa kuleta mabadiliko kwa tatizo la watu wa Syria.

Hitimisho

Orodha ya nchi ambazo Umoja wa Mataifa imefeli kulinda raia wasio na hatia ni nyingi mno kuzieleza katika makala haya, huku Sudan, Afghanistan, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Rwanda zikiwa baadhi yake tu.

Umoja wa Mataifa uliundwa mnamo 1945 kama shirika la mwavuli wa kimataifa likiwa na malengo kadhaa msingi ikiwemo kuzuia vita na kudumisha amani katika maeneo ya mizozo. Lakini, mara nyingi Umoja wa Mataifa umefeli kote duniani zaidi kwa sababu haki ya turufu iko katika milki ya nchi tano pekee. zaidi umefeli katika ulimwengu wa Kiislamu kila wakati kwani umeundwa ili kuwapa hadhi ya juu wanachama wake wa kudumu wa Baraza la Usalama. Na pindi Umoja wa Mataifa huu unapokuwa hautumikii maslahi yao, mataifa haya huenda kinyume na shirika hili – kama ilivyo fanya Amerika ilipoivamia Iraq mnamo 2003.  

Hata wanapokuwa chini kama katika eneo la Srebrenica tunaona kuwa Umoja wa Mataifa haukuwa rafiki wa Waislamu, walisimama kando na kutazama mauwaji yakiendelea, licha ya kuwa wakaazi wa Srebrenica walikataa kuondoka, chini ya imani ya kimakosa kuwa majeshi ya Umoja wa Mataifa yatawalinda, lakini hawakuwasalimisha tu wanaume na wavulana wa Srebrenica bali pia waliwapa majeshi ya Serbia zaidi ya lita 30,000 za petrol ili kuwawezesha kuwasafirisha wanaume hao na kuwazika katika makaburi ya halaiki! Hivyo hivyo inaweza kusemwa kwa usaidizi wa uvamizi wa Palestina wa kimya cha bubu juu ya Burma.

Kuyaweka kwa maneno ya Balozi wa Amerika katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, aliye zungumza mbele ya Baraza la Usalama juu ya Mashambulizi ya Kemikali nchini Syria alieleza: "Pindi Umoja wa Mataifa unapofeli mara kwa mara katika jukumu lake la kutenda kwa ujumla, kuna nyakati katika uhai wa dola ambapo tunalazimika kuchukua hatua zetu wenyewe."

Sisi pia ni lazima tutambue kwamba tunahitaji kuchukua hatua yetu wenyewe kama Ummah. Na kufahamu kuwa tunaweza tu kutegemea usaidizi wa Mwenyezi Mungu (swt) pekee na kisha usaidizi wetu sisi kwa sisi. Kama alivyo teremsha Mwenyezi Mungu (swt):

 [وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ إِلَّا تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ]

“Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa.” [TMQ 8:73]. Ni Ummah huu pekee kiujumla ndio unaoweza kuzuia Srebrenica nyengine, kuikomboa Palestina na Kashmir na kumaliza vita nchini Yemen, na sio Umoja wa Mataifa. Hii yamaanisha ni lazima tuwashinikize watawala wa Waislamu na mujtamaa za Waislamu kuachana na nidhamu za utawala zinazotumikia Wamagharibi, na kuunda nidhamu ya utawala inayomtumikia Mwenyezi Mungu (swt). 

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Office of Hizb ut Tahrir na
Yasmin Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu