Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uislamu Unaiwajibisha Dola Kutoa Huduma za Bure za Matibabu za Kiwango cha Juu

(Imetafsiriwa)

Utangulizi: Uhitaji wa Matibabu kwa Magonjwa

Kwa kuongezeka mvuto katika Dini tukufu ya Uislamu ndani ya miongo mitatu iliyopita, kumekuwa na ongezeko la uwiyano wa shauku katika miongozo ya Uislamu kuhusiana na huduma za afya. Hii inakwenda sambamba na ongezeko la shauku katika nyanja nyengine za Uislamu, kama elimu, fedha na muungano wa kisiasa wa Ummah wa Kiislamu. Shauku mpya katika huduma za afya wakati wa zama za Khilafah sio jambo jipya kiasi hicho bali ni upatikanaji wa mchanganuo, unafuu wa mamia ya miaka ya mafanikio makubwa na uvumbuzi katika nyanja za madawa na huduma za afya. Imebaki kwetu sisi kuchunguza kwa undani miongozo ya Uislamu juu ya huduma za afya.

Sunnah Tukufu Zinaagiza Dola Kusimamia Huduma za Afya

Uislamu unalazimisha uangalizi wa dola juu ya tiba na upasuaji, wakati ukiruhusu huduma za afya za kibinafsi. Huduma za afya za serikali lazima ziwe bure kwa raia wote wa dola ya Khilafah, Waislamu na wasio Waislamu. Huduma hizi lazima zipatikane, zisambazwe kwa haraka, ziwe endelevu na ziwe za ubora wa hali ya juu. Mtume (saw) alipewa tabibu kama zawadi, ambaye hakumtumia yeye tu binafsi bali alimtoa kwa Waislamu wote pamoja. Hii inathibitisha kuwa matibabu ni kwa maslahi ya wote. Pia tunaona dalili mfano wa hiyo kuhusiana na operesheni za majeraha. Katika hadithi sahihi kutoka kwa Aisha (ra) amesema,

أُصِيبَ سَعْدٌ يَوْمَ الْخَنْدَقِ رَمَاهُ رَجُلٌ مِنْ قُرَيْشٍ يُقَالُ لَهُ ابْنُ الْعَرِقَةِ رَمَاهُ فِي الأَكْحَلِ فَضَرَبَ عَلَيْهِ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم خَيْمَةً فِي الْمَسْجِدِ يَعُودُهُ مِنْ قَرِيبٍ

“Sa’ad alipata majeraha siku ya Al-Khandaq alipopigwa na mshale katikati ya mkono na Mquraysh akiitwa Ibn Al-Ariqa, na Mtume (saw) alimjengea hema ndani ya msikiti kwa uangalizi." [Bukhari na Muslim]. Inafahamika kutoka kwa kiongozi wa dola, Mtume (saw), katika kuhudhuria kwake huduma za operesheni za Sa’ad kuwa dola ya Kiislamu ina jukumu juu ya huduma hiyo. Uwekaji sawa wa mifupa, matibabu ya kuchoma na hijama yalikuwa ni matendo yakitumiwa katika vitengo vya operesheni zinazozungukia wagonjwa wa kufanyiwa operesheni ambayo yalikuwa ni sehemu ya mbele ya majeshi ya Mtume (saw) yakiwa yanaenea kwenye ukombozi wa Kiislamu.

Makhalifa Waongofu walifuata Sunnah tukufu na walihakikisha uangalizi wa dola juu ya huduma za afya. Al-Hakim amepokea katika Al-Mustadrak kutoka kwa Zayd b. Islam kutoka kwa baba yake ambaye amesema,

مرضت في زمان عمر بن الخطاب مرضاً شديداً فدعا لي عمر طبيباً فحماني حتى كنت أمص النواة من شدة الحمية

“Nilikuwa naumwa sana wakati wa Umar b. Al-Khattab na Umar alimwita tabibu kwa ajili yangu. Alinipasha kwa joto hadi kufikia kufyonza kokwa za tende kutokana na joto kali.” Katika nyakati za baadaye za Khilafah, hospitali zilidhaminiwa na wakfu za Waislamu, japokuwa fedha kutoka hazina ya serikali ilitumika kuzikarabati baadhi ya hospitali. Hospitali ziliitwa bimaristan, mara nyingi zikihusishwa na maristan, kutokana na neno la Kiajemi bimar, ‘mgonjwa’ na stan, ‘mahala.’ Wafanyakazi wakijumuisha wanafamasia na orodha ya matabibu wanaozungukia wagonjwa wanapohitajika katika muda maalum, kuchukua historia zao, kufanya uchunguzi wa kitabibu na kuamuru utumiaji wa dawa. Hospitali ya mwanzo rasmi ilijengwa Cairo baina ya 872 na 874. Hospitali ya Ahmad ibn Tulun (أحمد بن طولون) ilitibu na kutoa dawa kwa wagonjwa wote bila malipo. Ilipewa jina la Wali, mtawala wa Wilaya aliyechaguliwa na Khalifah. Ikiwa na maeneo yaliotengwa ya kuogea, maktaba zilizosheheni na sehemu ya wagonjwa wa akili, ilikuwa ni ya kiwango cha juu kwa wakati huo. Wagonjwa walihifadhiwa nguo zao za kawaida na vitu vyao vya thamani na mamlaka ya hospitali kabla ya kupatiwa nguo maalum za wodi na kulazwa.

Hospitali ya karne ya kumi na tisa ya Al-Qayrawan (ٱلْقَيْرَوَان) pia ilikuwa ni ya aina yake kwa wakati huo. Ilipewa jina la Wilaya ya Qayrawan (ولاية قيروان) Morocco (Maghreb) ambapo Wilaya hiyo ilikuwa ni sehemu ya utawala wa Khilafah. Ilikuwa na kumbi rasmi ikiwemo vyumba vya wageni, wauguzi wa kike kwa ajili ya wagonjwa wanawake, msikiti kwa ajili ya swala na kusoma, matabibu wa muda wote na timu ya Fuqaha al-Badan (baraza la wataalamu). Hili kundi la wataalamu wa tiba na shughuli zao za matibabu zinajumuisha kupiga chuku, tiba ya mifupa, na tiba ya kuchoma.

Hospitali ya Al-Adudi (العضدي) iliasisiwa mnamo 981 Miladi na mtawala wa Baghdad, Adud al-Dawlah, na ilipewa jina lake. Iliendeshwa chini ya msimamizi maarufu Abu-Bakar al-Razi. Mnamo 1284 Miladi Hospitali ya Al-Mansuri ya Cairo ilijengwa ikiwa na milango minne, kila mmoja ukiwa na chemchem katikati yake. Sultan Mamluki Qalawun alihakikisha kuwa ilikuwa ina madaktari na vifaa vya kutosha kwa kuwahudumia wagonjwa. Aliwateuwa wahudumu wa kike na kiume kwa ajili ya wagonjwa ambao wakikaa katika wodi tafauti. Vitanda vilikuwa na magodoro na maeneo maalum yalihifadhiwa. Maji ya kutiririka yalipatikana katika maeneo yote ya hospitali.

Serikali ilisimamia kwa ukaribu uendeshaji wa hospitali ikiwa ni kazi ya kimahakama ya Khilafah. Uzembe katika huduma za afya haukuwachwa kuwa chini ya madai ya mtu binafsi. Ufuatao ni ushahidi wa ufuatiliaji wa kimahakama juu ya masuala yanayohatarisha haki za raia, ambapo qadhi akiitwa Muhtasib. Mtume (saw) amesema, «لَيْسَ مِنَّا مَنْ غَشَّ» “Hayuko pamoja nasi yule anayefanya ghushi.” (imepokewa na Ahmad na Ibn Majah kutoka kwa Abu Hurayrah). Mtume (saw) pia aliwakabili wenye kufanya udanganyifu na kuwaadhibu. Wajibu wa Qadhi Muhtasib kuhusiana na huduma za afya ulijumuisha kuhakikisha kuwa vipimo sahihi vinatumika katika dozi za kitabibu, akisisitiza juu ya elimu ya usafi, akikemea majengo mabovu na kuhakikisha usambazaji wa maji safi na mambo mengine yanayohusiana nayo. 

Mafunzo na Maelekezo kwa Mujibu wa Hadithi za Mtume (saw)

Kuna vipengele viwili vya elimu ya tabibu wa Kiislamu au daktari mpasuaji. Kuwatibu wagonjwa ni jambo la ibada ambalo lina hukumu maalum za Kiislamu zinazopaswa kufundishwa katika vyuo vya tiba. Pia udaktari ni somo khususia la kitaalamu linalojumuisha sayansi msingi za tiba pamoja na utabibu.

Ni juu ya tabibu Muislamu kufahamu hukmu zinazohusiana na kazi yake, kwa kuwa zinahitajika kujulikana kwa umuhimu wake kwenye Uislamu. Zingatia kuhusu ruhusa (رُخْصَةً) kutokana na josho juu ya kichwa wakati wa majeraha ya kichwa. Abu Daud amepokea kutoka kwa Jabir (ra) akisema,

رَجْنَا فِي سَفَرٍ فَأَصَابَ رَجُلاً مِنَّا حَجَرٌ فَشَجَّهُ فِي رَأْسِهِ ثُمَّ احْتَلَمَ فَسَأَلَ أَصْحَابَهُ فَقَالَ هَلْ تَجِدُونَ لِي رُخْصَةً فِي التَّيَمُّمِ فَقَالُوا مَا نَجِدُ لَكَ رُخْصَةً وَأَنْتَ تَقْدِرُ عَلَى الْمَاءِ فَاغْتَسَلَ فَمَاتَ فَلَمَّا قَدِمْنَا عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم أُخْبِرَ بِذَلِكَ فَقَالَ ‏"‏ قَتَلُوهُ قَتَلَهُمُ اللَّهُ أَلاَّ سَأَلُوا إِذْ لَمْ يَعْلَمُوا فَإِنَّمَا شِفَاءُ الْعِيِّ السُّؤَالُ إِنَّمَا كَانَ يَكْفِيهِ أَنْ يَتَيَمَّمَ وَيَعْصِرَ‏"‏ ‏.‏ أَوْ ‏"‏يَعْصِبَ‏"‏ ‏.‏ شَكَّ مُوسَى ‏"‏عَلَى جُرْحِهِ خِرْقَةً ثُمَّ يَمْسَحَ عَلَيْهَا وَيَغْسِلَ سَائِرَ جَسَدِهِ

“Tulikuwa safarini. Mmoja wetu lilimpiga jiwe lililomjeruhi kichwa chake. Kisha akaota usingizini (akatokwa na manii). Akawauliza wenzake: Je mnanipatia mimi ruhsa ya kutayammam? Wakasema: Hatuoni ruhsa yoyote kwako kwa kuwa unaweza kutumia maji. Basi akakoga na akafariki. Tulipokwenda kwa Mtume (saw) na kuelezwa juu ya hilo akasema: Wamemuuwa; Mwenyezi Mungu atapambana nao! Kwa nini wasiulize wakati hawajui? Kwani dawa ya ujinga ni kuuliza. Ilikuwa inamtosheleza kufanya tayammum na kupangusia kwa maji au kufunga bendeji juu ya jeraha (mpokezi Musa ametia shaka); kisha apakaze juu yake na akoshe sehemu zilizobaki za mwili wake.” Katika sheria za Kiislamu, moja ya ruhusa kwa ajili ya kufanya tayammam ni kuwepo jeraha ambalo linaweza kutibuka kwa kupitisha maji ndani yake, na kupelekea kifo. Vile vile, kuna hukumu nyingi zinazohusiana na kumshughulikia mgonjwa, kama ruhusa ya kuangalia utupu kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu, uharamu wa kuwa pamoja baina ya daktari mwanamume na mgonjwa mwanamke na karaha ya kutumia kilevi katika matibabu. Hivyo, ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya kitabibu katika Khilafah, matabibu na wapasuaji wanaelimishwa katika fiqhi inayohusiana nayo.

Fiqhi hii maalum ilikuwa ni katika elimu iliowajibishwa na Dini. Kwa upande wa ubingwa wa kitaalamu, madaktari wa Kiislamu na wapasuaji walipata mafunzo na utaalamu ndani ya mazingira ya mzunguko wa hospitali. Kuwashughulikia wagonjwa, kuwaondolea madhara na kuwapatia afueni ni sababu ya malipo makubwa. Katika kutekeleza majukumu yao, madaktari Waislamu lazima wawe waangalifu juu ya visababishi, kuchunguza kwa makini sababu na athari zake, kama Maswahaba (ra) wa Mtume (saw) walivyofanya katika masuala yote ya kitaalamu. Hivyo, katika utabibu, madaktari Waislamu walizingatia miko ya ulaji, utabibu kupitia utumiaji wa virutubisho pamoja na mitishamba na madini. Walihakiki wagonjwa na kufanya ukaguzi ili kuboresha huduma za matibabu. Ilikuwa ni kupitia utaratibu wa kisayansi ambao ulienea kwa karne nyingi.

Katika sehemu moja ya jengo la Hospitali ya Al-Mansuri, daktari mkuu alipatiwa chumba kwa ajili ya kufundisha na kutoa mihadhara. Hakukuwa na vizuizi kwa idadi ya wagonjwa walioweza kutibiwa na zahanati za ndani zilitoa dawa kwa wagonjwa kwa kuchukua nyumbani. Hospitali za kufundishia zilikuwa ni msingi wa mafunzo kwa ajili ya wanafunzi wapya wa tiba kama ilivyo mara nyingi hivi leo. Miaka mia nane iliopita, hospitali hizi za mafunzo zilitoa masomo ya nadharia na vitendo kwa wanafunzi. Mafunzo yalifanyika katika vikundi na kwa mtu mmoja mmoja kama ilivyo hivi leo. Mihadhara ilifanyika katika kumbi kubwa za hospitali na mada kwa kawaida zilikuwa ni masomo kutoka katika miswada ya kitabibu na aliyekuwa akiitwa tabibu msomaji. Baada ya kusomwa, daktari mkuu au mpasuaji alipokea maswali. Wanafunzi wengi walisoma maandishi kwa madaktari maarufu na kwa kuwa karatasi zilikuwa nyingi katika ulimwengu wa Kiislamu, miswada iliyoandikwa kwa ajili ya matumizi ya kibinafsi pia ilihifadhiwa. Katika nchi za Ulaya, machapisho haya yalikuwa haba na mara chache yalimilikiwa na mwanafunzi.

Mbali ya kufundisha, mafunzo ya utabibu yaliendeshwa kwa makundi ya wanafunzi kwa kuhudhuriwa na daktari wa zamu au mpasuaji anayezungukia wodi. Wanafunzi wa masomo ya juu walifuatilia daktari akichukua historia na kuchunguza wagonjwa wakati akiweka maagizo kwao katika idara ya wagonjwa wa nje wasiolazwa hospitali. Moja ya chuo cha tiba kilikuwa katika Hospitali ya Al-Nuri Damascus. Chini ya muongozo wa daktari Abu al-Majid al-Bahili, mtawala wa karne ya kumi na mbili Nurudin ibn Zangi (1118-1174) aliianzisha hospitali. Iliitwa kwa jina lake Nurudin na aliipatia vyakula na dawa na pia idadi kubwa ya vitabu vya tiba ambavyo viliwekwa katika ukumbi maalum.

Kulikuwa na mpangilio wa kuhitimu mafunzo na tahasusi. Kama ni mfano, madaktari bingwa wa macho walitakiwa kuwa na sifa juu ya msingi wa kitabu Ten Treatises on the Eye (كتاب الأطروحات العشر للعين) kilichoandikwa na Hunayn ibn Ishaq, ambacho kinachanganua anatomia na fiziolojia ya macho pamoja na kutafsiri aina za matibabu. Tabibu katika ulimwengu wa Kiislamu alipatiwa leseni (ijazah) baada ya kumaliza elimu yake. Kama mfano, kuna maandiko yaliosainiwa na Ibn al-Nafis (amefariki 1288/687H), kuwa mwanafunzi wake, Mkristo akiitwa Shams al-Dawlah Abu al-Fadl ibn Abi al-Hasan al-Masihi, amesoma na kuhitimu tasnia ya Ibn al-Nafis. Cheti kilikuwa na maandishi ya mkono ya Ibn al-Nafis mwenyewe na kuwekwa tarehe 29 Jumada I mwaka 668 H (25 Januari 1270). Ibn Nafis alitunga “Commentary on Anatomy of the Canon” (شرح تشريح القانون) na kumpita Harvey katika kuvumbua mzunguko wa damu baina ya mapafu na moyo.

Kila maradhi (دَاء) Yana Dawa (دَوَاء), Isipokuwa Uzee (الْهَرَمُ)

Abu Daud amepokea katika Sunan yake kuwa Mtume (saw) amesema,

تَدَاوَوْا فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلاَّ وَضَعَ لَهُ دَوَاءً غَيْرَ دَاءٍ وَاحِدٍ الْهَرَمُ»‏

“Fanyeni tiba kwani Mwenyezi Mungu (swt) hakuweka maradhi ila ameweka na dawa yake, isipokuwa maradhi aina moja nayo ni uzee.”

Imam Ahmad amepokea katika Musnad yake kuwa Mtume (saw) amesema,

«إِنَّ الله لم ينزل داء إلّا أنزل شِفَاءً، عَلِمَهُ مَنْ عَلِمَهُ وَجَهِلَهُ مَنْ جَهِلَهُ»

“Hakika Mwenyezi Mungu (swt) hakuteremsha maradhi isipokuwa ameteremsha na tiba, anaielewa tiba hiyo yule mwenye kuielewa na haielewi yule asiyeielewa.” [An-Nisa’i, Ibn Majah, Al-Hakim na Ibn Hibban].

Inapopatikana tiba sahihi ya maradhi, basi maradhi hutibika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt). Baadhi ya watu wataielewa na wengine hawatoielewa. Elimu ya matibabu itafahamika kwa wataalamu ima wawe Waislamu au wasio Waislamu. Inaenea kwa aina zote za matibabu, ikiwemo miko ya ulaji, virutubisho, mitishamba, madini au chumvi chumvi na michanganyiko. Hadithi hizi zinabainisha kuwa kuna tiba kwa maradhi yote. Hivyo inatumainishwa tiba itakayopelekea kutibu maradhi, kwa Irada ya Mwenyezi Mungu (swt). Maradhi hutoka Kwake (swt) na tiba ni kutoka Kwake (swt). Ponyo (shifaa) pia ni kutoka Kwake (swt). Ponyo halipo ndani ya dawa yenyewe kwa asili yake. Ni Mwenyezi Mungu (swt), Al-Qadir, ndiye aliyeweka ndani ya tiba uwezo (qudra) wa kutibu maradhi.

Katika maelezo yake ya hadithi namna hizi, mwanachuoni wa tiba, Ibn Qayyim amesema,

فَقَدْ تَضَمَّنَتْ هَذِهِ الْأَحَادِيثُ إثْبَاتَ الْأَسْبَابِ وَالْمُسَبَّبَاتِ

“Hadithi hizi zinahakikisha kuwa kuna sababu na visababishi kwa yanayotokea duniani.” Na akaongeza,

وَلِهَذَا عَلَّقَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وسلم الشّفاء على مصادفة الدواء للداء

“Hivyo hivyo, Mtume (saw) akafungamanisha shifaa juu ya matibabu yake muwafaka.”

Hivyo, kuna hali ya maradhi na hali ya uzima. Kama maradhi yanakuwa sugu, yanaendelea miaka na miaka, basi huzingatiwa kuwa kuna kasoro katika matibabu, ima iwe katika kujikinga na madhara, lishe, miko ya ulaji au tiba. Kinachovuliwa ni mchakato wa uzee, hatua za udhaifu unaotokana na uzee, unaopatikana kwa kuzorota ufanyaji kazi wa viungo vya mwili wa mwanaadamu. Ni mchakato huu wa uzee ndio Mwenyezi Mungu (swt) ametutayarishia sisi kwa ajili ya kurejea Kwake (swt), kutuondoshea madhambi yetu na kutusafisha kwa ajili ya Aakhira. Mwenyezi Mungu (swt) atupatie subra katika uzee wetu na subra ya heshima kwa wazee wetu.

Daktari Muislamu huwafanyia tiba wagonjwa wake, kwa kutumia kila aina muwafaka ya tiba. Wakati wa zama za Khilafah, Waislamu walichunguza kwa ukaribu tiba zilizopatikana, zikiwemo tiba za Kiyunani, wakizitumia na kuziendeleza. Madaktari Waislamu wa hivi leo lazima wafanye kama hivyo. Utabibu ni fani ya kitaalamu hivyo ni lazima waelekewe wataalamu katika utabibu. Muelekeo huo huonekana pia katika masuala mengine ya kitaalamu kwenye Sunnah tukufu, kwa mfano, katika nyanja za kijeshi. Katika kila tendo ambalo maudhui yake yanahitaji ufahamu na tafakuri, Mtume (saw) ametoa kipaumbele kwa rai za wataalamu juu ya rai za watu wa kawaida, hata kama rai za watu wa kawaida zina idadi kubwa ya watoaji maoni. Dalili ya hili inaonyeshwa katika mashauriano (shura) ya Mtume (saw). Wakati Mtume (saw) alipolisimamisha jeshi la Waislamu nyuma ya kisima cha maji karibu na Badr, Al-Habab ibn ul-Munthir (ra) hakupendelea kituo hichi kwa kuwa ni mzoefu wa maeneo kama hayo na ni mtaalamu katika vita, hivyo alimwamwambia Mtume (saw):

يَا رَسُولَ اللهِ ؛ مَنْزِلٌ أَنْزَلَكَهُ اللهُ لَيْسَ لَنَا أَنْ نَتَعَدَّاهُ ، وَلَا نُقَصِّرُ عَنْهُ ، أَمْ هُوَ الرَّأْيُ وَالْحَرْبُ وَالْمَكِيدَة

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mahala hapa amekuamuru Mwenyezi Mungu na hatuwezi sisi kusonga wala kuondoka, au ni suala la rai na vita na mbinu?” Mtume (saw) akasema:

«بَلْ هُوَ الرَّأْيُ وَالْحَرْبُ وَالْمَكِيدَةُ»

“Bali ni suala la rai, vita na mbinu.” Al-Habab (ra) akaonyesha eneo jengine. Mtume (saw) na wale aliokuwa pamoja naye wakahamia na kuweka kambi, ambapo visima vya maji vikawa nyuma ya jeshi, ikiwazuilia navyo maadui. Katika hadithi hii, Mtume (saw) alitengua rai yake kwa ile ya mtaalamu, na hakutafuta rai ya Waislamu wengi. Juu ya yote, kama ingekuwa ni Wahy kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), asingeiacha rai yake.

Mafunzo kutoka Sunnah Tukufu ni kwa ajili ya kuweka sheria. Ni wajibu kufanya matayarisho ya kijeshi na ni wajibu kutoa huduma za afya. Hata hivyo, mbinu na aina maalum zinawachwa kwa wataalamu katika vitengo husika, ima iwe kwenye masuala ya kijeshi au afya. Hivyo rai za Mtume (saw) zinazohusiana na utabibu maalum haziwafungi au kuwahusu Waislamu tu, kama ilivyokuwa haikufungwa rai yake binafsi inayohusiana na eneo la kuweka kambi katika Badri. Waislamu wanaweza kuchukua kutoka kwa wasio Waislamu muda wa kwamba hazipingani na hukmu za sheria wala hazihusiani na imani za kikafiri. Kutafuta matibabu hakufungwi kwa tiba zilizotajwa tu ndani ya Quran na Sunnah, kama zilivyokuwa hazikufungwa kwenye zile zinazotangazwa na makampuni ya dawa hivi leo.

Kutafuta Matibabu Kunapendelewa na Sio Wajibu

Ni wajibu kwa serikali kutoa huduma za afya bure, lakini ni jambo linalopendelewa na sio wajibu kwa Waislamu kutafuta tiba wanapokuwa wanaumwa. Amri ya kujitibu ni kidokezo na sio wajibu. Imam Ahmad ameripoti kuwa Anas (ra) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

«إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ حَيْثُ خَلَقَ الدَّاءَ خَلَقَ الدَّوَاءَ فَتَدَاوَوْا»

“Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameumba maradhi na dawa, basi jitibuni.” Abu Dawud na Ibn Majah wamepokea kutoka kwa Usama ibn Sharik kuwa alikuwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) wakati watu walipokuja kutoka jangwani na kumuuliza: Je tutafute matibabu kwa magonjwa?” Mtume (saw) akasema,

«نَعَمْ، يَا عِبَادَ اللَّهِ تَدَاوَوْا، فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلَّا وَضَعَ لَهُ شِفَاءً»

“Ndio, enyi waja wa Mwenyezi Mungu, tafuteni tiba, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuweka maradhi isipokuwa kayawekea na tiba (shifaa).” Katika Hadithi Mtume (saw) amewaamuru watu kufanya tiba. Katika Hadithi ya pili, Mtume (saw) amewaelekeza watu kutoka jangwani kutafuta tiba, kwani Mwenyezi Mungu (swt) ametoa vyote viwili maradhi na tiba. Ashirio (khitaab) katika hadithi hizo mbili zimekuja kwa muundo wa amri. Amri inayoonyesha kutaka. Utakaji namna huo haufanyi kuwa wajibu isipokuwa iwe ni ya kukata (jaazim). Ili iwe ni ya kukata, amri itahitaji kidokezo chengine (qarina).

Katika Sunnah zilizotajwa hapo hakuna qarina inayotujulisha kuwa amri hiyo ni wajibu. Zaidi ya hivyo, kuna Hadithi nyengine zinazoonyesha kuwa inaruhusiwa kujiepusha na tiba. Hii inaonyesha kuwa amri ya kutafuta tiba katika Hadithi hizo mbili hazionyeshi uwajibu. Imam Muslim amepokea kwa njia ya Imran ibn Husayn kuwa Mtume (saw) amesema,

«يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مِنْ أُمَّتِي سَبْعُونَ أَلْفًا بِغَيْرِ حِسَابٍ، قَالُوا: مَنْ هُمْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: هُمْ الَّذِينَ لَا يَسْتَرْقُونَ، وَلَا يَتَطَيَّرُونَ، وَلَا يَكْتَوُونَ، وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ»

“Watu sabiini alfu katika Ummah wangu wataingia Peponi bila hisabu.” Wakauliza, “Ni nani hao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Ni wale wasiofanya ruqya, tatayur, kuchoma kwa moto, na wanamtegemea Mola wao.” Imam Bukhari amepokea kuwa Ibn Abbas amesema, ‘Huyu mwanamke mweusi alikuja kwa Mtume (saw) na akasema, “Mimi nina kifafa na kinaponijia huwa ninakuwa uchi, basi muombe Mwenyezi Mungu (swt) aniponyeshe.” Mtume (saw) akasema,

«إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الْجَنَّةُ، وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللَّهَ أَنْ يُعَافِيَكِ»

“Kama ukitaka, kuwa na subra (katika maradhi haya), utapata Pepo, na kama ukitaka, nitamuomba Mwenyezi Mungu akuponyeshe.” Akasema “Nitasubiri.” Kisha akasema, “Ninakuwa uchi; Niombee kwa Mwenyezi Mungu (swt) nisiwe uchi.” Mtume (saw) akamuombea Mwenyezi Mungu.’

Kwa hivyo Sunnah inaonyesha kuwa inaruhusiwa kutofanya tiba. Katika Hadithi ya mwanzo, Mtume (saw) amesema kuwa miongoni mwa watu watakaoingia Jannah bila hisabu ni wale wasiofanya ruqya au tatayur, ambayo humaanisha kutofanya tiba. Wanayawacha mambo kwa Mola wao (swt) na kumtegemea Yeye tu (swt). Istirqaa na iktiwaa ni njia za matibabu. Katika hadithi ya pili, Mtume (saw) amempa mwanamke mweusi fursa baina ya kufanya subra na kifafa chake, kwa malipo ya Pepo, au dua kwa Mwenyezi Mungu (swt) kwa tiba yake. Hii inajulisha ruhusa ya kuacha matibabu.

Kwa hivyo Sunnah zinaonyesha kuwa hakuna wajibu katika kupata tiba. Hata hivyo, kutokana na msisitizo mkubwa wa Mtume (saw) wa kufanya tiba, amri hiyo inakuwa ni mandub (jambo lililopendekezwa).

Virutubisho (غِذَاءِ) and Miiko (حِمْيَةِ)

Wakati wa zama za Mtume (saw), miongoni mwa aina tafauti za matibabu ilikuwa ni miko katika ulaji na virutubisho. Mtume (saw) aliwaelekeza Waislamu kutumia njia zote kwa kuwatibu wagonjwa. Pia, inasisitizwa kuwa kupata tiba hakufungwi tu kwa tiba katika Quran Tukufu na Sunnah. Wajibu katika Dini ni kutoa huduma za afya, lakini mbinu na njia za tiba zimeachwa kuwa katika mambo ya Duniya.

Ama kuhusu miko, Ibn Qayyim amepokea kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

«إنَّ اللَّهَ إذا أحبَّ عبدًا حماه من الدُّنيا كما يحمي أحدُكُم مريضَهُ عن الطَّعامِ والشَّرابِ»

“Hakika Mwenyezi Mungu (swt) anapompenda mja, humnyima kutokana na dunia, kama anavyomnyima mmoja wenu mgonjwa wake kutokana na chakula na kinywaji.”

Kama mfano wa miko, Mtume (saw) alishauri hili katika maradhi ya kiwambo ute cha jicho (رَمَدٌ), kuepuka tende. Imepokewa kuwa Suhaib (ra) amesema,

«قَدِمْتُ عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم وَبَيْنَ يَدَيْهِ خُبْزٌ وَتَمْرٌ فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ادْنُ فَكُلْ ‏ فَأَخَذْتُ آكُلُ مِنَ التَّمْرِ فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم تَأْكُلُ تَمْرًا وَبِكَ رَمَدٌقَالَ فَقُلْتُ إِنِّي أَمْضُغُ مِنْ نَاحِيَةٍ أُخْرَى فَتَبَسَّمَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم»

“Nilikuja kwa Mtume (saw) na mbele yake kuna mikate na tende. Mtume (saw) akasema: ’Njoo ule.’ Nikaanza kula tende. Mtume (saw) akasema: ‘Unakula tende nawe una kiwambo ute jichoni kwako?’ Nikasema: ‘Ninachakuwa kwa upande mwengine.’ Mtume (saw) akatabasamu.” (Ibn Majah).

Mtume (saw) pia alishauri miko ya ulaji kwa aliyepata afueni baada ya maradhi. Umm al-Mundhar bint Qays al-Ansariyyah amepokea,

«دَخَلَ عَلَىَّ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَمَعَهُ عَلِيٌّ عَلَيْهِ السَّلاَمُ وَعَلِيٌّ نَاقِهٌ وَلَنَا دَوَالِي مُعَلَّقَةٌ فَقَامَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَأْكُلُ مِنْهَا وَقَامَ عَلِيٌّ لِيَأْكُلَ فَطَفِقَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ لِعَلِيٍّ ‏ مَهْ إِنَّكَ نَاقِهٌ ‏‏ حَتَّى كَفَّ عَلِيٌّ عَلَيْهِ السَّلاَمُ ‏‏ قَالَتْ وَصَنَعْتُ شَعِيرًا وَسِلْقًا فَجِئْتُ بِهِ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏‏ يَا عَلِيُّ أَصِبْ مِنْ هَذَا فَهُوَ أَنْفَعُ لَكَ»

“Mtume (saw) alikuja kunizuru akiwa pamoja na Ali (ra) na alikuwa amepata afueni. Tulikuwa na tende zilizowiva zimetundikwa. Mtume (saw) akaanza kula na Ali (ra) naye akaanza kula lakini Mtume (saw) akamwambia Ali (ra) kwa kurejea rejea, simamisha (kula) Ali, kwani wewe (ndio kwanza) unapata afueni na Ali (ra) akasita. Akasema (Ummu al-Mundhar) (ra), Nikamtengenezea sha’iri na viazi nikamletea. Mtume (saw) akasema, ewe Ali, tumia hivi kwani ni vyenye manufaa zaidi kwako.” [Abu Daud].  

Mtume (saw) pia alizungumzia juu ya kutamani chakula kwa mgonjwa kuwa ni muongozo wa lishe. Ibn Majah amepokea kutoka kwa Ibn Abbas (ra) kuwa Mtume (saw) alimtembelea mtu na kumuuliza: «مَا تَشْتَهِي» “Nini unatamani?” Akasema: “Nina hamu ya mkate wa ngano.” Mtume (saw) akasema: «مَنْ كَانَ عِنْدَهُ خُبْزُ بُرٍّ فَلْيَبْعَثْ إِلَى أَخِيهِ» “Mwenye mkate wa ngano basi na amletee ndugu yake.” Kisha Mtume (saw) akasema: «إِذَا اشْتَهَى مَرِيضُ أَحَدِكُمْ شَيْئًا فَلْيُطْعِمْهُ» “Pindi mgonjwa wenu yeyote akitamani kitu basi mlisheni.” Ni muhimu kujua hapa kuwa kuna kazi imefanyika kuhusiana na masuala ya utamanifu na mahusiano yake na ukosefu wa virutubisho, wakati wa ulaji wa vitu visivyofaa katika utoto na ujauzito.

Waislamu wakati wa Khilafah waliendeleza tiba kupitia miko ya ulaji na virutubisho. Daktari wakati wa kizazi cha mwanzo, Al-Harith ibn Khaladah, ameelezea kuwa

الْحِمْيَةُ رَأْسُ الدَّوَاءِ، وَالْمَعِدَةُ بَيْتُ الدَّاءِ، وَعَوِّدُوا كُلَّ جِسْمٍ مَا اعْتَادَ

“Miko ya chakula ni kichwa cha tiba, na tumbo ni nyumba ya maradhi, na mpeni kila mtu kile ilichokizowea (katika chakula na dawa).” Ibn Qayyim ameendelea kutoa maoni,

وَقَدِ اتَّفَقَ الْأَطِبَّاءُ عَلَى أَنَّهُ مَتَى أَمْكَنَ التَّدَاوِي بِالْغِذَاءِ لَا يُعْدَلُ عَنْهُ إِلَى الدَّوَاءِ

“Matabibu wamekubaliana kuwa iwapo maradhi yataweza kutibiwa kwa virutubisho (التَّدَاوِي بِالْغِذَاءِ), dawa (الدَّوَاءِ) lazima ziepukwe.” Katika kitabu cha Ibn Qayyim kuna mlango unaitwa,

فَصْلٌ فِي هَدْيِهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي الْحِمْيَةِ

“Mlango kuhusu muongozo wa Mtume (saw) katika Miko” unaozingatia baadhi ya Hadithi.

Kuna kiwango kikubwa cha kazi iliofanywa kwa karne nyingi ndani ya kipindi cha Khilafah kuhusiana na miiko ya ulaji na matibabu kwa kutumia virutubisho. Kuna miongozo mipana kwa maradhi mengi yanayojulikana, ikiwemo maumivu ya kifua (pleurisy), mafindofindo (tonsillitis), homa ya manjano, ugonjwa wa moyo (angina), na kisukari. Zaidi ya hayo, tiba kwa kutumia virutubisho (التَّدَاوِي بِالْغِذَاءِ) ilikuwa ni sehemu ya wajibu wa madaktari, kama ilivyo miko ya ulaji. Haya ni sawa na yanaingia akilini. Madaktari ni wataalamu katika elimu ya chanzo cha magonjwa (aetiology), sayansi ya mwili na viungo (anatomy), fiziolojia, elimu ya magonjwa (pathology) na taaluma ya madawa (pharmacology). Pia madaktari ndio wanaoshuhudia maradhi makubwa ya aina mbali mbali katika mazingira ya hospitali. Kwa hivyo wapo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kumaizi wakati gani virutubisho na miko hutosheleza au wakati gani tiba rasmi hulazimika. Pia watakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutumia matibabu ya huduma za dharura.

Wakati wa utawala wa Kiislamu, tiba kwa kutumia virutubisho haikuwachwa moja kwa moja kwa wataalamu wa virutubisho na wa miko ya vyakula kwa kuwa hawakuwa na utaalamu katika matibabu ya kihospitali. Ndani ya muundo wa huduma za afya wakati wa Khilafah, jukumu la wataalamu wa virutubisho na wa miko lilikuwa ni kukamilisha na ni la pili juu ya lile la daktari. Jukumu lolote la aina hii huonekana kuwa ni la hatari kama kumtaka mtaalamu wa dawa kutoa tiba kwa mgonjwa. Kuna msemo wa Kiurdu unaonukuliwa, “neem hakeem, khatrah jaan,” wenye maana “daktari mwanagenzi ni mhatarishaji maisha.” Hekima inayoegemea uzoefu ni yenye thamani na kufadhilishwa kuliko hekima tupu.

Fikra ya virutubisho na miiko ya vyakula katika kutibu maradhi ni suala la elimu jumla ya kidunia. Wengi wananukuu “Kifanye chakula chako kiwe ndio dawa yako na dawa iwe chakula chako,” imepachikwa kimakosa kwa mtaalamu wa tiba za Kigiriki (Unani), Hippocrates. Pia kuna nukuu kutoka kwa Thomas Edison, aliye na kipaji katika fani nyingi, alisema, “Daktari wa baadaye hatotoa dawa, bali atapendelea kwa mgonjwa wake katika kuushughulikia mwili kwenye ulaji na katika sababu na kinga ya maradhi.” Hii inakwenda sambamba na ufahamu wa sasa wa tiba ambapo hatua za kulinda zitumike kabla ya kwenda kwenye matibabu. Inaelezwa na madaktari bingwa kuwa Aina ya Kisukari II inaweza kugeuzwa kwa kufuata miko, na wagonjwa wa maradhi ya figo hupata nafuu kutokana na kuacha aina fulani ya vyakula, katika kile kinachojulikana kuwa ni mlo wa figo.

Mazingatio yanakuja kwa jamii ya matabibu ya kilimwengu juu ya namna vyakula vilivyosafishwa na kuongezewa vitu vingi vinavyochangia unene, kisukari na maradhi ya moyo. Uangalifu unazingatiwa kwenye manufaa ya virutubisho ambavyo vimesheheni kwenye matunda, mbogamboga, mafuta, jamii ya kunde na njugu, kwa shukrani kubwa ya “mlo wa Mediterenia.” Mlo wa Mediterenia umekuwa ni sehemu ya utamaduni wa ulaji bora wa Waislamu wa Ash-Sham na Maghrib kwa karne nyingi.

Utumiaji wa Dawa kwa Magonjwa

Mtume (saw) akiwa kiongozi wa dola ametoa mapendekezo kwa ajili ya tiba. Aina maalum ya matibabu aliyoitaja Mtume (saw) sio sehemu ya Wahyi na inaingia ndani ya uwanja wa mambo ya kidunia yalioruhusiwa. Hivyo Waislam hawafungiki na tiba iliyotajwa katika Sirah tu.

Kwa njia ya mfano, imeelezwa kuwa Asma bint Umais amesema: “Mtume (saw) ameniambia: «بِمَاذَا كُنْتِ تَسْتَمْشِينَ» “Kitu gani unatumia kwa ajili ya kuharisha? Nilisema, ‘shubrum (mtongotongo)’ Mtume (saw) akasema: «حَارٌّ جَارٌّ» Ni imoto na ina nguvu.’ Baadaye nikatumia senna kama dawa ya kuharisha na akasema: لَوْ كَانَ شَىْءٌ يَشْفِي مِنَ الْمَوْتِ كَانَ السَّنَى» “Lau kungekuwa na kitu cha kutibu kifo, kingekuwa Senna.” (Ibn Majah). Senna glycoside, pia hujulikana kama Sennoside au Senna, ni tiba inayotumika siku hizi kutibu uyabisi wa choo na kusafisha utumbo mkubwa kabla ya upasuaji, kukiwa na ushahidi ulioenea sana kutokana na majaribio ya mwanaadamu.

Kuhusiana na fani ya taaluma ya moyo (cardiology), Sa’ad amesema kuwa Mtume (saw) amesema,

«إِنَّكَ رَجُلٌ مَفْئُودٌ ائْتِ الْحَارِثَ بْنَ كَلَدَةَ أَخَا ثَقِيفٍ فَإِنَّهُ رَجْلٌ يَتَطَبَّبُ فَلْيَأْخُذْ سَبْعَ تَمَرَاتٍ مِنْ عَجْوَةِ الْمَدِينَةِ فَلْيَجَأْهُنَّ بِنَوَاهُنَّ ثُمَّ لِيَلُدَّكَ بِهِنَّ»

“Wewe ni mwenye kusumbuliwa na maradhi ya moyo. Nenda kwa al-Harith ibn Kaladah ndugu yake Thaqif, yeye ni tabibu. Achukue tende saba za ajwah za Madina aziponde pamoja na kiini chake na azitie mdomoni mwako.” [Abu Daud]. Tende za mtende wa Ajwah (Phoenix dactylifera L.) zilikuwa zikitumika sana katika matibabu ya maradhi ya moyo, kote katika ardhi ya Khilafah.

Kuhusiana na magonjwa ya ENT (Masikio, Pua na Koo), Umm Qasis, mtoto wa Mihsan amesema kuwa Mtume (saw) amesema,

عَلاَمَ تَدْغَرْنَ أَوْلاَدَكُنَّ بِهَذَا الْعِلاَقِ عَلَيْكُنَّ بِهَذَا الْعُودِ الْهِنْدِيِّ فَإِنَّ فِيهِ سَبْعَةَ أَشْفِيَةٍ»

“Kwanini mnawatesa watoto wenu kwa kuwabinya kimeo (kwa ajili ya mafindofindo, [tonsillitis])? Tumieni mshubiri wa kihindi kwani una aina saba za tiba.” Abu Dawud amesema: Mjiti wa mshubiri anakusudia costus. Bukhari na Muslim wamepokea kuwa Mtume (saw) amesema,

«لَا تُعَذِّبُوا صِبْيَانَكُمْ بِالْغَمْزِ مِنَ الْعُذْرَةِ عَلَيْكُمْ بِالْقُسْطِ»

“Msiwaadhibu watoto wenu kwa kuwabinya kimeo (kwa ajili ya mafindofindo).” Kwa karne nyingi Waislamu wakitumia costus kwa ajili ya kutibu mafindofindo na watu wa tiba za mitishamba wa mashariki wanaendelea kutumia hadi leo.

Wakati wa zama za Khilafah, kulikuwa na utumiaji mkubwa ulioenea wa miti shamba na madini. Kulikuwa pia na utaratibu wa kusisimua wa majaribio ya mwanaadamu na uchunguzi katika hospitali za dola ya Khilafah, pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa dozi na udhibiti wa ubora. Qadhi Muhtasib akichunguza viwango vya usalama, na uzembeaji wa kitabibu lilikuwa ni kosa linalostahiki adhabu kwa sheria za Kiislamu linalohusiana na diyyah na jinaya. Mufradat (dawa moja moja) zilipendelewa zaidi kuliko Murakabaat (dawa nyingi kwa pamoja) na alama ya ubingwa wa tiba ilikuwa ni utumiaji wa tiba rahisi, wa dawa moja, baada ya kujaribiwa kinga na kutibu kwa virutubisho.

Kutokana na ulezi wa serikali na ukarimu wa watu kwa mali za wakfu, matibabu ya kimapokeo ya Waislamu yaling'ara na kuenea duniani kwa karne nyingi. Kitabu kikubwa zaidi cha kiada kwenye materia medica cha zama hizo kiliandikwa na Ibn al-Baytar, aliyezaliwa Malaga Granada mwishoni mwa karne ya kumi na mbili chini ya utawala wa Kiislamu. Kinatoa muongozo kwa mpangilio wa alfabeti wa zaidi ya dawa moja moja (mufradaat) 1,400 kutokana na uchunguzi wa Ibn al-Baytar mwenyewe pamoja na 150 kutoka kwenye marejeo ya vyanzo vilivyoandikwa.

Kwa zaidi ya milenia moja, tiba ya kuridhisha kwa maradhi ya mwili (مَرَضُ الْأَبَدَانِ) ilikuwa ni moja ya maeneo mashuhuri ya Khilafah. Kuna vitabu mbalimbali vya tiba ikiwemo sehemu ya ‘زاد المعاد في هدي خير العباد‘ “Provisions of the Hereafter in the Guidance of the Best of Servants.”

Mtunzi wa kitabu ni Ibn Al-Qayyim aliyefariki mnamo 1292 Miladi, Mwenyezi Mungu (swt) amrehemu. Kitabu kinaanza kwa sifa za rehma kwa walimwengu wote, Mtume Muhammad (saw), ikiwemo ushauri wake kuhusiana na matibabu ya maradhi mbali mbali.

Kutokana na elimu iliyokuwepo kipindi hicho, Ibn Qayyim alisisitiza,

قَوَاعِدَ طِبِّ الْأَبْدَانِ ثَلَاثَةٌ حِفْظُ الصِّحَّةِ، وَالْحِمْيَةُ عَنِ الْمُؤْذِي، وَاسْتِفْرَاغُ الْمَوَادِّ الْفَاسِدَةِ

“Misingi ya tiba ya mwili ni mitatu, kuhifadhi siha, kujikinga na vyenye kudhuru na kuondosha vitu vyenye sumu.”

Matibabu katika zama za Khilafah yalijengwa juu ya utambuzi wa sababu za magonjwa, elimu juu ya athari za mwili katika kuhimili maradhi (aspects of functional anatomy and physiology), elimu juu ya maradhi (pathology) na elimu ya madawa (pharmacology). Ibn Qayyim anaeleza,

وَأَمْرَاضُ الْمَادَّةِ أَسْبَابُهَا مَعَهَا تَمُدُّهَا، وَإِذَا كَانَ سَبَبُ الْمَرَضِ مَعَهُ، فَالنَّظَرُ فِي السَّبَبِ يَنْبَغِي أَنْ يَقَعَ أَوَّلًا، ثُمَّ فِي الْمَرَضِ ثَانِيًا، ثُمَّ فِي الدَّوَاءِ ثَالِثًا.

“Maradhi yanayosababishwa na vitu vya kushikika yanaambatana na sababu. Kwa upande wa maradhi ya kimwili, mazingatio ya sababu ni kipaumbele, ikifuatiwa na mazingatio ya maradhi, wakati mazingatio ya dawa yanakuja mwisho.”

Ibn Qayyim amezingatia pia mtazamo unaoegemea ulazima wa mtazamo wa kipimo na muongezeko. Amesema,

 وَقَدِ اتَّفَقَ الْأَطِبَّاءُ عَلَى أَنَّهُ مَتَى أَمْكَنَ التَّدَاوِي بِالْغِذَاءِ لَا يُعْدَلُ عَنْهُ إِلَى الدَّوَاءِ، وَمَتَى أَمْكَنَ بِالْبَسِيطِ لَا يُعْدَلُ عَنْهُ إِلَى الْمُرَكَّبِ “Wamewafikiana madaktari kuwa iwapo maradhi yanaweza kutibika kwa virutubisho basi dawa ziepukwe. Pia wamekubaliana kuwa endapo maradhi yanaweza kutibika kwa tiba nyepesi, tiba mchanganyiko iepukwe.” Hekima hapa ni kuepuka athari hasi za ziada au uingiliaji usiofaa au matibabu.

Ibn Qayyim amemuelezea daktari kuwa ni yule anaye epusha kile kinachomdhuru mtu anapokumbana nacho. Pia anaye epusha kile kinachomdhuru mtu anapokikosa. Daktari huondoa kutoka kwa mwanaadamu kile kinachosababisha dhara kinapozidi, na kuongezea kile kilichopungua. Daktari husaidia kuleta afya nzuri au kuihifadhi afya nzuri. Anaondoa sababu iliyopo kwa kilicho kinyume yake au mbadala, au kuondoa sababu, au kuifukuza sababu kwa kile chenye kuikinga kutokana na kupatikana kwake kupitia miko. Utaona kuwa miongozo yote hii ni kwa mujibu wa muongozo na ushauri wa Mtume (saw) kwa Matakwa ya Mwenyezi Mungu, Nguvu na Msaada Wake.”

Hitimisho: Mwenyezi Mungu (swt) Ameumba Mwili wa Mwanaadamu na Tiba ya Maradhi yake

Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu (swt), Aliyemuumba mwanaadamu katika umbo bora zaidi. Ni umbile lililojengewa hatua za kujirekebisha kwa kujilinda kutokana na maradhi. Ni umbile linalohisi kiu ili kujihifadhi na kuishiwa na maji. Ni umbile linalohisi upungufu wa virutubisho na kuhitaji chakula ili kuvijaza tena. Ni umbile linalotoa kikohozi kufukuza vitu vya madhara ilivyovuta, na kutapika kwa kutoa vitu vya madhara ulivyoviingiza. Hupata homa ili kuruhusu uondoaji wa maradhi, na kuunda usaha kudhibiti vitu vichafu badala ya kuviachia kuenea katika muundo wake. Je kwa hivyo hatuzingatii na kufikiri kwa makini juu ya kile alichotuumbia Mwenyezi Mungu (swt)?

Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu (swt), Aliyeumba madini yasiyo na idadi, mitishamba na mazao ya wanyama ambayo ni njia ya tiba kwa ajili ya umbile la mwanaadamu. Ni viumbe hivi ambavyo ni maajabu ya vilivyotengenezwa na Muundaji (as-Saani’a), Mpangaji (al-Mudabbir), Anayejua neema bora zaidi kwa ajili ya kiumbe aliyependelewa zaidi, mwanaadamu. Basi neema zipi za Mola wetu tunazikanusha?

Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu (swt), Aliyempeleka mbora wa walimwengu, Imam wa Mitume (as), Sayyidina Muhammad (saw) kuwa ni rehma kwa walimwengu wote, aliyetuhadharisha, aliyetupa bishara njema na uongofu. Ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambaye ametuletea Dini iliokamilika ambayo imeusimamisha Ummah wa Kiislamu juu ya msingi imara, ikaunyanyua kuwa Ummah bora zaidi ulioletwa kwa watu. Katika wakati wa utawala wa Kiislamu, Ummah huu uliongoza katika nyanja zote za maisha, ikiwemo tiba, ikibeba ushahidi wa utukufu wa Dini yake, ambayo ni roho ya maisha yake. Na inshaallah Uislamu utarejea ukiwa ni dola ya Khilafah na kuongoza wanaadamu kwa mujibu wa bishara za Mtume (saw).

و آخر دعوانا ان الحمد ﷲ رب العلمین

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Musab Umair – Wilayah Pakistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu