Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Masuluhisho Yaliyopendekezwa kwa Gaza ya baada ya Vita
(Imetafsiriwa)

Swali:

Huku vita vya mauaji ya halaiki vya umbile la Kiyahudi, kwa uungaji mkono muovu wa Marekani ya Magharibi, vikiendelea dhidi ya watu wa Gaza kwa zaidi ya miezi mitano, na wahanga wake kufikia zaidi ya mashahidi na majeruhi 100,000, pamoja na kuangamizwa kwa sehemu kubwa ya majengo yake, kuna mazungumzo mengi kuhusu miradi ya massuluhisho ya kile kitakachokuja baada ya vita vya Gaza na jinsi mambo yatakavyokuwa kisiasa kulingana na mipango ya dola za kikoloni zikiongozwa na Marekani. Kwa hivyo, ni nini kinachotarajiwa kutoka kwa mipango na masuluhisho haya? Je, inatarajiwa kwamba Ukingo wa Magharibi utabaki kama ulivyo na kutakuwa na uvamizi wa kijeshi wa Gaza? Au itakuwa ni dola isiyo na jeshi katika Ukingo wa Magharibi na Gaza? Au Ukingo wa Magharibi utabaki kama ulivyo na Gaza itakuwa chini ya utawala wa kimataifa na wa Kiarabu au kujitawala yenyewe kama Ukingo wa Magharibi? Je, ni lipi suluhisho sahihi? Shukran.

Jibu:

Kwanza, kabla ya kujibu maswali hayo hapo juu, tutaainisha yafuatayo:

Kwanza: Baadhi ya masuala muhimu kuhusu Palestina, Ardhi Iliyobarikiwa:

1- Inajulikana kuwa Azimio la Balfour la Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, ambalo lilijumuishwa katika barua yake ya Novemba 2, 1917 kwa Bwana Rothschild, lilijumuisha uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa kuanzishwa kwa nchi ya kitaifa ya Mayahudi huko Palestina. Ahadi hii ilikuwa katika siku za mwisho za kushindwa kwa Uthmani Khilafah katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na uhaini wa baadhi ya Waarabu na Waturuki... Miaka kadhaa kabla, Herzl, mwakilishi wa umbile la Kizayuni linaloungwa mkono na Uingereza, aliwasilisha ombi mnamo tarehe 18 Mei, 1901 kwa Khalifa wa Uthmaniyya, akijaribu wakati huo kutumia mgogoro wa kifedha ambao Uthmani Khilafah ilikuwa inaukabili kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kujaza nakisi ya Khilafah kwa kubadilishana na kuwapa ardhi huko Palestina, lakini jibu la Khalifa Abdul Hamid katika kumjibu Herzl lilikuwa jibu kali na la busara: “Siwezi kusalimisha hata shubiri moja ya ardhi ya Palestina, kwani si mali yangu, bali ni mali ya Umma wa Kiislamu. Watu wangu walipigania nchi hii na kuinywesha kwa damu yao. Mayahudi nawabakie na mamilioni yao, na ikiwa Khilafah itasambaratika siku moja, basi wanaweza kuchukua Palestina bila ya thamani, lakini nikiwa hai, hilo halitatokea...” Khalifa alikuwa na ruwaza, utambuzi, na kuona mbele. Alikuwa mukhlis katika mtazamo wake. Baada ya kuvunja Khilafah, Palestina ilitolewa kwa Mayahudi bure! Hivyo ikaanza hadithi ya kunyakuliwa kwa Palestina na kuhamishwa na kuuawa kwa watu wake, na yale ambayo Khalifa Abd al-Hamid aliyatarajia, Mwenyezi Mungu amrehemu, yalitimia. Na hivyo kufutwa kwa Khilafah (1342 H - 1924 M) kulifanyika, ambako kuliongozwa na Magharibi, ikiongozwa na Uingereza wakati huo, pamoja na wasaliti kutoka kwa Waarabu na Waturuki. Kukomeshwa huku kulikuwa utangulizi halisi wa kuundwa kwa umbile la kikatili la Kiyahudi nchini Palestina.

2- Kisha Marekani ilijihusisha baada ya Vita vya Pili vya Dunia, na kuchangia ipasavyo katika kutolewa kwa Azimio la Baraza la Usalama Na. 181 lenye kuigawanya Palestina mnamo Novemba 1947... Marekani ilianza kushindana na Uingereza na Ulaya yote katika kutabanni Uzayuni wa Kiyahudi. Biden alisema katika hotuba iliyotolewa katika mapokezi ya likizo ya White House ya Tamasha la Kiyahudi la Taa (Hanukkah): “Si lazima uwe Myahudi ili uwe Mzayuni, na mimi ni Mzayuni.” (whitehouse.gov; Al-Sharq Al-Awsat, 11/12/2023). Wakati Rais Biden wa Marekani alipozuru Tel Aviv mnamo tarehe 18/10/2023 kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, alikutana na maafisa wa huko na kusema: “Ikiwa 'Israel' haikuwepo, tungelazimika kuivumbua... 'Israel' lazima iwe tena mahali salama kwa Mayahudi.” Alisema kwamba “ataliomba Bunge la Congress la Marekani kifurushi cha msaada ambacho hakijawahi kupeanwa kwa 'Israel' wiki hii. “Hatutasimama na kutofanya chochote tena, sio leo, sio kesho, sio milele,” (Al Jazeera, 19/10/2023).

Hii inaashiria kwamba Marekani ndiyo inayopigana vita hivyo, na kwamba umbile la Kiyahudi haliwezi kuendeleza vita bila msaada wa nje, hasa uungwaji mkono usio na kikomo wa Marekani. Ni umbile kwa asili yake lisiloweza kusimama kidete lenyewe. Umbile la Kiyahudi linaashiria kushindwa kwake kwa mikono yake yenyewe kwani halina uwezo wa kupigana isipokuwa kwa kamba (msaada) kutoka kwa watu, kama Al-Qawi Al-Aziz (Mwenye Uwezo na Mwenye Nguvu) anavyosema:

[ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ]

“Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu.” [Aal-i-Imran:112].

Wameikata kamba ya Mwenyezi Mungu, na kilichobakia kwao ni kamba ya watu kutoka Marekani na Ulaya na vibaraka wao ambao ni wasaliti kutoka kwa watawala katika nchi za Kiislamu ambao hawanyooshi kidole mbele ya uvamizi wa kikatili wa Mayahudi. Bali mbora wao ni yule aliyesimama karibu na kuwahesabu mashahidi na waliojeruhiwa! Vilevile inaashiria kwamba Marekani inaliona umbile hili kama kambi yake kuu ambayo inaitumia kupigana na Umma wa Kiislamu ili kuzuia umoja wake na kusimamisha dola yake, Khilafah.

3- Umbile la Kiyahudi limeanzisha hujuma ya kikatili zaidi ya mara moja huko Gaza baada ya kujiondoa kutoka humo mnamo tarehe 15/8/2005, hadi Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa ilipotokea mnamo Oktoba 7, 2023, ambayo ilikuwa pigo kwa adui wakati mujahidina walipenya ngome zake na kuua mamia ya askari wake, hadi karibu 1,200. Walikamata idadi ya askari wake. Maadui walizindua jibu la kinyama ambalo halijawahi kushuhudiwa kwenye Gaza, ambalo limekuwa likiendelea kwa zaidi ya miezi 5. Liliharibu majengo yake mengi, likilenga hospitali, liliua wagonjwa, na kuwakanyaga kwa tinga wakiwa hai, pamoja na shule ambazo watu wa Gaza walikimbilia. Idadi ya waliokufa shahidi ilifikia zaidi ya 31,000, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, na idadi ya waliojeruhiwa ilifikia zaidi ya 70,000. Adui alifuata sera ya kunyima chakula kwa kuzuia misaada, chakula, maji na nyenzo za kimsingi kuwafikia watu ili kuwashinikiza mujahidina wawaachie wafungwa wanaowazuilia. Vita vyake vilikuwa vita vya mauaji ya halaiki kwa maana halisi ya neno hilo. Lilihimizwa kufanya hivyo kwa kuungwa mkono na nchi za Magharibi, pande zote mbili za Marekani na Ulaya, na wafuasi wao. Viongozi wa mataifa ya Magharibi walimiminika kuzuru umbile hilo ili kueleza uungaji mkono kamili kwa umbile la Kiyahudi katika vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendesha Gaza.

4-Lilishajiishwa pia na kimya cha tawala katika nchi za Kiarabu na Kiislamu. Badala ya kuyakusanya majeshi kuwanusuru watu wa Gaza, baadhi yao walilaani shambulizi la mujahidina na wakaendeleza mahusiano yao na umbile la Kiyahudi kana kwamba hakuna kitu kilichotokea, na nchi za uhalalishaji mahusiano, za zamani na mpya, ziliendeleza uhalalishaji mahusiano yao na adui, na hazikukata mafungamano na kuachana na khiyana yao ya uhalalishaji mahusiano. Hawakufuta mikataba na makubaliano na umbile la Kiyahudi, kama vile Camp David na utawala wa Misri, Wadi Araba na utawala wa Jordan, na wengine. Hiyo ni, hawakuhakikisha hata hali ya chini ya vita. Zaidi ya hayo, uhusiano wa kibiashara na baadhi ya nchi hizi haukuathiriwa na uvamizi wa kikatili wa umbile la Kiyahudi. Mnamo tarehe 11/1/2024, Waziri wa Uchukuzi wa Uturuki Abdulkadir Oraloglu alikiri kwamba (takriban meli 701 ziliondoka kutoka bandari ya Uturuki hadi 'Israel' kuanzia Oktoba 7 hadi Disemba 31, 2023, kumaanisha wastani wa takriban meli 8 kwa siku.” (Al Jazeera , 11/1/2024). Hakika, baadhi ya nchi hizi sio tu hazitangazi usaidizi kwa Gaza kwa kujibu uvamizi dhidi yake, pia hazikutangaza vita  kwa umbile la Kiyahudi kwa kuwasaidia askari wake. Umbile la Kiyahudi lililenga maeneo ya Syria na kuua askari wake wengi, lakini Iran haikutangaza vita dhidi yake!

5- Marekani inakazia kauli zake juu ya masuluhisho ya dola mbili, huku ikiwa na shauku juu ya umbile la Kiyahudi na kutetea vitendo vyake vyote vya kishenzi na kutoa uungaji mkono kwa ajili yake, lakini inahofia kwamba Marekani itapoteza kile kilichobakia katika nafasi yake ya kiakhlaki, kana kwamba ina akhlaki! Rais wake, Biden, alisema, “Hakuna kuregea nyuma katika hali halisi kama ilivyosimama Oktoba 6, hiyo ina maana Hamas haiwezi tena kuwatia hofu 'Israel'…Inamaanisha pia, pindi mgogoro huu ukiisha lazima kuwe na ruwaza ya kile kitakachofuata, na, kwa maoni yetu, lazima kiwe ni suluhisho la dola mbili…hiyo ina maanishaa kufanya juhudi kubwa kwa pande zote.” (Tovuti ya CNN, 25/10/2023). Pia alisema mnamo tarehe 12/12/2023: (“Kuna wasiwasi halisi duniani kote kwamba Marekani inapoteza kituo chake cha akhlaki… kutokana na uungaji mkono wetu kwa ‘Israel’”. (Al Jazeera, 12/12/2023)).

Hata hivyo, alisisitiza sera ya Marekani, akisema, (“Ni mstari mwekundu lakini kamwe sitaiacha Israel. Ulinzi wa Israel bado ni muhimu. Kwa hiyo hakuna mstari mwekundu (ambao kwao) nitakata silaha zote ili wasiwe na Kuba la Chuma (Iron Dome) la kulilinda."" (MSNBC Channel, 9/3/2024).

Kwa hivyo, Marekani inaunga mkono umbile la Kiyahudi licha ya mvutano katika uhusiano wa Biden na Netanyahu kutokana na ukaribu wake na Trump, mpinzani wa uchaguzi wa Biden.

6- Amerika pia inafanya kazi ya kushawishi umbile la Kiyahudi kukubali suluhisho la dola mbili kwa kuufanya utawala wa Saudia ulitambue umbile la Kiyahudi na kuwa sawazisha mahusiano nalo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan Al Saud alisema katika Mkutano wa Davos (“Saudi Arabia inaweza kuanzisha mahusiano ya amani na ‘Israel’ ikiwa kadhia ya Palestina itatatuliwa...” (The Independent, 20/1/2024)). Hapo awali, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Bin Salman alisema katika mahojiano na mtandao wa Fox News wa Marekani mnamo tarehe 21/9/2023: “Kila siku tunazidi kukaribia uhalalishaji mahusiano na ‘Israel’.” Mnamo tarehe 26/9/2023, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas alimpokea balozi wa Saudia, Nayef Al-Sudairi, katika makao makuu yake huko Ramallah, ambaye awali aliwasili Ukingo wa Magharibi kupitia kituo cha uchunguzi cha Kiyahudi, kama utangulizi wa kuhalalisha mahusiano na umbile la Kiyahudi kwa kisingizio cha kuwa balozi wa kipekee na kamishna asiye mkaaji wa Palestina na balozi mdogo mkuu huko al-Quds (Jerusalem)!

Pili: Sasa tunajibu kile kilichoelezwa katika swali kuhusu matarajio ya mipango ya Marekani na umbile la Kiyahudi baada ya kumalizika kwa Vita vya Gaza:

1- Kukabidhi Ukanda wa Gaza kwa Mamlaka ya Palestina ndani ya muundo wa suluhisho la dola mbili. Suluhisho hili linatakiwa na Marekani kwa maneno, si kwa vitendo, yaani ni kucheza na maneno. Biden anataka uondolewe nguvu za kijeshi, ikimaanisha isiwe dola huru. (Rais wa Marekani Joe Biden alisema - jana, Ijumaa - kwamba alijadili suala la suluhisho la dola mbili na Waziri Mkuu wa ‘Israel’ Benjamin Netanyahu, na kwamba Netanyahu hakupinga suluhisho hili...Biden aliongeza katika taarifa kwa waandishi wa habari, kwamba kuna idadi kadhaa ya miundo ya suluhisho la dola mbili, ikizingatiwa kuwa nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa hazina vikosi vyao vya kijeshi (Al-Jazeera 4/1/2024)). Yaani Biden inakusudia dola ya aina hizi bila vikosi vya jeshi! Hata hivyo, umbile la Kiyahudi halikubaliani hata na mpango huu wa Marekani. (Katika mkutano na waandishi wa habari uliofuatiliwa na Anadolu, Netanyahu alisisitiza kwamba Tel Aviv “inakataa katakata kuasisiwa kwa dola ya Palestina na upande mmoja” (Anadolu, 18/2/2024)). Kwa vyovyote vile, suluhisho la dola mbili lililopendekezwa na utawala wa Marekani haliwezi kutekelezwa kwa umakini bila hatua ya Marekani... na utawala wa Biden haumpi shinikizo Netanyahu na serikali yake kwa sababu ya uchaguzi ujao wa rais wa Marekani, kwa sababu Biden anahitaji kura za Mayahudi katika uchaguzi na pesa za upigaji debe wa Kiyahudi kwa ajili ya kampeni yake ya uchaguzi, hasa kwa vile mshindani wake ni Trump, ambaye anaunga mkono kwa nguvu umbile la Kiyahudi... Ama Ulaya na Uingereza, wanafuata hatua za Marekani. Ama matakwa ya watawala katika nchi za Kiislamu ya kutaka suluhisho la dola mbili, ni usaliti usiovuka kile kinachosemwa na Marekani, kuondoa nguvu za kijeshi na bila ya uhuru wa kujitawala, yaani kitu sawa na kujitawala wenyewe!

2- Umbile la Kiyahudi kuukalia tena kimabavu Ukanda wa Gaza. Waziri wa Usalama wa Kitaifa Ben Gvir na Waziri wa Uchumi Smotrich ni miongoni mwa wafuasi wenye shauku kubwa ya mpango huu. Mawaziri hawa wawili wa mrengo wa kulia wenye siasa kali wanahoji kuwa raia wa Kiyahudi, pamoja na wanajeshi wanaokalia kwa mabavu, wanapaswa kuwa ndani ya Gaza na kwamba hii ndiyo njia pekee ya kudumisha udhibiti wa Ukanda huo. (Ben Gvir, ambaye anaongoza moja ya vyama vidogo vya kitaifa katika muungano wa mrengo wa kulia wa Netanyahu, alisema katika mkutano kwamba kurejea kwa walowezi wa Kiyahudi na jeshi ndio njia pekee ya kuhakikisha kuwa shambulizi baya lililoanzishwa na wapiganaji wa Hamas dhidi ya ‘Israel mnamo 7 Oktoba halitarudiwa (Reuters, 29/1/2024)). Hata hivyo, Marekani na umma wa Kiyahudi hauungi mkono maoni haya (Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, alithibitisha mnamo Jumatano kwamba ‘Israel’ “haiwezi kukalia kimabavu” Ukanda wa Gaza, baada ya kumalizika kwa vita vinavyoendesha hivi sasa dhidi ya Hamas. Aliongeza: “Uhalisia ni kwamba kunaweza kuwa na haja ya kipindi cha mpito mwishoni mwa mzozo, lakini ni muhimu kwamba watu wa Palestina wawe kitovu cha utawala huko Gaza na katika Ukingo wa Magharibi, na hatuoni ukaliaji mpya wa kimabavu,” (Guardian; Al-Hurra, 8/11/2023). Hii ni kwa sababu ukaliaji tena wa kimabavu wa kijeshi wa Gaza utasababisha gharama kwa umbile la Kiyahudi na hasara za kijeshi na kiuchumi.

3- Hamas kuendelea kudhibiti Gaza. Marekani, Ulaya, na umbile la Kiyahudi hawataki Hamas kubaki mamlakani mjini Gaza, kwa sababu wanaamini kwamba hii itasababisha kurudiwa kwa mashambulizi ya Oktoba 7. Blinken aliwaambia waandishi wa habari jijini Tokyo: “Gaza haiwezi … kuendelea kuongozwa na Hamas; hiyo inakaribisha kurudiwa kwa tarehe 7 Oktoba,” (Stategov; Guardian, 8/11/2023). Gallant alisema, “Hamas haitadhibiti Ukanda wa Gaza baada ya vita ... Tel Aviv inajiandaa kuudhibiti kutoka kwa taasisi ya kimataifa.” (Anadolu, 18/12/2023).

4- Uhamishaji usalama katika Ukanda wa Gaza kutoka kwa jeshi la umbile la Kiyahudi kwenda kwa jeshi la kimataifa. Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa, hasa na baadhi ya wanasiasa wa Marekani ni kuwepo kwa vikosi vya kimataifa mjini Gaza kutoka nchi za Kiarabu na nchi nyenginezo...na hili lilijitokeza kwenye vyombo vya habari...

(Kwa mujibu wa Jarida la ‘Wall Street Journal’, kuzishawishi nchi za Kiarabu ambazo zimetia saini mikataba ya amani au mikataba ya kuhalalisha mahusiano na ‘Israel’ kutoa au kusimamia kikosi cha usalama cha Gaza au kuisimamia, lakini hiyo itahitaji baadhi ya nchi au mashirika kuchukua jukumu la kiutawala na kusimamia usalama. Jarida hilo linasema kuwa baadhi ya majirani wa Kiarabu wanasitasita... (Al-Hurra, 3/11/2023)). Majadiliano hayo yalirudiwa, Russia Today ilichapisha mada hii tena mnamo tarehe 4/12/2023 kama ifuatavyo: “Washington pia inaunga mkono uhamishaji wa usalama katika Ukanda wa Gaza kutoka kwa jeshi la ‘Israel’ hadi jeshi la kimataifa, labda lililoundwa na baadhi ya nchi za Kiarabu, lakini ‘Israel’ haikubaliani na mazingira ya kupeleka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa katika eneo la vita, na haina imani na uwezo wa shirika hilo la kimataifa kulinda maslahi ya ‘Israel’.

5- Kukabidhiwa utawala wa kiraia mjini Gaza kwa Wapalestina pasi na kuunganishwa na Ukingo wa Magharibi, lakini umbile la Kiyahudi litawajibika kwa usalama, kama ilivyo katika Ukingo wa Magharibi. Al Jazeera ilichapisha mnamo tarehe 27/2/2024 kwamba mnamo tarehe 23/2/2024, waziri mkuu wa umbile la Kiyahudi Benjamin Netanyahu aliwasilisha mpango wa Gaza wa “Siku Baada” kwa Baraza la Mawaziri la Masuala ya Usalama na Kisiasa. (Mpango huo uliowasilishwa na Benjamin Netanyahu kwa wajumbe wa serikali yake ulijumuisha maelezo mengi kuhusu mustakabali wa Ukanda wa Gaza. Moja ya vipengele vyake muhimu katika uwanja wa usalama ni: ‘Israel’ inadumisha uhuru wa kijeshi na hatua za usalama katika maeneo yote ya Ukanda wa huo bila vikwazo vya muda, huku ikianzisha ukanda wa usalama ndani ya Ukanda wa Gaza kwenye mipaka yake na Palestina inayokaliwa kwa mabavu mwaka 1948... Aidha, 'Israel' itaupokonya silaha Ukanda wa Gaza, na kuunyang’anya uwezo wowote wa kijeshi, isipokuwa kile kinachohitajika kudumisha usalama wa umma ...)

6- Kwa kuzingatia uwezekano wa hapo awali wa mipango ya Wamarekani na Mayahudi, uwezekano mkubwa wa kile wanachopanga kutekeleza ni kile kilichotajwa katika nukta (5) hapo juu; Gaza isiyounganishwa na Ukingo wa Magharibi, bali taratibu za usalama na kijeshi ndani yake ni sawia: (‘Israel’ itadumisha uhuru wa kijeshi na hatua za usalama katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza bila kizuizi cha wakati) haswa kwa vile Mayahudi wanatekeleza mpango huu huu katika Ukingo wa Magharibi. Iliripotiwa kuwa Netanyahu aliwasilisha mpango huu kwa maafisa wa Marekani na walionekana kuwa na idhini nao (ilidaiwa kuwa Netanyahu alihakikisha kwamba mpango alioutayarisha unaambatana na mpango wa Marekani wa suluhisho la kudumu katika Mashariki ya Kati, na kwamba Marekani ilishauriwa kuhusu mpango huo kupitia kwa Waziri wa Masuala ya Kimkakati, Ron Dermer, mjumbe wa baraza dogo la mawaziri la vita vya ‘Israel’, ambalo lina uhusiano wa karibu na Washington (NTV, 31/1/2024), yaani kwamba Marekani ilifahamu mpango wa Netanyahu mapema.

Ama kuhusu kile ambacho Biden alirudia kauli yake kuhusu suluhisho la dola mbili, sio tofauti sana. Badala yake, kama ilivyoelezwa katika taarifa yake ya awali, katika nukta (1), ambayo ni (Biden aliongeza, katika taarifa kwa waandishi wa habari, kwamba kuna aina kadhaa za suluhisho la dola mbili, akibainisha kuwa nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa hazina vikosi vyao wenyewe... (Al Jazeera, 4/1/2024)). Anamaanisha uondoaji wake wa nguvu za kijeshi, na wala hana pingamizi yoyote kwa suluhisho la dola mbili kutanguliwa na hatua ya mpito, kama katika kauli yake, katika nukta ya (2): (“Uhalisia ni kwamba kunaweza kuwa na haja ya kipindi fulani cha mpito mwisho wa mzozo…” (Guardian; Al Hurra, 8/11/2023)).

Tatu: Suluhisho sahihi la Shariah ambalo lazima litekelezwe:

1- Baada ya kuzingatia hayo hapo juu, inaonekana kutoka kwa mipango ya Marekani na dola ya Kiyahudi, kwamba wanapanga kufanya Ukingo wa Magharibi na Gaza ziondolewe nguvu za kijeshi na mamlaka ya usalama ndani yake iwe ni ya Mayahudi. Ima hiyo iwe ni chini ya jina la dola moja, yaani kwa kuziunganisha, hata kama hii itakuwa katika hatua kama Marekani inavyotaka, yaani, Ukingo wa Magharibi ubaki kutengwa na Gaza katika awamu ya mpito, na kisha Gaza iunganishwe na Ukingo wa Magharibi bila nguvu ya kijeshi. Au, kama dola ya Kiyahudi inavyotaka, kwa Gaza kubaki kutengwa na Ukingo wa Magharibi tangu mwanzo na mwisho, bila nguvu za kijeshi, na mamlaka halisi ndani yao iwe ni ya umbile la Kiyahudi. Ni wazi kutokana na hili kwamba wanachopanga Marekani na Mayahudi ni sumu na khiyana kwa Mwenyezi Mungu, Mtume Wake, na Waumini. Ingawa si ajabu kwamba umbile la Kiyahudi na Marekani wanapanga kwa ajili hiyo, kwani wao ni adui, lakini cha ajabu ni kwamba hakuna hata mmoja wa watawala katika nchi za Kiislamu anayechukua hatua, hasa wale wa eneo la Palestina, kuyahamasisha majeshi yao kuinusuru Gaza, watu wake, Al-Aqsa, na viunga vyake, na kuling'oa umbile la Kiyahudi na kisha kuiregesha Palestina yote kwa watu wake. Je, yule anayeikalia kwa mabavu ardhi ya Kiislamu na akawatoa watu wake humo hastahiki kupigwa vita na majeshi ya Waislamu na kufukuzwa humo kama walivyowafukuza watu wake?

[وَاقْتُلُوهُمْ حَيْثُ ثَقِفْتُمُوهُمْ وَأَخْرِجُوهُمْ مِنْ حَيْثُ أَخْرَجُوكُمْ]

“Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote walipo kutoeni; [Al-Baqara: 191].

Je, watawala wanawezaje kutotambua hili?! Bali masaibu yao yamewazonga, kwa kuwa kujisalimisha kwao ni kwa wakoloni makafiri, hasa Marekani, hawakatai amri zake zozote ili kuhifadhi viti vyao vibovu vya utawala.

[قَاتَلَهُمُ اللهُ أَنَّى يُؤْفَكُون]

“Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki?” [Al-Munafiqun: 4]

2- Vita hivi vimefichua mambo mawili muhimu: la kwanza ni udhaifu na udhalilifu wa Mayahudi, kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyowataja katika Kitabu chake.

[ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ]

“Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu.” [Aal-i-Imran:112].

Walikata kamba ya Mwenyezi Mungu baada ya Mitume wao, na hakuna kilichobakia kwao isipokuwa kamba ya watu, Marekani na wafuasi wake. Watu wa aina hii sio watu wa vita au kustahili ushindi. Pili ni usaliti wa watawala katika nchi za Kiislamu. Wanatazama kinachoendelea. Mbora miongoni mwao ni yule anayehesabu idadi ya mashahidi na waliojeruhiwa.

[صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَرْجِعُونَ]

“Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.” [Al-Baqara: 18]

Mambo haya mawili yanapaswa kuwasukuma wenye ikhlasi na watu wenye nguvu katika majeshi ya Waislamu kutangaza uhamasishaji jumla ili kutimiza wajibu wa Mwenyezi Mungu wa kupigana na Mayahudi wanaoikalia kwa mabavu Palestina.

[وَلَا تَهِنُوا فِي ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ إِنْ تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللهِ مَا لَا يَرْجُونَ]

“Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui. Ikiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji kwa Mwenyezi Mungu wasio yataraji wao.” [An-Nisa: 104].

Hivyo basi, muliondolee mbali umbile lao, kwani wao ni duni zaidi kwa Mwenyezi Mungu (swt) kuliko kushinda katika vita, na hapo ndipo itatimia ahadi ya Mwenyezi Mungu.

[فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ لِيَسُوءُوا وُجُوهَكُمْ وَلِيَدْخُلُوا الْمَسْجِدَ كَمَا دَخَلُوهُ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَلِيُتَبِّرُوا مَا عَلَوْا تَتْبِيراً]

“Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa.” [Al-Isra: 7].

Basi kimbilieni kuwanusuru ndugu zenu wa Gaza, na endapo tawala dhalimu katika nchi za Kiislamu zitasimama dhidi yenu, basi ziondoeni kwa njia zote... na musimamishe utawala wa Mwenyezi Mungu badala yake, Khilafah kwa njia ya Utume, katika kutimiza bishara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ، ثُمَّ سَكَتَ» “Kisha utakuwepo utawala wa kutenza nguvu, utakuwepo kwa muda atakao Mweyezi Mungu uwepo kisha atauondoa atakapo kuuondoa. Kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume.’ Kisha yeye (saw) akanyamaza.” [Musnad ya Imam Ahmad]

Kisha Khalifa, wasaidizi wake, na wanajeshi wa Uislamu, kuanzia cheo cha juu kabisa hadi cheo cha chini kabisa, watatoka kwenye ushindi hadi ushindi, wakiimba “Allahu Akbar” na Ummah ukiimba “Allahu Akbar” pamoja nao, wenye nguvu kwa msaada wa Mola wao Mlezi na wenye izza kwa Dini yao, hivyo hakuna adui atakayesubutu kuasisi umbile katika ardhi ya Uislamu.

[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]

“Na siku hiyo Waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum: 4-5].

12 Ramadhan 1445 H

22/3/2024 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu