Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Uhalisia wa Yaliyotokea na Yanayotokea Aden!
(Imetafsiriwa)

Swali:

Ni yapi yaliyotokea na yanayotokea mjini Aden? Ni vipi kunakuwepo vita baina ya Baraza la Al-Zubaidi na serikali ya Hadi, ijapo kuwa Al-Zubaidi alikuwa ni gavana wa Aden aliye teuliwa na Hadi, na baada ya kutimuliwa, alibakia mjini Aden pasi na serikali ya Hadi kuchukua hatua yoyote dhidi yake, bali alikuwa akiyakusanya majeshi yake mbele ya macho na masikio serikali hiyo?! Na nini kinacho tarajiwa sasa ambapo Baraza la Mpito limeichukua Aden? Shukran na heshima ni kwako.

Jibu:

Kwa jibu lililo wazi ni muhimu kutathmini yafuatayo:

Kwanza, tangu mwanzoni mwa Oparesheni 'Kimbunga Kikali' (Decisive Storm), Uingereza ilitambua kuwa uingiliaji kati wa Saudi Arabia chini ya jina Opaeresheni Kimbunga Kikali (Decisive Storm), pamoja na oparesheni za angani, kihakika haikuwa na lengo la kuwamaliza Mahouthi. Vyenginevyo, wangekuwa wametumia majeshi ya nchi kavu. Lakini ilikuwa ni kuwaonyesha Mahouthi kama watetezi wa Yemen mbele ya ndege za kivita, hivyo basi kuonekana kama wanao nyanyaswa na, wakati huo huo, kama mashujaa ili kupata umaarufu wa kukubalika, na kupata rai jumla, na kisha kuwahusisha katika serikali wakiwa na hisa kamili katika utawala wa Yemen. Baada ya kuwa tu kabila katika eneo la Saada, sasa wawekuwa mahasimu wa serikali katika Yemen nzima! Kwa kuwa Uingereza ilijua hili, iliihusisha Imarati katika muungano wa kimbunga cha Saudi Arabia ili kutoa nafasi kwa Imarati kukabiliana kihakika na Mahouthi na sio kwa uwepo tu. Uingereza hivyo basi ilianza kuisukuma Imarati kunali vitu viwili:  

Lengo la kwanza: ni kutafuta badali ya Hadi, kwani anakaribia kuwa mfungwa nchini Saudi Arabia na hana usaidizi. Hivyo Uingereza ilitaka kutafuta badali ya Hadi mjjini Aden ili awe msaidizi wake na sio mfungwa nchini Saudi Arabia. Kwa sababu hii, Imarati ilipata badali katika hatua za kufuatana. Kulikuwa na Harakati ya Kusini (Al-Hirak) ambayo ilijitangaza rasmi eneo la kusini mwa Yemen mnamo 2007 ikiongozwa na mwanaharakati wa upinzani Hassan Baoum anaye nasibishwa na Marekani na kuungwa mkono na Iran. Uingereza ilihofishwa na harakati zake, lakini hofu hii ilifikia kileleni mwake baada ya kifo cha Salih, ambapo ushawishi wa Uingereza ulififia baada ya kufaulu kwa Mahouthi kupanua ushawishi wao kaskazini. Hivyo basi ilianza kuzingatia kwa makini kuwa na nguvu kusini, kama karata ya shinikizo ambayo ingeiwezesha kuwepo ndani ya utawala wa Yemen, endapo haitaweza angaa kuwa sehemu ya utawala kusini. Hivyo basi, ilianza kufikiri kwa makini kuhusu kumakinisha ushawishi wake kusini, hususan kwa kuwa haikumtegemea Hadi pekee kwa misingi kuwa Saudi Arabia inamdhibiti. Hivyo basi Uingereza ilikuwa na hamu katika jambo hili kupitia Imarati ili kupenya katika Harakati asili ya Kusini au kuitelekeza kupitia kuunda harakati mpya kuongoza katika uwanja huo, na kisha ikaangazia kupitia Imarati na wafuasi wake kutafuta harakati kusini sambamba na mrengo wa Baoum ili kuipiku katika lengo la kusini; walipata kile walichokuwa wakikitafuta katika Aidarous Al-Zubaidi. Ni mmoja wapo wa viongozi wanaojulikana katika Harakati ya Kusini, na kujulikana kwa ukaribu wake na kambi ya Uingereza. Aliteuliwa na Raisi Hadi mnamo 7/12/2015 kama gavana wa Aden, miezi baada ya kuanzishwa kwa (oparesheni) Kimbunga Kikali cha Saudia (mnamo Machi 2015).   

Hii ilikuwa ni ishara kubwa ya uaminifu wa vibaraka wa Uingereza kwake. Aidarous Al-Zubaidi alizungukwa na hisia kubwa mjini Aden. Alikuwa gavana wa mji huo aliye fanikiwa aliye rudisha umeme huko, kuyafurusha magenge ya silaha na kupigana na Mahouthi. Alivutia makini kama utambulisho muhimu wa kisiasa kusini aliye shindana na uongozi maarufu wa Hassan Baoum katika Harakati ya Kusini. Kijeshi, Aidarous Al-Zubaidi anamtegemea Hani bin Brek, muasisi wa majeshi ya Ukanda wa Kusini, ambaye anatajwa pakubwa kama mtu wa Imarati eneo la kusini [na aliasisi yale yanayo itwa majeshi ya "ukanda wa usalama", wanamgambo wanaoungwa mkono na Imarati kusini mwa Yemen… (Sasa Post, 2/11/2017)]. Na hivyo Al-Zubaidi na Brek walikuwa na ushawishi mkubwa kusini, lakini kwa kuwa walikuwa katika serikali ya Hadi na utiifu wao umefichulia kuwa kwa Uingereza, na si maarufu katika wito wa Harakati ya Kusini. Hatua ya kwanza ilikuwa kuwatoa katika serikali ya Hadi kwa njia inayo waonyesha kuwemo ndani ya mzozo mkali, hususan Al-Zubaidi, pamoja na kambi ya Hadi, ili wakaazi wa kusini wakusanyike nyuma yao/yake kuunda Harakati mpya ya Kusini, na hili ndilo lililo fanyika. Mnamo Aprili 27/4/2017, raisi wa Yemen alitoa amri ya kumtimua Aidarous Al-Zubaidi, gavana wa Aden, na waziri wa serikali, Hani bin Brek, huku Hani akiagizwa kufanyiwa uchunguzi. Maelfu ya Wayemeni walishiriki katika maandamano katika mji ulio kusini wa Aden wakiyashutumu maamuzi ya Hadi. Kisha Al-Zubaidi akatangaza uraisi wake wa muundo wa Baraza la Mpito la Kusini katika mji wa Aden mnamo 11/5/2017, na kwamba Hani bin Brek atakuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo lililo na wanachama 26. Hivyo basi, Uingereza kupitia Imarati, iliunda badali ya serikali ya Hadi, yaani Baraza la Mpito ili kulitumia wakati wake utakapo wadia. Hivyo alibakia Aden na ana nguvu kubwa inayo lindwa na jeshi la Imarati.

Lengo la Pili: Kuikomboa Hodeidah kutoka mikononi wa Mahouthi

A- Imarati iliingia Yemen kupitia nchi kavu na angani kwa sababu vita vya angani pekee havingemaliza vita ardhini isipokuwa kwa uingiliaji kati ardhini. Hivyo iliyasukuma majeshi yake na wasaidizi wake katika Hodeidah. Ilikaribia kuichukua lau si kizuizi cha Marekani kwa kisingizio cha msaada wa kibinadamu. Ama ni kwa nini kuna maslahi katika Hodeidah, ni kwa sababu Uingereza inajua kwamba nguvu ya Mahouthi ni usaidizi wa Iran. Baada ya kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Sana'a na kudhibitiwa kwa bandari za kusini, bandari mpya ya Hodeidah ndio njia pekee kwa Iran kutuma usaidizi wake kwa Mahouthi. Hivyo basi, Imarati ilikwenda Hodeidah kuidhibiti, Mahouthi wakakabiliwa na hatari kubwa ya kukaribia kutekwa kwa Hodeidah na bandari yake na majeshi yanayo ungwa mkono na Imarati, yalipokuwa yanakaribia pambizoni mwake. Hivyo basi, vita vya Hodeidah na maono ya Imarati na wanamgambo wake ya kuchukua udhibiti wa bandari yake mpya ilikuwa ndio hatari kubwa kwa utawala wa Mahouthi nchini Yemen. Hivyo basi Mahouthi wakachangamsha majeshi yake yote ili kuzuia hili kutokea, na Marekani ikasajili maafisa wake kulilia hali ya kibinadamu nchini Yemen, na kwamba bandari ya Hodeidah ndio njia ya kuzuia baa la nja nchini Yemen. Imarati na washirika wake wa kieneo walikuwa wakisubiri fursa za kimataifa kuanzisha mashambulizi na kukamilisha udhibiti wa Hodeidah baada ya kufika pambizoni mwake. Marekani ilikuwa na wasiwasi zaidi kuhusu kuzuia shambulizi la Imarati juu ya Hodeidah, kwa sababu iwapo Hodeidah itawaponyoka mkono Mahouthi, hili litaiingiza Marekani katika tatizo!   

B- Kisha ikawa ni mauaji katili ya mwanahabari wa Kisaudi Khashoggi yaliyo fanyika jijini Istanbul. Yamesababisha hisia kali katika mazingira ya kimataifa dhidi ya Saudi Arabia na Trump vilevile kwa ajili ya kuitetea kwake Saudi Arabia. Marekani ilitaka kuipurukusha hali ya kimataifa kwa kadhia inayo finika mada ya Khashoggi na kuiondolea fedheha Saudi Arabia na utawala wa Trump, hivyo wakachagua Yemen. Kisha Bunge la Seneti la Marekani likapiga kura kumaliza usaidizi wa kijeshi wa Marekani kwa vita nchini Yemen [na katika hatua ya kihistoria maseneta walipiga kura 56 dhidi ya 41 kumaliza usaidizi wa kijeshi kwa kampeni inayoongozwa na Saudia nchini Yemen… (Reuters 14/12/2018)]. Kutokana na hili na ili kuondoa fedheha ya kimataifa kwa Saudi Arabia na kuziba kadhia ya mwanahabari wa Kisaudi, Marekani ilitoa wito wa kusitishwa vita nchini Yemen ndani ya siku 30. [Waziri wa Ulinzi James Mattis alitoa wito kwa pande zote za mzozo wa Yemen kusitisha vita ndani ya siku 30, na kuingia katika majadiliano ya umakinifu ili kumaliza vita nchini humo. Alisisitiza kuwa: "pande zinazo pigana nchini Yemen ni lazima zisonge mbele kuelekea juhudi za amani." Na kuendelea: "Tunahitaji kufanya hivi ndani ya siku 30, na nadhani kuwa Saudi Arabia na Imarati wako tayari kuchukua hatua katika kadhia hii." ((Gulf Online 31/10/2018)].

C- Hii ilifuatiwa na makubaliano ya Sweden ili kutatua kadhia ya Yemen, na Uingereza ilijua kuwa makubaliano hayo yanasimamiwa na Marekani kwa manufaa ya Mahouthi. Wenye kujadiliana ni Mahouthi na Hadi aliye shindwa nguvu na Saudi Arabia. Imeripotiwa kuwa ujumbe wa serikali ulikuwa na rai ya kutotia saini makubaliano hayo kwa sababu hayataji kuondoka kwa Mahouthi Hodeidah. Lakini Hadi alikubali chini ya shinikizo kutoka Saudi Arabia! [Duru za Al-Jazeera zilisema kuwa ujumbe wa serikali uliwasilisha waraka kwa Hadi, "anayeishi jijini Riyadh", unao pendekeza kutotiwa saini mkataba huo kwa sababu hautaji waziwazi kuondoka kwa Mahouthi kutoka katika mji wa Hodeidah, na bandari yake, lakini raisi wa Yemen alielekezwa kuutia saini baada ya shinikizo kali kutoka Saudi Arabia katika masaa kadhaa yaliyopita, kwa mujibu wa duru … (Aljazeera.net 13/12/2018)]. Bila shaka Marekani iliyakaribisha waziwazi makubaliano hayo, [Waziri wa Kigeni wa Marekani, Pompeo, aliyakaribisha makubaliano hayo, akisema kuwa "amani inawezekana nchini Yemen" … (BBC 14/12/2018)]. Hamu ya Marekani ilikuwa ni kufanyiwakazi makubaliano hayo pasina Mahouthi kujiondoa kutoka Hodeidah; ilidhani hili lingewezekana kwa sababu pande zinazo jadiliana ziko chini ya udhibiti wake: Mahouthi na Hadi aliye shindwa nguvu na Saudi Arabia.

Pili, Uingereza iligundua kuwa muda umewadia kwa badali ya Hadi kutekeleza dori yake. Endapo Marekani itafaulu katika kuwamakisha Mahouthi kaskazini, badali ya Uingereza kwa Hadi itawekwa kusini, ikiifanya Marekani na Saudia Arabia kushindwa kutafuta suluhisho pamoja na Mahouthi chini ya kibaraka wa Uingereza anaye dhibitiwa na Saudi Arabia inayo fungamanishwa na Marekani, bali itapata mbele yake harakati imara ya Kiingereza eneo la kusini inayoifanyia kazi Uingereza pasina kudhibitiwa na Saudi Arabia. Hivyo Uingereza itakuwa sehemu ya suluhisho lolote kwa kadhia ya Yemen. Hivyo, badali ilitayarishwa, yaani baraza la Al-Zubaidi, kuanza matukio ya Aden:

1- Matukio ya hivi karibuni mjini Aden yamekuwa yakienda kwa kasi! Taharuki zilianza baina ya Baraza la Mpito la Kusini na majeshi ya serikali halali mjini Aden, na kisha ghasia kuzuka baina ya "ukanda wa usalama" na majeshi ya serikali: yote yalianza mnamo 7/8/2019 na Jumamosi jioni 10/8/2019 yaani baada ya siku nne tu [Baraza la Mpito la Kusini nchini Yemen lilitangaza mnamo Jumamosi jioni udhibiti wake wa kasri la raisi la Ma'ashiq mjini Aden baada ya siku nne za ghasia … (: France 24 mnamo 10/8/2019)]. Kambi na vitengo vyenginevyo mjini Aden pia zilianguka ndani ya udhibiti wao!

2- Kilicho saidia kutatua matukio haya kwa haraka "ndani ya siku nne" ni kuwa serikali ya Hadi na taasisi zake na Rais na Makau wa Rais ni watiifu kwa Uingereza; waliendesha dori iliyo agizwa Baraza hilo na Uingereza! Hivyo, Baraza hilo liliweza kutatua jambo hili kwa haraka, na baadhi ya viashiria vyaonyesha hili:

A- [Afisa katika majeshi ya ukanda wa usalama alisema, "Tulikabidhiwa kasri la Ma'ashiq na majeshi ya rais bila ya makabiliano" (France 24 on 10/8/2019)].

B- [Waziri wa Usalama wa Ndani Ahmed al-Maisari: Kimya cha afisi ya rais wa Yemen juu ya yale yaliyotokea mjini Aden kilitia shaka na kukosa mafanikio. (Aljazeera, 11/08/2019)].

C- [… Kamanda wa majeshi maalumu katika serikali ya Yemen, Meja Jenerali Fadl Baesh, alitangaza mnamo Jumamosi, 10/8/2019, kuhama kwake na kujiunga na majeshi ya Baraza la Mpito. Kanda ya video, iliyo peperushwa na majukwaa yanayo milikiwa na Baraza hilo la Mpito inamuonyesha Fadl Baesh akitangaza kuhama kwake kutoka katika majeshi ya serikali, na wanajeshi wake kujiunga na majeshi ya Baraza la Mpito la Kusini linalo ongozwa na Rais Meja Jenerali Aidarous Al-Zubaidi" … (Middle East Online mnamo 10/8/2019)].

D- Hii ni ikiongezewa na dori kubwa ya Imarati, yenye kuhadaa mithili ya bwana wake. Imarati ndio muungaji mkono mkubwa wa Al-Zubaidi! Lakini, baada ya kila hatua ichukuayo dhidi ya mipango ya Saudi Arabia, mara moja hutangaza kuwa ni mwanachama wa muungano unao ongozwa na Saudia! Na kwamba wanafanya kazi pamoja ili kuituliza Yemen!

Tatu: Inaonekana kana kwamba Saudi Arabia haikutarajia kasi hii katika maazimio hayo, hususan katika kipindi cha hajj. Baraza la Mpito liliiteka Aden mnamo Jumamosi jioni 10/8/2019. Na kisha Saudi Arabia ikaanza kutambua jambo hilo.

A- [...Muungano wa Usaidizi kwa Uhalali nchini Yemen ulitoa wito mwishoni mwa jana juu ya vitengo na miundo yote ya kijeshi mjini Aden, ikiwemo Baraza la Mpito la Kusini na majeshi ya ukanda wa usalama, yaliyo chukua udhibiti wa hali huko, kurudi mara moja katika maeneo yao; na kujiondoa kutoka katika sehemu zote zilizo ziteka katika siku hizi zilizopita na kutogusa mali za umma na za kibinafsi. Muungano huo pia ulitoa wito wa kusitisha vita mara moja katika mji mkuu wa muda wa Yemen, Aden, kufikia jana usiku 1:00 am, likisisitiza kuwa majeshi yake "yatatumia nguvu ya kijeshi dhidi ya yeyote anaye kiuka hili … na dakika chache baada ya makataa haya, Baraza hilo la Mpito likatangaza makubaliano yake ya kusitisha vita, na kuwa linaridhishwa na wito wa Riyadh wa mazungumzo … (Al-Sharq Al-Awsat mnamo 11/8/2019)]. Mwisho … Lakini, [Naibu Spika Hani Brek alisema katika Twitter kuwa Baraza hilo linabakia kujitolea kwa muungano huo, lakini akasisitiza kuwa "hakutakuwa na majadiliano chini ya vitisho". Duru rasmi katika Muungano wa Waarabu iliitaja taarifa ya Baraza la Mpito ya kusitisha vita kama iliyo nzuri lakini isiyo tosheleza, ikisisitiza haja ya kujiondoa kutoka katika maeneo linayo yadhibiti kupitia njia ya kijeshi. Duru hiyo ilisema kuwa mkutano baina ya pande za Yemen nchini Saudi Arabia utakuwa "punde tu baada ya kujiondoa kwa Baraza la Mpito na kurudi kwa majeshi yake katika maeneo yao" … (Independent Arabic mnamo 11/8/2019)]. Mwisho   

B- Ili kulipa hadhi tangazo la muungano huo, ililenga moja ya maeneo hayo: [moja ya maeneo hayo yanayleta hatari ya wanaharakati wa kujitenga dhidi ya serikali halali ya Yemen katika mji mkuu wa muda wa Aden lililengwa. Muungano huo ulisema kuwa ndio oparesheni ya kwanza unayoifanya kwa muktadha huu na itafuatiwa na oparesheni nyinginezo endapo taarifa ya kusitisha vita haitatiiwa mjini Aden, inayo hatarisha kutumia nguvu dhidi ya wakiukaji … (Al-Arabiya 11/8/2019)].

C- [Duru rasmi katika Muungano wa Waarabu ilitaja kuwa (majeshi ya Baraza la Mpito la Kusini yalianza kujiondoa kutoka maeneo yaliyokuwa yameyadhibiti mjini Aden baada ya majeshi hayo ya muungano kulenga mojawapo ya maeneo ya Baraza hilo. Ulengaji huu ulijiri baada ya maonyo yaliyotolewa na uongozi wa muungano huo katika taarifa mnamo Jumamosi jioni, 10/8/2019, iliotaka kusitishwa kwa vita mara moja mjini Aden … (RT 11/8/2019)].

Nne: Kinacho tarajiwa ni moja ya vitu viwili:

Kwanza: ni kuwa Saudi Arabia, baada ya kuzialika pande hizo mbili kwa mazungumzo nchini mwake itajaribu kila iwezalo kumdhibiti Al-Zubaidi na baraza lake kama ilivyo fanya kwa Hadi na serikali yake, na ingawa hili sio rahisi kupatikana kwa sababu Uingereza iko nyuma ya kuundwa kwa Baraza hili, kutokana na kuporoka kwa Hadi ndani ya udhibiti wa Saudia; hivyo basi haitairuhusu kuanguka tena ndani ya shimo lile lile alimoanguka Hadi. Kuna uwezekano mkubwa kuwa Saudia itatumia sera ya karoti na kigongo kwa Al-Zubaidi. Itamshawishi kushiriki katika serikali ya Hadi akiwa na mamlaka zaidi ndani yake, na Hadi atakuwa na mamlaka machache, lakini atabakia kama raisi ili kuokoa sura. Na Saudia itamtishia Al-Zubaidi, endapo atakataa hili, kwa mashambulizi ya kijeshi. Uwezekano hauondolewi kuwa mkutano wa Mfalme Salman na Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi mnamo 12/8/2019 ni kwa lengo hili ili kuyaregesha mambo kama yalivyo kuwa awali, kwani Saudi Arabia inajua kuwa Imarati iko nyuma ya kuasisiwa kwa Baraza la Mpito linalo ongozwa na Al-Zubaidi.

Pili, endapo Baraza hilo la Mpito litakataa, na juhudi za Saudi Arabia zitafeli, basi Uingereza itaingilia kati moja kwa moja na kuzungumza na Marekani na kuahidi kulisukuma Baraza hilo la Mpito ili kujadiliana na Mahouthi kutafuta suluhisho ambapo Mahouthi wana hisa kubwa ya nguvu. Huenda isiwe ni sadfa kwa Muhammad Al-Bakhaiti, mwanachama wa afisi ya kisiasa ya Mahouthi kuchapisha haya katika ukurasa wake wa Facebook mnamo 11/8/2019 yaani punde tu baada ya udhibiti wa Baraza la Mpito kwa Aden pamoja na kusadifiana na wito wa Saudia wa mazungumzo: (Tunatoa wito kwa vitengo vyote vya kisiasa, hususan vitengo vikuu vinavyo wakilishwa na Ansar wa Mwenyezi Mungu, Chama cha Congress, Chama cha Mageuzi na Baraza la Mpito kukaa katika meza ya mazungumzo ili kumaliza vita na kukubaliana juu ya kuundwa kwa mamlaka mapya ya mpito yatakayo wakilisha kila mmoja na kisha kukubaliana juu ya mradi wa maridhiano)

Hivyo, mazingira ya suluhisho kama hilo yanaonekana kuwa tayari, kwani Marekani inataka kuimaliza kadhia ya Yemen kama ilivyo weka wazi katika taarifa zake kabla ya majadiliano nchini Sweden, na Saudia Arabia inataka kujitoa ndani ya janga la Yemen. Na Uingereza tayari ishaunda kundi ambalo litakuwa chini ya udhibiti wake pasi na kujisalimisha kwa Saudi Arabia. Pia inakubaliana na majadiliano hayo na wala haiyapotoi njia yake kama ilivyo kuwa nyuma wakati ambapo Hadi alishindwa nguvu. Ikiwa Marekani na Uingereza zitakubaliana suluhisho la pamoja, wafuasi wao watalitekeleza: Mahouthi, Baraza la Mpito na Saudi Arabia. Lakini kikwazo cha suluhisho lolote la pamoja baina ya warasilimali hawa litakuwa ni fahamu zao za upatilizaji fursa na manufaa zinazo zunguka ndani ya damu zao. Kipaumbele kwa Marekani pamoja na Uingereza kabla ya suluhisho la pamoja ni kuwa kila mmoja analazimisha suluhisho linalo nali maslahi yake, na hili ndilo linalo refusha majadiliano yao, huku Mahouthi, Saudia, Hadi na Baraza wakisubiri!

Tano: Kinacho umiza ni kuwa watu wa Yemen wana uwezo wa kutatua kadhia yao wenyewe endapo tu watakuwa na ikhlass kwa Mwenyezi Mungu (swt) na wakweli kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Ni vipi wanawaruhusu maadui zetu kuchukua udhibiti wa utatuzi wa kadhia zetu? Mkoloni kafiri anajadili na kutafiti suluhisho la umwagikaji damu ya Waislamu, na kisha kukaa pambizoni mwa damu hiyo kuchagua suluhisho linalo kubaliana na maslahi yao, na watawala na wasaidizi wao katika biladi za Waislamu kupofuliwa na kiburi chao, kana kwamba yanayojiri yanatokea katika ardhi ya mbali na sio katika ardhi za Waislamu! Kuzisalimisha kadhia zetu kwa wakoloni makafiri ili kuzitatua na kuwategemea wao ni kosa kubwa mno linalo wafedhehesha watendaji wake hapa ulimwenguni na watateseka na adhabu yake kesho Akhera.  

 [سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِنْدَ اللَّهِ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ]

“Itawafikia hao walio kosa udhalili na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo kuwa wakivifanya” [Al-An’am: 124]

12 Dhul Hijjah 1440 H
Jumanne, 13/8/2019 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 20:53

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu