Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali

Mapya Yanayojiri Katika Uwanja wa Syria

Kuanzia Tangazo la Erdogan la Mpango Wake wa Kushambulia Mashariki mwa Furat Hadi Tangazo la Trump la Kuviondoa Vikosi Vyake Kutoka Syria!

(Imetafsiriwa)

Swali:

Taarifa za Erdogan kuhusu shambulizi juu ya mashariki ya Furat, kisha kuakhirisha shambulizi hilo, kisha kutangaza upya shambulizi hilo, nk., na kisha kukimbilia kwa Urusi kupangilia operesheni hizo, baada ya ombi la Wakurdi la kulindwa kutokana na serikali ya Syria kufanyika. Kisha tangazo la Trump kuwa ange viondoa vikosi vya Amerika kutoka mashariki ya Furat … na kisha ikafuatiwa na mazungumzo ya kujaza mwanya na kadhalika … Swali ni: ni kipi kilicho nyuma ya kusitasita kwa Erdogan kushambulia mashariki ya Furat? Je vitendo na taarifa hizi za Erdogan kwa maelekezo na Amerika au pasi na maelekezo, inaashiria sera tofauti kati ya Trump na Erdogan? Na ni ipi dhamira ya kuondolewa kwa jeshi la Amerika kutoka Syria? Samahani kwa urefu wa swali hili, Allah akujazi kheri.

Jibu:

Kwa kuchunguza kwa makini matukio tangu Erdogan kutangaza mpango wake wa kushambulia mashariki ya Furat na tangazo la Trump la kujiondoa kutoka Syria hadi leo, ni wazi kuwa:

Kwanza: sera ya Erdogan inaambatana na sera ya Amerika, haifarikiani nayo, bali kama inavyosemwa inaiandama sako kwa bako, hivi ndivyo namna yake:

1- Balozi wa Amerika nchini Syria James Jeffrey aliwasili jijini Ankara na kukutana na maafisa wa Uturuki mnamo 7/12/2018, na kuchora mpango wa Amerika nchini Syria wa kipindi hiki, hususan katika mji wa Manbij na Idlib. Jeffrey alisisitiza kuwa ushirikiano juu ya Manbij umekuwa ni muundo wa amani nchini Syria. “Haiwezekani kupata suluhisho la mwisho huko bila ya ushirikiano wa karibu kati ya Amerika na Uturuki.” Kuhusu ushirikiano na wanamgambo wa Kikurdi, alisema: “Daima tumethibitisha kuwa kazi yetu pamoja na majeshi ya kidemokrasia ya Syria dhidi ya ISIS ni ya muda tu na ya kimikakati …” (RT Online, 8/12/2018), na siku nne baada ya ziara hiyo Erdogan alitangaza mpango wake mpya wa mashariki ya Furat katika hotuba iliyo peperushwa na runinga, Raisi wa Uturuki alisema: “Tutaanzisha operesheni za kijeshi, ndani ya masiku machache, ili kuiondoa mashariki ya Furat mikononi mwa magaidi wanaotaka kuitenga,” akikusudia maeneo yanayodhibitiwa na Vitengo vinavyo husika na Hifadhi ya Watu.” (Shirika la habari la BBC 12/12/2018)

2- Masaa kadhaa kufuatia tangazo hilo la kampeni mpya ya kijeshi ya Uturuki kwa mashariki ya Furat, kulikuweko na taarifa za Amerika zenye kupinga. Ilikuwa ni kutoka kwa msemaji wa Pentagon, Kamanda Sean Robertson, aliyesema katika taarifa, Kitendo chochote cha kijeshi cha upande mmoja kaskazini mwa Syria kitakuwa ni “wasiwasi mkubwa”, kwani huenda kikahatarisha vikosi vya Amerika vinavyofanya kazi pamoja na SDF eneo hilo.” Aliongeza kusema, “Vitendo vyovyote kama hivyo hatutavikubali.” (New Gulf Post, 13/12/2018). Baada ya upinzani huu, uliotoka Pentagon na kutoka kwa wanachama wakuu wa chama cha Republican katika bunge la Seneti, Uturuki imejipata katikati ya maoni mawili tofauti yanayo chipuza kutoka Washington, hivyo basi mpango wa Uturuki umesimama ukisubiri rai ya mwisho jijini Washington! Raisi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema mnamo Jumatatu, 17/12/2018: Kuwa nchi yake huenda ikaanzisha operesheni mpya ya kijeshi nchini Syria wakati wowote … Erdogan alisema katika hotuba katika eneo la Konya katikati mwa nchi hiyo, “Tunatangaza rasmi kuwa tutaanzisha operesheni ya kijeshi mashariki ya Furat” aliongeza kusema: Tumejadili hili pamoja na Bw. Trump na majibu yake yalikuwa mazuri.” (Reuters, 17/12/2018)

3- Raisi Trump ghafla alitangaza mnamo Jumatano 19/12/2018 kuviondoa vikosi vya Amerika kutoka Syria, na kwamba hilo lilitokana na kumalizika kwa kazi, ambayo ni kuishinda “ISIS”. Trump alisema: “Baada ya ushindi wa kihistoria dhidi ya ISIS, wakati umewadia wa kuwarudisha vijana wetu shupavu nyumbani!” (shirika la habari la Urusi la Sputnik News Agency, 20/12/2018). Pamoja na kujiondoa huku, Amerika inaonekana kana kwamba inaiachia Uturuki mashariki ya Furat, na mara moja mpango wa Erdogan ulipokuwa hai, kwa mujibu wa duru hiyo hiyo: jeshi la Uturuki lilituma nguvu ziada kwa vitengo vyake karibu na mpaka wake na syria, Kusini mwa nchi hiyo.

4- Tangazo la Raisi wa Amerika la kujiondoa kutoka Syria limesababisha dhoruba ya malalamishi miongoni mwa wanasiasa wa Kiamerika jijini Washington, na lilipingwa na wanachama wakuu wa chama cha Republican, na kutokana na athari yake ilipelekea kujiuzulu kwa ghafla kwa Waziri wa Ulinzi wa Amerika James Matisse kutoka wadhifa huo. Katika barua yake ya kujiuzulu, Matisse alidokeza vikali tofauti za kisera pamoja na Raisi Trump …” ( shirika la habari la BBC, 21/12/2018). Kwa fedheha hii jijini Washington, raisi wa Uturuki alisema katika hotuba jijini Istanbul, “Tuliamua wiki iliyopita kuanzisha uvamizi wa kijeshi mashariki ya mto Furat … Tulizungumza kwa simu na Raisi Trump na kumekuwako na mawasiliano na mabalozi na maafisa wa usalama, Amerika imetoa taarifa, zilizotusukuma kusubiri kidogo. Erdogan aliongeza kusema: “Tume akhirisha operesheni yetu ya kijeshi dhidi ya “wapiganaji wa Kikurdi” katika eneo la mashariki ya Mto Furat ili tuweze kuona uwanjani natija ya uamuzi wa Amerika wa kujiondoa nchini Syria,” (Reuters, 22/12/2018).

Hivyo basi, ni wazi kuwa operesheni ya kijeshi ya Uturuki mashariki ya Furat imerudi baada ya siku mbili tu katika hatua ya kusubiri tena, kwa sababu inazunguka pambizoni mwa maamuzi yanayo kuja kutoka Washington, ya kuianzisha au kuigandamiza. Tangazo la shambulizi na kuakhirishwa kwake lilishurutishwa na makadirio ya Amerika tangu ziara ya Jeffrey na ziara zilizo fuata. Yaani, Uturuki haina sera nchini Syria kando na yale yanayo kuja kutoka Washington, ikikaribia kuifanya yote kuzunguka katika duara la Amerika, ikiifanya kuwa kibaraka wa karibu. Serikali nchini Uturuki inaangalia maslahi ya Amerika zaidi kuliko maslahi yake, hii imetokea mara nyingi, kama katika operesheni za Ngao ya Furat na Tawi la Zaituni! Na imefungwa na mistari mekundu ya Amerika kama ilivyo kuwa katika Manbij wakati wa Operesheni ya Ngao ya Furat ilipowadia, na kujiweka mbali nao! 

Pili, lengo nyuma ya uamuzi wa Trump wa kujiondoa laweza kufahamika kutokana na yafuatayo:

1- Baada ya kuvunjika moyo kutokana na kuingilia kati kwa Amerika nchini Afghanistan na Iraq, Raisi Obama mwanzoni alitetea aina mpya ya kuingilia kati iliyo ondoa au kupunguza kushiriki kwa vikosi vya Amerika, na kutegemea pakubwa washirika kuwapa vikosi katika vita. Tangu kuanza kwa mzozo wa Syria, Amerika imepeleka wafuasi wake eneo hilo, kama vile Uturuki, Iran na nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba, pamoja na Muungano wa Ulaya ili kucheza dori changamfu katika kuavya mapinduzi hayo dhidi ya Assad. Hilo lisitoshe, Amerika ilitafuta usaidizi wa Urusi wazi wazi katika kutafuta suluhisho la kidiplomasia kupitia Mikataba ya Geneva. Lakini, Amerika iliondoka kijeshi kutoka Syria.

Pindi Trump alipowasili, aliangazia kadhia hii. Na uamuzi wa kujiondoa mnamo 19/12/2018 ukachukuliwa. Trump alitetea uamuzi wake. Aliandika tweets mara kadhaa katika ukurasa wa Twitter mnamo 20/12/2018: “Anatimiza ahadi aliyoweka wakati wa kampeni yake ya uchaguzi mnamo 2016 ya kuondoka Syria. Kuondoka Syria haikuwa ni ghafla. Nimekuwa nikifanya kampeni juu yake kwa miaka, na miezi sita iliyopita, pindi nilipotaka kufanya hivyo hadharani, nilikubali kubakia kwa muda zaidi. Urusi, Iran, Syria na wengineo ni maadui wa kieneo wa ISIS. Tunawafanyia kazi yao. Sasa ni wakati wa kurudi nyumbani na kujenga upya.” Trump alisema katika tweet katika ukurasa wake rasmi wa Twitter: “Kiasili tulikuwa tuweko huko kwa miezi mitatu, na hiyo ilikuwa miaka saba iliyopita – kamwe hatukuondoka.” Aliendelea kusema: “Pindi nilipo kuwa Raisi, ISIS ilikuwa imepitiliza. Sasa ISIS imeshindwa pakubwa na nchi nyenginezo za eneo, ikiwemo Uturuki, zinatakikana kuendeleza kwa urahisi chochote kilicho bakia. Sisi tunarudi nyumbani!” (Russia Today 22/12/2018)

Wakati huo huo, aliishukuru Urusi, Iran, serikali ya Syria na Erdogan kwa huduma yao adhimu kwa Amerika katika mkataba wa Sochi juu ya Idlib, mnamo 17/9/2018, akikumbusha kuwa ni yeye ndiye aliyetaka kufanya makubaliano haya na wakajibu ombi lake … Anajua kwamba Urusi na Iran na chama chake nchini Lebanon na wafuasi wake, Uturuki, Saudi Arabia na wafuasi kutoka mashirika na wengineo wako tayari kupigania lengo hilo hilo la Amerika; kuzuia kuporomoka kwa serikali ya Syria na kuzuia kurudi kwa Uislamu, walijitolea kwa siri na dhahiri kwa makubaliano ya Geneva, Astana na Sochi na katika maazimio ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama yanayo husiana na Syria na hususan Azimio 2254 lililo salimishwa na Amerika katika Baraza hilo, ambalo liliafikiwa kwa pamoja; pande zote hizi na nyenginezo zilitoa wito wa kutekelezwa kwake. Tumetaja katika jibu la swali mnamo 29/7/2018 kuwa mojawapo ya mipango ya Amerika:  

“Ni kutegemea juu ya majeshi ya eneo “kwa ajili ya kuweka amani”, na huenda wakavileta vikosi vya Misri, Saudia na Uturuki kwa ajili ya lengo hili. Habari hizi zi ngeni … Mtazamo huu wa Amerika wa suluhisho nchini Syria unalotoa wito wa kusajiliwa vikosi kutoka ng’ambo … utawala wa Raisi Donald Trump unapanga kubadilisha majeshi ya Amerika kwa majeshi ya Waarabu nchini Syria ili kudumisha ustawi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo baada ya kushindwa kwa ISIS.”  

2- Akili ya Trump ni ile ya mfanyi biashara, iliyotawaliwa na fikra ya faida na hasara. Anataka kuokoa gharama za wanajeshi wa Amerika katika Hazina ya Amerika. Ingawa Saudi Arabia na Imarati zililipia gharama nyingi zaidi za wanajeshi wa Kikurdi na za kuwahami kwa silaha, na pia kuchangia katika gharama za muungano wa kimataifa: Saudi Arabia na Imarati, hivi majuzi zilikuwa ndio mchezaji hafifu muhimu zaidi nchini Syria, dhidi ya ripoti zilizo kuwa nyuma ya vyombo vya habari zilizotaja usaidizi wa Riyadh kwa Wakurdi wa Syria, katika mpaka wa Uturuki.” ( Al-Arabiya-Misri mnamo 4/12/2018). Saudi Arabia pia ilitangaza mnamo Disemba 14, 2018, malipo ya kiwango fulani kwa muungano wa kimataifa unao ongozwa na Amerika. “Saudi Arabia imechangia $100 milioni, huku Imarati ikichangia $50 milioni katika ufadhili mpya,” msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Amerika Heather Nauert alisema.” (Khaleej Online, 17/12/2018)   

Lakini, anataka kuziziba gharama zote hizi za wanajeshi wake na gharama za kuzunguka kwao na silaha kwa sababu anazichukulia gharama hizi kuwa hasara kwa elimu yake kama mfanyi biashara, na anataka kupeana dori yake kwa mtu mwengine, na hili kwa sasa halikufichika katika taarifa zake zilizo nukuliwa na wanahabari wa Reuters 20/12/2018 kufuatia uamuzi wake wa kujiondoa kutoka Syria; “Trump aliongeza: Je, Amerika inataka kuwa askari Polisi wa Mashariki ya Kati, huku ikiwa haipati chochote isipokuwa inatumia maisha ya watu yenye thamani na trilioni za dolari kuwalinda wengine ambao, mara nyingi, hawana shukrani na yale tunayoyafanya? Je, tunataka kuwa huko milele? Ni wakati sasa kwa wengine hatimaye (pia) kupigana …” Yote haya yaonyesha kuwa Amerika inataka wengine kubeba vita vyake, ili damu zao pia zimwagike badala ya damu za Amerika, na hazina zao zitumike badala ya hazina ya Amerika!

3- Trump anataka pande zengine kujihusisha katika suluhisho la kisiasa kama itakavyo Amerika na sio katika vitendo vya kijeshi angaa katika dhurufu za sasa. Alifanya hili kwa kulisitisha jeshi la Urusi na majeshi ya serikali kutokana na kushambulia Idlib kwa sababu anataka kulipata suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa mipango yake juu ya yote mengine, na tumetaja hilo katika jibu la swali tulilotoa mnamo 22/9/2018:

 “Urusi sasa imejua sera hii ya Amerika … hii ndio sababu haikuweza kukamilisha shambulizi ililolitayarisha ili kumaliza mgogoro mjini Idlib kwa njia yake kwa sababu Uturuki ilipinga (ikisukumwa na Amerika) na Iran ikasalia kimya … Hivyo basi, mkutano wa Iran mnamo 7/9/2018 ulifeli kuidhinisha mpango wa Urusi wa kushambulia Idlib na kumaliza mgogoro huo kwa njia ya Urusi. Ni siku chache tu sasa tangu mkutano kati ya Erdogan na Putin na shambulizi limebadilishwa kwa kubuniwa eneo lisilo la kijeshi! Hii ni kwa kuptia baraka za Amerika, shirika la habari la Novosti lilimnukuu afisa mmoja wa Amerika mnamo 18/9/2018 akiliambia shirika hilo: “Tunazikaribisha na kuzishajiisha Urusi na Uturuki kuchukua hatua za kivitendo kuzuia shambulizi la kijeshi kutoka kwa serikali ya Assad na washirika wake juu ya mkoa wa Idlib…

Hivyo basi, Urusi imekomesha ubwagaji wake mabomu wa Idlib na kurudisha manuari zake, ambazo zilifanya mazoezi ya kijeshi katika bahari ya Mediterranea, na bado ingali inaiomba Amerika moja kwa moja au kupitia Uturuki kuitatua kadhia ya Idlib kijeshi kabla ya suluhisho la kisiasa. Lakini Amerika inataka suluhisho la kisiasa kabla ya suluhisho lolote la kijeshi mjini Idlib, ili kulitumia kama karata ya shinikizo ili kuitishia Urusi juu ya kambi zake za kijeshi nchini Syria na kisha kuufanya upinzani kuibua kadhia ya kambi hizo katika suluhisho hilo la kisiasa … Yaani, maslahi ya Uturuki na Amerika nyuma yake kusitisha shambulizi la Urusi kwa Idlib kimsingi ilikuwa kwa maslahi ya Amerika na wala si kuizuia serikali kutoifikia Idlib au kuwalinda raia, bali katika wakati ambao Amerika italazimisha utekelezaji wa suluhisho hilo inalolitaka na kuilazimisha Urusi kwalo. Kisha hawatajali damu za Idlib, raia au wasio raia, kuondoa nguvu za kijeshi au kutoondoa … na historia yao inazungumzia hili katika maeneo tofauti tofauti ya Syria, na uhalifu wao unajulikana vizuri mno …” Mwisho wa nukuu

Hivyo basi, Trump kuamua kujiondoa kumezifanya pande zote kuwa karibu na lengo hili, imeihadaa Uturuki na kuifanya kufikiria itajaza mwanya baada ya kujiondoa kwa majeshi ya Amerika … Na kutia hofu katika nyoyo za Wakurdi sasa kuwa wanakabiliwa na tishio la Uturuki, na hivyo Wakurdi wakakimbilia kwa serikali wakiomba himaya, ambalo ndilo inalotaka serikali. Kukabiliana na matishio ya Uturuki kwa Wakurdi mjini Manbij, serikali inapeleka majeshi yake eneo la Manbij … na kwa sababu Urusi inaisaidia serikali na wakati huo huo inakubaliana na Uturuki, imekuwa ni vigumu kwa Uturuki kuipiga vita serikali mjini Manbij isipokuwa mahusiano mapya yabuniwe katika eneo hilo … Hivyo basi, Trump aliziacha pande zote bila ya khiari ila kuanzisha mazungumzo ya suluhisho, kwa mujibu wa yale Amerika inayotaka! Baadhi ya pande hizo zimeanza kuzungumza hadharani na nyengine kuzungumza kwa siri:

A- Msemaji mmoja wa Wizara ya Kigeni ya Urusi alisema kuwa “Uamuzi wa Washington wa kuviondoa vikosi kutoka Syria ni lazima uchangia katika suluhisho pana la hali hiyo, ukiangazia ukosefu wa uwazi katika ratiba ya kujiondoa kutoka Syria.” (Sputnik Arabic 26/12/2018).

B- Duru za Al-Mudun zilithibitisha kuwa mchakato wa kudhibiti Manbij, ambao ulitangazwa siku mbili zilizo pita, umesitishwa kwa matakwa ya upande wa Uturuki, na uliakhirishwa kwa lengo la kuendeleza majadiliano ya Uturuki pamoja na Urusi na Amerika.” (27/12/2018) mwisho.

Hivyo basi, Trump aliweza kubadilisha juhudi za pande zote za makubaliano ambazo alizipa njia kupitia uamuzi wa kujiondoa alioutaja … ikaziacha pande hizo zikiwa hazina khiari nyengine isipokuwa mpango wa Amerika wa kutatua mgogoro nchini Syria.  

4- Kadhia ya uchaguzi pia ni mojawapo ya sababu muhimu za Trump. Trump ana msimamo wa zamani wa kibinafsi dhidi ya vita vya nje, kwa mujibu wa kampeni “Amerika Kwanza” iliyomfanya kushinda uchaguzi. Hivyo basi, kutoa wito wa kuondolewa kwa vikosi kutoka Syria na Afghanistan ni kwa manufaa yake binafsi, kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi ujao wa 2020. Hivyo basi ana hamu ya kuregea kwa vikosi 2000 vya Amerika kutoka Syria ( gazeti la The Guardian, 19/12/2018) na 7,000 kutoka Afghanistan, ( NPR, 21/12/2018) na kisha apate umaarufu wa Waamerika kwa jumla na kupata uungwaji mkono katika kuchaguliwa tena mnamo 2020:

Tatu: Trump amewasababishia vibaraka na wafuasi wake maumivu makali ya kichwa, kutokana na uamuzi wake wa kujiondoa hata kabla utabikishwaji wake kwa mwendo wa kinyonga ambao huenda ukachukua miezi, endapo utamalizwa kikamilifu … akitafakari yale yaliyojiri na yanayojiri. Inaonekana kuwa Trump hawachukulii uzito vibaraka na wafuasi hawa, lau kama wanajua wangemuacha lakini hawaelewi! Amewatumia kutabikisha njama zake kwa fedheha na uhadaifu hata Urusi na Ulaya pia hazikusazwa:

1- Wakurdi ambao ni watumishi watiifu wa Amerika walidhani kuwa Amerika inawapa mafunzo na silaha ili kujitenga kutoka Syria na kuwa na dola yao wenyewe ambayo Amerika itadhamini kuilinda. Walianza kutabikisha yale Amerika inayotaka kwa ajili ya dola hiyo ahidiwa! Hivyo basi, walikuwa mstari wa mbele katika kila vita Amerika ilivyotaka! Waziri wa Ulinzi wa Amerika, wakati huo, Ashton Carter aliyasifu Majeshi ya Kidemokrasia ya Syria, mwavuli wa makundi ya Kikurdi yaliyo andaliwa na Amerika. “Wamethibitisha kuwa washirika wetu wazuri mno uwanjani katika kupigana na ISIL,” Carter alisema: Tunashukuru sana kwa hilo, na tuna nia ya kuendelea kufanya hivyo, tukitambua ugumu wa dori yao hiyo ya kieneo.” ( The Hurriyet Daily News, 18/3/2016). Na hivyo Wakurdi walidhani kuwa Amerika itabakia kuwasaidia kisiri na dhahiri, taarifa ya James Jeffrey, Mwakilishi Maalumu wa Amerika nchini Syria iliyotajwa juu, haikuwazindua: “Juu ya ushirikiano na wanamgambo wa Kikurdi, alisema: Daima tunathibitisha kuwa kazi yetu pamoja na Majeshi ya Kidemokrasia ya Syria dhidi ya ISIS ni muda tu na ya kimikakati …” (RT Online 8/12/2018).   

Na waliendelea katika huduma yao na hili lilirahishia Amerika kuwatumia popote walipotaka kuhudumia maslahi yao wenyewe na wala si ya Wakurdi! Na pindi maslahi ya Amerika yalipo hitaji kujiondoa na kuiwacha migongo yao kuanikwa kwa matishio ya Uturuki, Amerika ilitoa uamuzi huo bila ya kuzingatia maslahi ya Wakurdi … Hili limewasukuma mikononi mwa serikali, kama Amerika ilivyo taka ili kuiruhusu serikali kuregea kaskazini mwa Syria na kwa matakwa ya Wakurdi! “Viongozi wa Wakurdi, wanaodhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Syria na ambao wametatizika na uamuzi wa Amerika wa kujiondoa kutoka eneo hilo, wameisihi Urusi na mshirika wake Damascus kutuma vikosi ili kuulinda mpaka kutokana na tishio la shambulizi la Uturuki. Wito wa Wakurdi wa kurudi kwa majeshi ya serikali ya Syria mpakani, ambao kwa miaka mingi ulikuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo wa Kikurdi, umefichua kina cha mgogoro wao huku kukichomoza kwa uamuzi ghafla wa Raisi Donald Trump wa kuviondoa vikosi.” ( Sputnik Arabic 27/12/2018)  

Majeshi ya Kidemokrasia ya Syria yameuchukulia uamuzi ghafla wa kujiondoa kwa Amerika kutoka mashariki mwa Syria “kudungwa kisu cha mgongo na khiana kwa damu ya maelfu ya wapiganaji”, katika maoni yake ya kwanza juu ya uamuzi huo mnamo Jumatano, Chama cha Uchungaji Haki za Kibinadamu kilinukuu duru ambazo kilizitaja kama za kutegemeka, kikisema kuwa nguvu zinazoongoza katika majeshi ya kidemokrasia ya Syria zinakadiria kujiondoa kwa majeshi ya Amerika katika tukio lililofanywa, ni kisu mgongoni mwa majeshi ya kidemokrasia ya Syria na vitengo vya ulinzi vya Wakurdi, “vilivyo chukua udhibiti katika miezi na miaka iliyopita juu ya eneo kubwa la kijiografia lililodhibitiwa na ISIS, ambalo ni eneo la Mashariki ya Furat pamoja na Manbij. (Tovuti ya habari ya Tahrir, 19/12/2018) Mwisho wa nukuu

2- Uturuki pia iliachwa imefedheheka, ilidhani kuwa kujiondoa kwa Amerika kutaifanya kujaza pengo, hususan kwa kuwa uamuzi wa kujiondoa ulikuwa baada ya mawasiliano ya Trump pamoja na Erdogan kupitia simu hiyo. Gazeti la Russia Today liliripoti mnamo 19/12/2018, “Afisa mmoja wa Amerika alifichua kwamba Raisi wa Amerika Donald Trump ameamua kuviondoa vikosi vya Amerika kutoka Syria kama natija ya mazungumzo yake ya hivi majuzi pamoja na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, afisa huyo wa Amerika alisema katika mahojiano na waandishi wa habari wa Reuters mnamo Jumatano kuwa uamuzi huo ulichukuliwa baada ya maongezi ya simu kati ya Trump na Erdogan Ijumaa iliyopita. Duru hiyo hiyo ilisema: “Kila kilichotokea baadaye kinatekelezwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo hayo ya simu.” 

Kuhusiana na maongezi ya simu kati ya Erdogan na Trump, shirika la habari la Uturuki la Anadolu liliripoti mnamo 21/12/2018: Raisi wa Uturuki alisema: Trump alituuliza: Je, mwaweza kuimaliza ISIS? Erdogan akasema: “Tayari tushawamaliza, na twaweza kuendelea na hili siku zijazo … tunahitaji tu usaidizi wenu wa vifaa … Mwishowe, Waamerika wakaanza kujiondoa, na sasa lengo letu ni kuendelea na mahusiano yetu ya kidiplomasia pamoja nao sawa sawa.” Hivyo Uturuki ilidhani ndiyo itakayojaza pengo … Lakini kilichotokea ilikuwa ni kuingia kwa serikali mjini Minbij kwa ombi la Wakurdi! “takriban wanajeshi 1,000 wa serikali, walioandamana na vifaru na silaha nzito, walikusanyika katika kivuko cha Tayheeh, na takriban wanachama 40 wa serikali waliingia eneo la makutano na kijiji cha SDF cha Al-Yalni, kaskazini mashariki mwa Al-Arima. Ni nukta ya kwanza ya jumuiko kwa majeshi ya serikali baada ya makubaliano pamoja na SDF juu ya kupeleka majeshi ya pamoja dhidi ya vituo vya udhibiti vya Jeshi Huru na majeshi ya Uturuki …” (tovuti ya Al-Mudun 27/12/2018).

Na kisha ujumbe wa Uturuki ukaelekea mnamo 29/12/2018, ukijumuisha Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Kigeni wa Uturuki na Kiongozi wa Majeshi ili kujadili kadhia hiyo. Lakini taarifa za baadhi ya maafisa wa Urusi zilikuwa za uchokozi kwa Uturuki: Msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Urusi Maria Zakharova, alisema mnamo Jumatano, 27/12/2018: “mamlaka ya Syria ni lazima yadhibiti ardhi zitakazo achwa na Waamerika." Aliendelea kusema: “Bila shaka, kuna swali msingi: ni nani atakaye dhibiti maeneo yatakayo achwa na Waamerika? Ni wazi hili ni lazima lifanywe na serikali ya Syria kwa mujibu wa kanuni ya kimataifa.” Zakharova alitangaza: “Tunawasilisha rai kwa karibu na kutabikisha sera maalumu juu ya faili ya Syria pamoja na wenzetu wa Uturuki, katika mwelekeo wa sera ya kigeni pamoja na uwanja wa operesheni za kijeshi ili kupambana na ugaidi uwanjani.” (tovuti ya Al-Mudun, 27/12/2018). Seneta maarufu wa chama cha Republican Lindsey Graham pia alisema kuwa Trump amejitolea kuhakikisha kuwa Uturuki haigongani na majeshi ya Vitengo vya Ulinzi wa Raia baada ya kuondolewa kwa vikosi vya Amerika kutoka Syria na kuithibitishia Uturuki, mshirika wa Amerika katika NATO kubuniwa kwa eneo la usalama ili kulinda maslahi yake. Uturuki inavikadiria Vitengo vya Ulinzi wa Raia kuwa tawi la harakati ya kujitenga ya Kikurdi katika eneo lake na kutishia kulishambulia kundi hili. ( Arabic Post, 31/12/2018).

“Jeshi la Urusi kisha likabuni upya Kituo cha Mawasiliano na Maridhiano cha Urusi nchini Syria katika mji wa Al-Arima kitongoji cha Manbij, baada ya kujiondoa kutoka humo muda mchache uliopita.” (tovuti ya Al-Mudun, 27/12/2018).  

3- Hata Urusi nchi iliyo na kadri ya nguvu, Amerika inaitoa kutoka mgogoro mmoja hadi mwengine. Urusi inajua kuwa imezama katika kizungumkuti cha Syria tangu kuingilia kwake kijeshi nchini Syria baada ya mkutano kati ya Obama na Putin mnamo 29/9/2015. Badali yake Putin alitarajia kuondolewa kwa vikwazo baada ya kadhia ya Crimea, lakini havikuondolewa … Kisha Urusi ikataka kutatua kadhia ya Idlib kijeshi ili kupumzishwa mzigo wa Syria na kujikwamua kutoka katika janga hilo na kuchukua suluhisho la kisiasa baada ya muda huo mrefu. Hakuna kitakacho sababisha madhara yoyote maadamu ilikuwa huru kutokana na hatua ya kijeshi nchi Syria; lakini, Amerika ilizuia hili, na kutaka suluhisho la kisiasa kwanza. Tulitaja hili katika jibu la swali lililotolewa mnamo 22/9/2018 lililotajwa juu: “Hivyo, Urusi ilisitisha ubwagaji wake mabomu wa Idlib na kurudisha manuari zake, zilizofanya mazoezi ya kijeshi katika bahari ya Mediterania, na ingali inaiomba Amerika moja kwa moja au kupitia Uturuki ili kutatua kadhia ya Idlib kijeshi kabla ya suluhisho la kisiasa. Lakini Amerika inataka suluhisho la kisiasa kabla ya suluhisho lolote la kijeshi mjini Idlib, ili kulitumia kama karata ya shinikizo ili kuitishia Urusi juu ya kambi zake za kijeshi nchini Syria na kisha kuufanya upinzani kuibua kadhia ya kambi hizo katika suluhisho hilo la kisiasa …”   

Na kisha tatizo la uamuzi wa Trump wa kujiondoa ukatia msumari wa moto kwenye kidonda!!! Kisha yaliyojiri baadaye, pindi Urusi ilipokuwa katikati ya serikali na Uturuki mjini Manbaj na maeneo mengine ya Kikurdi mashariki mwa Furat! Urusi inaisaidia serikali, na Urusi na Uturuki zina makubaliano, na mkusanyiko wa majeshi ya Uturuki na ya serikali unakaribia, na Urusi imejipata katikati yao, jambo linaloifanya Urusi kuwa katika tatizo endapo vita vitazuka … Hivyo, Amerika inaitoa Urusi kutoka katika tatizo moja hadi jengine!

4- Ama kwa Ulaya, baadhi ya nchi zilijihusisha na muungano wa kimataifa na kujiondoa kwa Amerika kutaziacha zimefedheheka, haziwezi kubakia peke yao … Wakati huo huo zilitaka Amerika iteseke nchini Syria na kutowaangalia kwa mbali kwa salama! Hii ndio sababu zilipinga na kushambulia uamuzi wa kujiondoa. Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza alisema: “Muungano wa kimataifa dhidi ya ISIS umepiga hatua kubwa, lakini bado kungali na kazi kubwa, na hatupaswi kupoteza dira ya tisho la ISIS hata bila ya ardhi, ISIS inasalia kuwa tishio.” (Euro News, 19/12/2018), ambayo inakataa sababu ya Trump ya kujiondoa. Raisi wa Ufaransa, Emmanuel Macron, pia alikashifu uamuzi wa Raisi wa Amerika Donald Trump wa kuviondoa vikosi vya Amerika kutoka Syria, akisisitiza kuwa “mshirika ni lazima awe mwaminifu.” “Nimesikitishwa sana kuhusu uamuzi wa Trump juu ya Syria,” alisema, akizungumza kutoka mji mkuu wa Chad wa N'Djamena. “Kuwa mshirika kwa maanisha kupigana sako kwa bako,” Macron aliongeza kuwa Ufaransa inafanya hivyo pamoja na Chad katika kupigana na makundi ya kisilahi ya kijihadi. (Shirika la habari la BBC 23/12/2018) Mwisho.

Nne: Mwisho, ni uchungu kuwa wakoloni makafiri wanadhibiti kadhia zetu, ndio wanao amua … na watawala katika biladi za Waislamu wanatekeleza … pasi na kuona aibu mbele ya Allah Al-Aziz na Al-Hakim, na Mtume wake (saw), bali kila wanapo onyeshwa haki hujiweka mbali nayo ili kuwaridhisha mabwana zao wanao waweka vitini mwao. Hawatafakari yale yaliyowapata watangulizi wao, waliotupwa na mabwana zao pindi dori zao zilipomalizika, hivyo basi, walijiangamiza kwa mikono yao wenyewe hapa duniani na kesho Akhera, kwa sababu walikuwa wamejiweka mbali na haki walio onyeshwa.

وَهُمْ يَنْهَوْنَ عَنْهُ وَيَنْأَوْنَ عَنْهُ وَإِنْ يُهْلِكُونَ إِلَّا أَنْفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ﴿

“Na wao wanakataza (wengine) kutokana nayo na wao wanajiweka mbali nayo. Na hakika hawaangamizi isipokuwa nafsi zao, lakini hawahisi (hilo).” [Al-An’am: 26]  

Na kisha wakapoteza hii dunia na Akhera, hakika ni hasara kubwa ilioje.

23 Rabii’ Al-Akhir 1440 H

Jumapili, 30/12/2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 21:02

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu