Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Trump na Kongamano la Shirika la Kujihami la NATO
(Imetafsiriwa)

Swali:

Kongamano la NATO lilifanywa jijini Brussels, mji mkuu wa Ubelgiji na makao makuu ya Muungano wa Ulaya, mnamo 11 na 12/7/2018. Lilihudhuriwa na raisi wa Amerika na viongozi wa nchi 29 wanachama wa muungano huo. Mdahalo kati yao na Trump ulipamba moto na kukaribia kufungika juu ya kadhia ya kuongeza matumizi kwa majeshi hadi asilimia 2 ya mapato jumla ya nchi. Ni kwa nini Amerika inafanya hivyo? Na ni ipi hatma ya muungano huu?   

Jibu:

Ili kufafanua jibu hili, tutatathmini yafuatayo:

1- Raisi wa Amerika, Trump, anatenda tofauti kinyume na diplomasia na ujanja. Anatangaza wazi wazi kwamba anataka na kuwashinikiza wengine hadharani; kile asemacho na aulizacho nyuma ya pazia na katika mikutano ya faragha na wenzake kutoka nchi nyenginezo ndicho kile asemacho na atakacho hadharani kwa hali ya utovu wa heshima na kiburi zaidi kuliko George W. Bush, mwana. Hivyo basi, yuko kinyume na mtangulizi wake, Obama, aliyekuwa akifanya hivyo nyuma ya pazia, akiwashinikiza wenzake na dola nyenginezo, akifanya ujanja wa kisiasa na miviringo ya kisiri kana kwamba ni mwanasiasa wa Kiingereza! Raisi huyu wa zamani, Obama, ndiye aliyelazimisha ongezeko la uzalishaji jumla wa nchi (GDP) kwa asilimia 2 juu ya nchi wanachama mnamo 2014, na kuanza kuzishinikiza kwa njia tofauti tofauti ili kujifunga na makubaliano hayo.

Habari kuhusu mawasiliano yake na nchi hizi wanachama kuhusiana na ongezeko hili yalifanywa pasi na kuzua taharuki kwa raia kwa kuonesha kuwa muungano huu uko imara kama mwili mmoja, na kiongozi wao ni Amerika, ambayo imeridhika na maendeleo yake na wanachama wake, huku ukweli ukiwa, iko katika sintofahamu kubwa nazo. Wanachama wa NATO walimuahidi Obama mwaka huo kutumia kiwango hicho cha GDP za nchi zao katika ulinzi kufikia 2024, lakini takriban nchi 15 wanachama, zikiwemo Ujerumani, Canada, Italy, Ubelgiji na Uhispania, zingali matumizi yake ni madogo asilimia 1.4 na huenda zikashindwa kutimiza ahadi zao jambo lililomkasirisha Trump. Chini ya mradi wa Amerika juu ya kadhia hii, nchi za NATO zitajitolea kufikia 2030 kutoa, ndani ya siku 30, vikosi 30, msururu wa ndege za kivita 30 na manuari 30 kupambana na uwezekano wa operesheni ya kijeshi dhidi ya Urusi. Amerika imeunda adui bandia, naye ni Urusi, ili kutawala Ulaya na kuwazuia kutokana na maamuzi huru ya kijeshi na ya kisiasa, na hivyo kuwalazimisha kubakia chini ya uongozi wake na angaa chini ya mwavuli wake wa kijeshi.    

2- Trump anaelewa ugumu wa hili pamoja na washirika wake, ugumu wa kuwashawishi, na hiyo ndio sababu aliandika katika mtandao wa Twitter mnamo 10/7/2018 alipokuwa akielekea katika kongamano hilo la NATO jijini Brussels: “Mkutano wake (unaotarajiwa mnamo Julai 16, 2018) mjini Helsinki na Raisi wa Urusi Putin huenda ukawa sahali zaidi kuliko kongamano hili la NATO”. Maneno yake yanabeba ukweli mwingi; Urusi inaonekana kujisalimisha na kuwa tayari kutoa huduma kwa Amerika ili kupata baadhi ya maslahi yake, na kujitokeza kama dola kuu yenye ushawishi kwa ulimwengu sambamba na kuwa dola ya kwanza, pamoja na kuukomesha uovu wa Amerika dhidi yake, hususan katika eneo la ushawishi wake na viunga vyake, ambalo Amerika anatafuta udhibiti wake. Ama kuhusu Ulaya, inaonekana kama adui, na mshindani na imeunda Muungano wa Ulaya ili kusimama dhidi ya Amerika na kushindana nayo, na hivyo basi, Amerika inabeba hisia ya uhasimu dhidi ya Muungano huo, na kufanya kazi kuuvunja wazi wazi; hivyo basi, iliunga mkono kujiondoa kwa Uingereza katika muungano huo (brexit). Trump aliishambulia sera ya Waziri Mkuu wa Uingereza Teresa May ya kwenda katika soko huru pamoja na Muungano wa Ulaya baada ya kuondoka katika muungano huo, alisema:

“Ikiwa watafanya mpango kama huo, tutaamiliana na Muungano wa Ulaya badala ya kuamiliana na Uingereza, hivyo huenda ikauuwa mpango huo.” Na akasema: “Kwa hakika nilimwambia Theresa May jinsi ya kutenda hili lakini hakuafiki, hakunisikiliza. Alitaka kufuata njia tofauti”

Trump alimsifu Boris Johnson, Waziri wa Kigeni wa Uingereza aliyejiuzulu kwa sababu ya upinzani wake kwa mpango wa May na kusema “ana uwezo wa kuwa Waziri Mkuu” (Chanzo: Shirika la BBC lilinukuu kutoka kwa gazeti la The Sun mnamo 13/7/2018) na kutoa wito hadharani kwa nchi nyenginezo kuondoka katika Muungano wa Ulaya. Vile vile alitoa ombi kwa Raisi wa Ufaransa, aliyemzuru Aprili iliyopita, kuondoka katika Muungano wa Ulaya. Gazeti la The Washington Post liliripoti mnamo 29/6/2018 kuwa “Trump alitoa ombi kwa mwenzake wa Ufaransa Macron kuondoka katika Muungano wa Ulaya kwa badali ya makubaliano ya ubadilishanaji kati yake na Amerika wakati wa ziara ya ikulu ya White House Aprili iliyopita.” Iilinukuu maafisa wawili wa Ulaya wakisema: “Trump alimwambia Macron: Kwa nini usiondoke katika Muungano wa Ulaya?” 

3- Hii ndiyo sababu Trump aliukashifu Muungano wa Ulaya, hususan Ujerumani, kwa sababu mgogoro wake na Amerika ni mkubwa mno na mzito! Katika jibu la swali mnamo Juni 7, 2018, tulitaja sababu za kuzidi kwa mgogoro huu haswa na Ujerumani. Tulisema: “Ujerumani ni kitovu kikubwa zaidi cha kifedha barani Ulaya na ni uchumi wa nne kwa ukubwa ulimwenguni baada ya Amerika, China na Japan, kwa hivyo macho ya Trump bado yalikuwa yanaielekea katika jaribio la kuchuma pesa nyingi kwa Amerika hususan kwa kuwa Amerika inadai kuwa Urusi ni tishio kwa Ujerumani ili kuifanya Ujerumani ijiunge na kuchangia zaidi katika NATO; Berlin hutumia asilimia 1.2 ya mapato yake ya kitaifa katika jeshi (dolari bilioni 42).  

Mizani ya kibiashara baina ya Amerika na Ujerumani inadokeza zaidi mwelekeo huu tuliotangulia kuutaja sasa hivi, takriban sarafu za Euro bilioni 107 ndio kiwango cha uagizaji bidhaa wa Amerika kutoka Ujerumani …” na tumetaja “mandhari ya Ulaya itashuhudia kuibuka zaidi kwa uongozi wa Ujerumani katika mustawa wa kisiasa na kiuchumi, na linaloashiria na kuthibitisha hili ni mwelekeo wa maafisa wa Ujerumani kwa sera za Amerika na tangazo la uchu wa Ujerumani kuuleta mzozo kati yake na Amerika hadharani.  Ikiwa hili litaongezeka, litaidhoofisha pakubwa Ulaya na, mwishowe, huenda likapelekea Ujerumani kujihami kikamilifu na kwa haraka”.

4- Trump ameona changamoto ya Ujerumani kwake kwa sintofahamu yake kwake, hususan kwa kuwa amedhihirisha uhasimu wake kwa Muungano wa Ulaya, ambao Ujerumani inauangalia kama fursa nzito kwa soko lake la kiuchumi. Na inaukadiria kama chombo ambacho kwacho Ujerumani inasafiria katika uwanja wa kimataifa ili kushawishi siasa za kiulimwengu. Hivyo basi, Trump anaikashifu Ujerumani haswa na kuitaka kumpa mabilioni ya dolari kwa ajili ya ulinzi iliopewa na Amerika tangu Vita vya Pili vya Dunia. Alisema kabla ya kongamano hili, alipoanzisha hujuma kwa Ujerumani wakati wa mkutano wake na Katibu Mkuu wa NATO, “Ujerumani ni mateka wa Urusi kwa sababu inapata kawi yake nyingi kutoka Urusi. Wanalipa mabilioni ya dolari kwa Urusi nasi hatuna budi kuwahami dhidi ya Urusi. Hili tutalifafanua vipi? Huku ni kukosa uadilifu” Trump alisema kabla ya kongamano hili: “Ujerumani inadhibitiwa kikamilifu na Urusi kwa sababu watapata kutoka asilimia 60 hadi asilimia 70 ya kawi yao kutoka Urusi, na mabomba mapya na huku wewe waniambia eti hiyo ni sawa kwa sababu mimi nadhani si sawa na nadhani ni jambo baya mno kwa NATO.” (Chanzo: Shirika la habari la BBC, Julai 12, 2018)  

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel alijibu: “Ujerumani ina sera zake yenyewe na hufanya maamuzi huru … nimeshuhudia mwenyewe sehemu moja ya Ujerumani ilipokuwa ikidhibitiwa na Muungano wa Kisovieti. Nina furaha sana kuwa leo tumeungana katika uhuru, nao ni Jamhuri ya Majimbo ya Ujerumani. Kwa sababu ya hilo tunaweza kuwa twaweza kuunda sera zetu huru na kufanya maamuzi huru.” “Sisi sio mahabusu, wa Urusi wala Amerika,” alisema Waziri wa Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas. (Chanzo: Shirika la habari la BBC, 12/7/2018) Trump na Merkel kila mmoja alimpuuza mwenziwe walipokuwa wakitembea katika sakafu ya makao makuu mapya ya NATO kuelekea katika jukwaa kupiga picha ya kidesturi. Trump mara kwa mara amekuwa akishtumu mradi wa mabomba ya gesi wa Nord Stream, unaounganisha Urusi na Ujerumani na kuitaka kuachana nao. Mradi huu unapingwa na baadhi ya watu Ulaya kusababisha mgawanyiko katika sera ya Muungano wa Ulaya. Poland hukadiria kuwa Ulaya haiuhitaji. “Nord Steam ni muundo wa nchi za Ulaya unaoipa Urusi pesa na kuipa mbinu ambazo zaweza kutumiwa dhidi ya usalama wa Poland,” Waziri wa Kigeni wa Poland Jacek Czaputowicz alisema alipowasili katika makao makuu ya NATO. (Chanzo: AFP, 11/7/2018)  

Anazungumza kwa niaba ya Trump. Hii ni kwa sababu Poland inafuata Amerika, inaifanyia kazi Amerika ndani ya Muungano wa Ulaya. Hivyo basi, Amerika imekuwa ikifanya kazi ndani ya Muungano wa Ulaya kwa muda mrefu ili kuuvunja, lakini lililojipya katika enzi ya Trump ni kuwa aliongeza vitendo vya hadharani vya moja kwa moja ili kuuvunja Muungano huo, kuilazimisha Ulaya kutekeleza asilimia 2 imekuwa ndio kadhia yake nyeti ya kuonesha mafanikio yake. Mtangulizi wake, Obama, hakufaulu kuilazimisha Ulaya kuongeza gharama ya Ulinzi hadi asilimia 2. Hili litaimarisha msimamo wake (Trump) nyumbani na kuimarisha fursa za Chama cha Republican katika uchaguzi wa nusu muhula pamoja na kupata muhula wake wa pili wa uraisi.   

5- Lakini Ufaransa ilijibu zaidi. Raisi wake Macron alisema: “Ufaransa itatimiza lengo la NATO lililoafikiwa la kuongeza matumizi katika ulinzi kwa asilimia 2 kufikia 2024,” na alisema: “mshikamano wa muungano huu utawezekana tu endapo mzigo huu utashirikianwa kwa usawa.” Alisema: “Trump alithibitisha tena kujitolea kwa Amerika katika mpangilio wa ulinzi, licha ya awali kuonesha shauku na kutotoa vitisho vya moja kwa moja vya kujiondoa wakati wa kongamano mnamo Alhamisi (12/7/2018).” (Chanzo: Reuters, 12/7/2018). Zingatia kwamba Ufaransa kwa sasa inatumia takriban asilimia 1.8 ya uzalishaji wake jumla katika ulinzi. Lakini inafanya kazi kuwa karibu na Amerika ili ipewe dori ya kimataifa ubavuni mwake ili kushibisha hisia za kupenda ukubwa zilizo watawala Wafaransa, lakini pasi na kuachana na Muungano wa Ulaya, mbali na hofu ya kuinuka kwa Ujerumani. Ufaransa wakati mwengine hufanya kazi kwa manufaa ya Muungano wa Ulaya, kama ilivyokuwa hali katika kongamano la hivi karibuni la G-7 nchini Canada, na vita vya kibiashara vya Trump, na katika kudumisha makubaliano ya nuklia ya Iran licha ya Amerika kujiondoa kutokana nayo, na nyakati nyenginezo inaegemea upande wa Amerika mithili ya yale yaliyotokea katika kongamano la Brussels la hivi majuzi.

6- Trump ameonesha kuwa Amerika iko tayari kuachana na NATO, na ingawa hajafanya hivyo sasa, lakini tishio hili lingalipo. Ametangaza vita kwa washirika wake na maadui zake. Huu ni mwelekeo mpya katika sera ya Amerika inayoongozwa na raisi wake aso busara, naye pia yuko tayari kuachana na miungano mengine. Tumesema katika jibu la swali mnamo 16/6/2018 “Yote haya yanaonesha kuwa faili ya vita vya kibiashara ni muhimu mno kwa Amerika, inapoendelea kuteseka kutokana na matunda ya mgogoro wa kifedha uliolipuka mnamo 2008 huku madeni yake yakifikia zaidi ya dolari trilioni 20, na Raisi Trump akili yake iko kwenye biashara akifanya kazi kuuokoa uchumi wa Amerika, akiinua kauli mbiu “Amerika kwanza”. Hili linatishia kuvunjika kwa taasisi za kimataifa zilizotumiwa na Amerika tangu jadi kulazimisha ushawishi wake ulimwenguni na hivyo kuvunjika kwa mfumo wa kiulimwengu na kuibuka kwa msimamo mpya wa kimataifa, ambapo Amerika haijitolei tena mhanga ili kubakia kuwa dola inayoongoza duniani, kwa usaidizi wa nchi nyenginezo na uvumilivu kwa kuifanya mizani ya kibiashara kulemea upande wake, lakini inajali tu ubwana pamoja na faida ya kibiashara pasi na usaidizi kutoka kwa washirika wake ili kuwaweka chini ya mwavuli na kutembea nyuma yake”.

7- Hivyo basi, vita kati ya washirika ni vikali. Huu ni utabiri wa kuvunjika kwa miungano yao na kuzuka kwa vita vya kiuchumi na vya kisiasa baina yao, na lau si hofu yao ya kutumia silaha za kinuklia, kungezuka vita vya tatu vya dunia baina yao kwa misingi ile ile ya vita viwili vya dunia vilivyopita. Washirika hawa ndio chimbuko la uovu duniani, kwa kutabanni kwao mfumo muovu wa kirasilimali, unaofanya manufaa kuwa kipimo cha vitendo, na thamani ya kimada kuwa thamani pekee inayotawala jamii. Hivyo basi, ulimwengu unahitaji sana kuibuka kwa dola ya kheri, dola ya Khilafah Rashida, kwa njia ya Utume, itakayoeneza uroho, akhlaqi na maadili ya utu, na wala haitatafuta tu kupata thamani ya kimada pekee. Na Allah ana waja wenye ikhlasi, ambao ni wakweli kwa Mtume wa Allah, ingawa hatumtakasi yeyote mbele ya Allah, wanaofanya kazi mchana na usiku kupata kheri hii kubwa. Ndimi zao zimelowa utajo wa Allah, na mikono na miguu yao imeshughulishwa na ulinganizi kwa Allah na nyoyo zao zimehakikishiwa Nusra ya Allah.     

إِنَّالَنَنْصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ ﴿

“Hakika Sisi kwa yakini tutawanusuru mitume wetu na wale walioamini katika maisha haya ya dunia na Siku watakayosimama mashahidi” [Ghafir: 51]

4 Dhul Qi’dah 1439 H

Jumanne, 17/7/2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 21:15

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu