Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Ziara ya Mohammad Bin Salman ya Uingereza, Amerika na Ufaransa
(Imetafsiriwa)

Swali:

Mfalme Mtarajiwa wa Saudia, Mohammad Bin Salman, alikamilisha ziara yake nchini Ufaransa, iliyo anza mnamo Jumatatu 09/04/2018 na kuchukua siku mbili hadi 10/04/2018. Awali alizuru Uingereza mnamo 10/03/2018 kwa siku tatu. Ikufiatiwa na ziara ya Amerika, kuanzia 20/03/2018 hadi 08/04/2018 … alipokewa kama kiongozi wa dola. Hivyo basi ni kipi kilicho nyuma ya ziara hizi? Jambo ambalo si la kawaida ni kuwa ziara hizi ni kwenda kwa wahusika wenye maslahi tofauti; ni kipi kilicho sawia baina yao? Tafadhali fafanua jambo hili, na Allah akulipe kheri.

Jibu:

Ziara kuu ya Mohammad Bin Salman (MBS) ni ile ya kwenda Amerika. Ziara yake ya Uingereza ni ziara ya maliwazo, kwa sababu alichukua hatua kali dhidi ya vibaraka wake nchini Saudi Arabia. Ziara yake nchini Ufaransa ni ziara ya pembeni ya kujenga mazingira ya umaarufu kwake, ili isemekane kuwa Bin Salman alizuru nchi kuu barani Amerika na Ulaya; haya hapa ni maelezo yake:

Kwanza: Ziara ya Mohammad Bin Salman kwenda Uingereza:

Ziara ya Mohammad Bin Salman kwenda Uingereza ilianza mnamo 07/03/2018 na kuchukua siku tatu hadi 10/03/2018. Kama tulivyo taja mwanzoni, ilikuwa ni ziara ya kuiliwaza Uingereza, kwa sababu MBS anajua kwamba Uingereza ina mizizi thabiti katika familia ya kifalme ya Saudi na hivyo basi yaweza kumletea yeye matatizo. Na hivyo basi aliizuru Uingereza kujenga mazingira ya utulivu kwa kufunga nayo mikataba ya kiuchumi ingawa haikuwa nyingi.

Hili lilithibitishwa katika taarifa ya mwisho. Ilikuwa karibu na ziara ya kawaida ikiwa na makubaliano ya kawaida kwa maneno jumla yasiyo na ufafanuzi, isipokuwa katika baadhi ya ofa za kiuchumi. Kwa mfano, taarifa hiyo ya mwisho ilieleza:

Uingereza inathibitisha usaidizi wake imara kwa ruwaza ya Saudia ya 2030 na mpango wa kiuchumi na kijamii wa Ufalme wa Saudi Arabia unaolenga upanuzi wa uchumi.

- Mwana wa kifalme Mohammad Bin Salman na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, mnamo Jumatano walizindua Baraza la kila mwaka la Ushirikiano wa Kimikakati kama hatua muhimu ya kuwepo kwa mzungumzo ya mara kwa mara kuimarisha nyanja zote za ushirikiano kati ya nchi mbili hizi …. Saudi Arabia inasifu ujuzi na tajriba ya Uingereza katika sekta mbali mbali za elimu kuanzia elimu ya chekechea, msingi na sekondari mpaka elimu ya juu na mafanikio katika mafunzo ya kiufundi … Saudi Arabia inafahamu ujuzi wa Uingereza katika matibabu … Uingereza imesifu umuhimu wa kuorodheshwa kwa mafanikio kwa kampuni ya Aramco katika soko la hisa kama sehemu ya mpango wa marekebisho ya kiuchumi ya Ufalme wa Saudi Arabia … na Saudi Arabia imeunga mkono msimamo wa London kama kituo kikuu cha kifedha duniani …   

Soko la Hisa la London limekubaliana pamoja na Soko la Hisa la Saudia (Tadawul) juu ya mpango wa kujenga uwezo na mafunzo ili kusaidia kuimarisha masoko ya hisa. Saudi Arabia na Uingereza zimesisitiza umuhimu wa mahusiano ya kiulinzi na kiusalama na dori yao katika kupata kwa pamoja utulivu wa kiusalama na wa kieneo. Nchi mbili hizi zilitangaza nia zao za kuangazia juhudi za kupambana na ugaidi na misimamo mikali kwa kubadilishana habari na kufahamu njia ambazo magaidi na wenye misimamo mikali huzitumia kuyashawishi makundi dhaifu. Nchi mbili hizi zimetia saini maelewano kadhaa ya pamoja kumakinisha zaidi ushirikiano na ushirika baina yao. Pia inajumuisha kutia saini maelewano yenye nia ya kutangaza hamu ya pande hizo mbili ya kukamilisha mazungumzo baina yao ili kufikia makubaliano ya Ufalme huo kupokea ndege 48 ziada za kivita aina ya Typhoon. Nchi mbili hizi pia zilisisitiza haja ya Iran kujifunga na misingi wa ujirani mwema na kutoingilia kati mambo ya kindani ya nchi hizo.

B) Baadhi ya mambo jumla ya kisiasa na ya kiusalama, ambayo hayakuangaziwa au kufafanuliwa kwa suluhisho la kina katika kadhia:

- Nchi mbili hizi zilisisitiza umuhimu wa kufikia suluhisho la kisiasa kwa mgogoro nchini Yemen kwa msingi wa mpango wa GCC na hatua za utabikishwaji wake, na matokeo ya mazungumzo ya kitaifa ya Yemen na azimio la Baraza la Usalama la 2216, ambalo litapelekea kupatikana kwa suluhisho la kisiasa litakalo dhamini usalama wa Yemen na hadhi ya eneo lake. Pande mbili hizi zilidhihirisha uungaji mkono wake imara kwa mjumbe mpya maalumu wa Umoja wa Mataifa (UM) aliyeteuliwa kwa ajili ya Yemen, Martin Griffith … Walikubaliana juu ya umuhimu wa jamii ya kimataifa kushinikiza wanamgambo Mahouthi ili kuruhusu utoaji msaada wa kibinadamu usio na pingamizi … Uingereza iliipongeza Saudi Arabia kwa kuendelea kujitolea ili kuhakikisha kampeni hiyo ya muungano wa majeshi iko sambamba na kanuni ya kimataifa ya kibinadamu … nchi mbili hizo zilithibitisha upya kujitolea kwao kwa suluhisho la kuwepo nchi mbili, kwa msingi wa Mpango wa Amani wa Waarabu na maazimio muwafaka ya UM.   

C) Baadhi ya mikataba ya kiuchumi yenye nia ya kuliwaza, kama natija ya matendo ya Bin Salman dhidi ya vibaraka wa Uingereza:

- Saudi Arabia na Uingereza zimejitolea katika ushirikiano wa muda mrefu kusaidia kupatikana kwa Ruwaza ya 2030, ili kujumuisha sekta nyingi, ikiwemo: kutathmini fursa za uwekezaji wa pamoja na Uingereza (na kupitia) Hazina ya Uwekezaji wa Ummah na biashara ya pamoja kati ya nchi mbili hizi…fursa hizi kwa pamoja zitagharimu dolari bilioni 100 kwa zaidi ya miaka 10, ikiwemo Hazina ya Uwekezaji wa Ummah (PIF) huku uwekezaji wa moja kwa moja ukigharimu dolari bilioni 30.

- Uingereza na Saudi Arabia zimekaribisha mikataba kadhaa mikubwa ya kibiashara waliyokubaliana pamoja wakati wa ziara hiyo; zinatarajiwa kuzidi dolari bilioni 2, kuunda na kudhamini nafasi za kazi na ufanisi nchini Saudi Arabia na Uingereza.

Ni wazi kutokana na hili kuwa ziara hiyo haiendi zaidi ya lengo lake, ambalo ni kuliwaza na kutuliza, takriban ziara yote ilikuwa ubadilishanaji jumla wa maneno, isipokuwa katika baadhi tu ya ahadi za kiuchumi, ambazo si muhimu na wala hazina uzito.  

Pili: Ziara ya Mohammad Bin Salman kwenda Amerika:

Mfuatiliziaji wa ziara ya MBS kwenda Amerika ataona kuwa Amerika inamuunda MBS kuwa mtumwa mtiifu kwake; inamdhalilisha mbele ya uso wake naye anatabasamu na inamtishia naye anajisalimisha; huu hapa ufafanuzi wake:

1) Baada ya kuchukua utawala baada ya kifo cha kakake, Abdullah, mnamo 23/1/2015, Mfalme Salman alianza mipangilio ya haraka ya kumakinisha utawala wake na wale watakao kuja baada yake. Alimng’oa kakake, Muqrin bin Abdulaziz kutoka katika cheo cha Mfalme Mtarajiwa, ambaye ni mtiifu kwa Uingereza, na kumteua mwanawe Mohammad Bin Salman (MBS) kama Mfalme Mtarajiwa, na kumkabidhi nguvu nyingi za kuimarisha utawala wake. Aliwang’oa na kuwatenga wengi wa wapinzani wake na wale ambao ni vibaraka wa Uingereza katika familia yake, na kuonesha utiifu wake mkubwa kwa Amerika. Hatua ya pili ilikuwa ni kuwafanya Waamerika kuwa karibu zaidi na MBS na uwezo wake, ili kumfahamu vizuri na kupima utiifu wake kwa Amerika. Hivyo basi alizuru Washington mnamo 15/3/17 baada ya kutawazwa rasmi kwa Trump kama Raisi wa Amerika, na Trump alimpokea kwa daraja ya juu katika ikulu ya White House mbele ya makamu wake wa raisi, Pence, na usalama wake wa taifa wa Amerika, akinyanyua daraja ya ziara hiyo. Trump alionesha uungaji mkono wake kwa Bin Salman. Hatua nyengine ilijiri mnamo 4/11/2017 ili kuimarisha mamlaka ya MBS kwa kukata mbawa za vibaraka wa Uingereza na wengineo na kumueka kila mmoja ndani ya udhibiti wake, na kuwadhalilisha na kutishia kufunga akaunti zao, ambapo mamia ya wana wafalme, mawaziri, ma-afisa na wafanyi biashara waliwekwa kizuizini  kwa kisingizio cha kupigana na ufisadi. Alitangaza kuwa alikusanya kutoka kwao dolari bilioni 100.    

Na hivi sasa, inakuja hatua nyengine kabla ya mwisho; ziara yake kwenda Washington kwa mara ya pili ili kuimarisha utiifu wake kwa Amerika na kuimarisha mafungamano yake kwake na kufanya matayarisho kwa hatua ya mwisho, kuteuliwa kwake kama mfalme halisi katika wakati wanaotarajia hivi karibuni. Pindi Bin Salman alipoanza ziara zake za kigeni, alipokewa kama mfalme, kama ilivyo tokea nchini Misri mnamo 4/3/2018, na ziara yake ya Uingereza mnamo 7/3/2018 ambapo alipokewa na Malkia, na kisha kufuatiwa na mapokezi na ziara ndefu nchini Amerika zinazo thibitisha hili. Trump alitaja hili alipozungumza na Bin Salman: “Kumekuweko na mambo mazuri tangu ziara yako ya mwisho ikuluni White House. Wewe ndiye mfalme mtarajiwa” wakati wa ziara yako ya mwisho, alisema, “na sasa wewe ni zaidi ya mfalme mtarajiwa.” (Chanzo: Russian Sputik 21/3/2018) 

2) Kwa hivyo punde tu Bin Salman alipofika Washington, alikutana na Raisi Trump mnamo 20/3/2018 M. Trump alisema: “Ni heshima kubwa kuwepo na Mfalme Mtarajiwa pamoja nasi, Saudi Arabia imekuwa rafiki mkubwa … Nilikuwa nchini Saudi Arabia mnamo Mei. Na tunaziregesha bilioni za dolari nchini Amerika … Na kitu chengine ambacho ninafuraha nacho zaidi ni kuwa tulizungumzia kuhusu uwekezaji ulio na thamani ya dolari bilioni 400,” Aliendelea: “Tunafahamiana. Saudi Arabia ni taifa tajiri mno, na twatarajia wataipa Amerika baadhi ya utajiri huo, kwa njia ya ajira, kwa njia ya ununuzi wa vifaa bora vya kijeshi duniani kote.”

Bin Salman alijibu: “mahusiano kati ya Saudi Arabia na Amerika, ni mahusiano ya jadi … zaidi ya miaka 80 ya muungano na maslahi makubwa – kisiasa, kiuchumi, na kiusalama, katika kila eneo – maeneo mengi … Na msingi wa uhusiano huo, ni mkubwa sana na wenye kina kikuu … tulipanga kutumia dolari bilioni 200 kwa ajili ya fursa za miaka minne ijayo, lakini ikaishilia kuwa dolari bilioni 400 kwa ajili ya fursa hizo”. (Chanzo: CNN 20/3/2018).

Amerika inaitishia Saudi Arabia na kufuja mali ya Waislamu kupitia watawala hao waliokhini amana na kuukhini Ummah. Anachojali Trump na Waamerika ni kufyonza pesa za Waislamu kupitia familia ya Saud, waliotangaza utiifu wao na muungano wao kwa makafiri, na kuwahudumia kwa kulinda maslahi yao eneo la Mashariki ya Kati, na kwa kufadhili uchumi wao na kulipa gharama zote za kulinda maslahi yao.

3) Trump alionesha karata zake mbele ya kamera na kuziweka dhidi ya kifua cha Bin Salman kwa michoro na picha za silaha ambazo Saudi Arabia itazinunua kutoka Amerika na itazipokea hivi karibuni. Alizihesabu dili na aina za silaha zenye thamani ya mabilioni, akimwambia kuwa: “Hiyo ni kidogo sana kwako.” Trump alisema: “Dili hizi zitazalisha nafasi mpya za kazi (nchini Amerika) na zinatarajiwa kufikia nafasi za kazi elfu 40.” (Chanzo: Sputnik Russian 21/3/2018). Kinacho bakia ni kuwa Trump anaweka kamba katika karata hizo na kuifunga shingoni mwa Bin Salman kana kwamba anamtumia ujumbe kuwa usaidizi wetu kwako ni kwa badili kiwango gani cha pesa utakazo tupa, na kuitoa ardhi kwa matumizi yetu, na kufanya kila kitu tunacho agiza bila ya pingamizi yoyote. Kitendo hiki kilikuwa ni tusi kwa Bin Salman aliyejibu kwa tabasamu kama bwege huku Trump akionesha jeuri na kutojali. 

4) Wakati wa ziara ya MBS, alikutana na maafisa katika idara hiyo na sekta nyenginezo muhimu:

A) Alikutana na Waziri wa Ulinzi wa Amerika, Mattis, na Mkuu wa Majeshi, Danford, akithibitisha utiifu wake kwa Amerika: “Changamoto za leo sio za kwanza ambazo nchi mbili hizi zimekabiliana nazo. Leo tunakabiliana na changamoto kali zaidi eneo hili na ulimwenguni, ima kutokana na vitendo vya serikali ya Iran au changamoto za makundi ya kigaidi,” alisema. (Chanzo: Gazeti la Saudia la Al-Wi’am 24/3/2018). “Ni lazima pia tuimarishe juhudi za haraka za kutafuta azimio la amani la vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen na tunakuunga mkono kwa hili.”, “Waziri wa Ulinzi wa Amerika, Mattis, alimwambia Mfalme Mtarajiwa Mohammad Bin Salman. “Tutavimaliza vita hivi na kwa njia nzuri kwa watu wa Yemen, hii ni kwa uchache”, pia aliahidi kufanya kazi na Riyadh kuimarisha “utulivu na usalama” eneo hili (Chanzo: Reuters, 22/3/2018). Kadhia ya Yemen ni kadhia ambayo Amerika bado haijafanikiwa kupata malengo yake ya mwisho, na Saudi Arabia, ambayo inafanya kazi hiyo ya kufanikisha kupatikana kwa malengo ya Amerika, bado iko katika mgogoro na bado haijaweza kujitoa ndani yake. Mwisho wa kadhia hii na kujiondoa salama kwa Saudi Arabia kutaimarisha mamlaka ya Bin Salman.   

- Bin Salman alitoa taarifa kwa jarida la Time mnamo 31/3/2018 ambapo alisema: “Tunaamini vikosi vya Amerika ni sharti vibakie kwa muda wa angaa nusu muhula, ikiwa si kwa muda mrefu … Amerika inahitaji kuwa na karata za kujadiliana na kutia shinikizo. Ukivitoa vikosi hivi nje, utapoteza karata hii” … “Bashar anabakia”, alisema. “Lakini naamini kuwa maslahi ya Bashar sio kuwaruhusu Wairan kufanya chochote wanachotaka kufanya.” Raisi wa Amerika Trump alisema mnamo Jumanne 3/4/2018: “Nataka kutoka (nchini Syria). Nataka kuviregesha vikosi nyumbani. Nataka kuanza kujenga upya taifa letu.”

“Kuhusiana na Syria, kazi yetu msingi ilikuwa ni kuiangamiza ISIS. Tunakaribia kukamilisha kazi hiyo. Na tutafanya uamuzi kwa haraka kwa ushirikiano na wengine katika eneo hili wa kipi tutakacho fanya. Saudi Arabia inahamu ya uamuzi wetu. Na nimesema, wajua, munataka sisi tubakie, na huenda mukalipia hilo.” (Chanzo: AFP, 3/4/2018). Hivyo, Trump anaendeleza sera ya vitisho kwa serikali ya Al Saud, ambayo inaumakini wa kudumisha ushawishi wa Amerika eneo hilo.

Pia alitoa taarifa kwa jarida la Atlantic mnamo 2/4/2018 alipoulizwa: “Je, unadhani Mayahudi wana haki ya kuwa na taifa angaa katika baadhi ya sehemu za ardhi ya mababu zao?” alisema:

“Naamini kuwa kila mtu, popote pale, ana haki ya kuishi katika taifa lao la amani … Naamini Wapalestina na Waisraeli wana haki ya kuwa na ardhi zao wenyewe.” (Chanzo: Tovuti ya Kisaudi ya Al Wi’am 3/4/2018)

Bin Salman hakuficha khiyana yake hata dhidi ya Ardhi Tukufu, ardhi ya Isra na Miraj.

- Na kwa jina la burudani, aliweka bajeti kubwa. Mwenyekiti wa Mamlaka Jumla ya Burudani nchini Saudi Arabia, Ahmed Bin Aqeel Al Khatib, alitangaza “nia ya mamlaka hiyo ya kuwekeza mpaka riyal bilioni 240, sawia na dolari bilioni 64 katika sekta ya burudani kwa miaka kumi ijayo.” Na kutangaza kujengwa kwa Jumba la Opera, la kwanza tangu kubuniwa kwa Ufalme huo” (Chanzo: Tovuti ya Al Arabiya 22/2/2018).

- Gazeti la Washington Post, mnamo siku ya nne na ya mwisho ya ziara yake jijini Washington na mkutano na maafisa wake mnamo 24/3/2018, lilifanya mahojiano na Bin Salman aliyesema, “Wakati wa mkutano huo, vita nchini Yemen, mpangilio wa amani wa Mashariki ya Kati, Iran, mpangilio wa mageuzi wa kindani, na matarajio ya Saudia ya nuclear yalizungumzwa.” Alisema kazi yake kubwa nchini Amerika ni kujishindia imani ya wawekezaji wa Amerika ikiongezewa na kupata usaidizi wa kiteknolojia na wa kielimu ili kusaidia juhudi za mageuzi nchini Saudi Arabia.  Alisema kwa kadhia za magazeti kuhusu kuwapa wanawake nyingi ya haki zao … Hii yamaanisha kuwa faili za eneo zima zilifunguliwa mbele yake na kuzungumzwa pamoja naye. Kwa hivyo anajua namna ya kuyatekeleza na kukimbilia usaidizi wake na utekelezwaji wake na Waamerika. Sehemu ya swali la Yemen, kuna mpango wa Trump katika Mashariki ya Kati na suluhisho kwa suala la Palestina; yeye (Trump) alisema kuwa atatangaza mpango katika miezi ijayo baada ya kuitambua Jerusalem kama makao makuu ya umbile la Kiyahudi ambalo yeye (Bin Salman) atafanya maridhiano nalo, pamoja na kubadilisha sera ya ndani ya Saudia kwa  kile Amerika inachotaka; ili kuifanya nchi hiyo kuwa ya kisekula na kupenyeza maadili ya hadhara ya Kimagharibi ndani yake, pamoja na kuwapa wawekezaji wa Kiamerika fursa za kuudhibiti kikamilifu uchumi wa nchi hiyo.   

Tovuti ya Arabic 21, mnamo 29/3/2018, ilinukuu gazeti la Kiingereza la The Independent likisema kwamba limeona mpango wa Mfalme Mtarajiwa wa Saudia, Mohammad bin Salman, ambao unajumuisha mikutano ya wakuu wa makampuni makubwa, wanasiasa, wenye mafuta, na wafanyi kazi katika teknolojia, burudani na sanaa unalenga kushikilia kandarasi kwa rai jumla ya Kiamerika. Kituo cha habari cha CBS kilifanya mahojiano naye katika kipindi “Sixty Minutes”, mahojiano ya kwanza ya kituo hicho kuwahi kumfanyia kiongozi wa Kisaudi kwa miongo kadhaa. Alitumia fursa hii kuboresha sura yake kama mwanamageuzi mchanga mkakamavu anaye tekeleza mageuzi muhimu, kama vile kudhibiti mamlaka ya polisi wa kidini na kuruhusu wanawake kuendesha magari. Gazeti hilo lilitaja kuwa alikutana na maafisa wa zamani mnamo Jumanne (27/3/2018) kama Kissinger, Bill Clinton na Hillary Clinton na wengineo, na wamiliki wa mageti makubwa, na atakutana na Raisi wa zamani Obama, na Waziri wa Kigeni wa zamani John Kerry, na David Petraeus.

- Bin Salman alionesha kujisalimisha zaidi na unyenyekevu zaidi alipotuma, baada ya kuondoka Amerika na kuelekea Ufaransa, ujumbe wa utiifu kwa Trump wa Amerika, ambao alisema: “Mheshimiwa, Raisi Donald Trump wa Amerika, salamu: Nina furaha wakati ninapo ondoka nchi yako, mshirika wetu, kudhihirisha shukrani zangu kwako kwa ukarimu wako kwangu na wajumbe nilio andamana nao, na kuchukua fursa hii kutoa heshima zangu kwa mara nyengine tena kwa mahusiano ya kihistoria na kistratejia baina ya nchi zetu mbili, ambazo zinashuhudia maendeleo zaidi katika nyanja zote, na siwezi kukosa kusisitiza kuwa mazungumzo yaliyo fanyika wakati wa ziara hii yatachangia katika kumakinisha zaidi mahusiano haya na kuyaimarisha, na kuimarisha mafungamano ya ushirikiano wa pamoja … nakutakia afya njema na furaha, na kwa watu wa Amerika kudumu na maendeleo na ufanisi”   

Tunatamatisha kuzungumzia ziara hii kwa kurudia yale tuliyo yasema mwanzoni. (Mfuatiliziaji wa ziara ya Bin Salman kwenda Amerika ataona kuwa Amerika inamuunda Bin Salman kama mtumwa wake mtiifu; inamdhalilisha mbele ya uso wake na huku anatabasamu na kumtishia na huku anajisalimisha).

Tatu: Ziara ya Mohammad Bin Salman kwenda Ufaransa:

1) Ziara hii ya Bin Salman kwenda Ufaransa ni ziara ya mapito pembeni kujenga mazingira ya umaarufu kwa Bin Salman, ili isemekane kuwa alizuru Magharibi, kuanzia Uingereza mpaka Amerika na kisha Muungano wa Ulaya (Ufaransa). Na kwa sababu ya kukosekana umuhimu wa ziara hii, imekosa hata mpangilio wa kidiplomasia wa ziara za kimataifa. Kwa mfano, “Afisa katika afisi ya waziri mkuu wa Ufaransa alisema mnamo Jumatatu kwamba Mfalme Mtarajiwa wa Saudia alifutilia mbali ziara yake katika jumuiko kubwa la kampuni zinazoibuka za teknolojia jijini Paris kuangazia kina cha mahusiano ya kiteknolojia kati ya Ufaransa na Saudia. Kwa mujibu wa gazeti la LA Tribune: kufutiliwa huko kwa ziara ya mwana wa mfalme Mohammad kwa kituo cha “Station F” huenda ikamuacha Macron kuhisi bugudha, hususan kwa kuwa katika ziara ya Bin Salman kwa magwiji wa teknolojia katika Bonde la Silicon nchini Amerika wiki iliyo pita, Bin Salman aliweka sharti la kuzuru kawanda hili lililo amsha hasira za Macron …”.  

Mtandao wa Arab World mnamo 09/04/2018, ukinukuu (© REUTERS / POOL) uliripoti:

LA Tribune lilifichua kuwa Mfalme Mtarajiwa wa Saudia Bin Salman amemkasirisha Raisi wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kuweka sharti kwa kampuni za Kifaransa kunufaika kutokana na kandarasi za kibiashara na Ufalme huo, gazeti hilo lilisema. “Bin Salman alimueleza Macron kuwa kampuni za Kifaransa, kama vile kampuni za Kiamerika, huenda zikanufaika kutokana na kandarasi za Ufalme huo, maadamu tu hazitafanya biashara na Iran, likiongeza kuwa sharti hili liliamsha hasira za Macron”.

2) Na kile walichokuwa “wakiringia” kuhusu kandarasi ya ushirika wa kistratejia haikutiwa saini, lakini wakaakhirisha saini hiyo kwa miezi minane hadi mwisho wa mwaka wa 2018.

Inajulikana kuwa mabadiliko katika sera ya kimataifa huwa ya haraka. Hivyo basi, ahadi za kutia saini makubaliano hayo au kukamilishwa kwa kandarasi hizo aghalabu hazitimizwi hususan ikiwa makataa ni marefu. Duru za karibu na afisi ya Raisi wa Ufaransa zimewatangazia maripota kuwa Macron na Mohammad Bin Salman watatayarisha hati ya kistratejia ambayo itakuwa tayari mwishoni mwa mwaka huu. Hii itapelekea kuwepo kwa kandarasi ambazo zitapelekwa (na Macron) Saudi Arabia mwishoni mwa mwaka huu kwenda kutiwa saini (Chanzo: Al Bayan 10/4/2018). Mtandao wa Al Arabiya pia uliripoti mnamo Jumatatu 9/4/2018: “Raisi na mwana wa mfalme watafanya kazi pamoja juu ya hati ya kistratejia ambayo itakuwa tayari kufikia mwishoni mwa mwaka huu na kuzalisha kandarasi zitakazotiwa saini pindi Macron atakapo kwenda Saudi Arabia kabla ya mwisho wa mwaka huu,” haya pia yaliripotiwa na shirika la habari la France 24, mnamo 09/04/2018.

3) Zaidi ya hayo yale ambayo Raisi wa Ufaransa ametangaza yamo ndani ya muundo wa matarajio na chini ya mipangilio inayo hitaji kujadiliwa na kushauriwa ili kandarasi hizo ziwe barabara:  

“Tunatarajia ushirikiano mpya, unao angazia kwa uchache kandarasi za sasa na zaidi uwekezaji kwa ajili ya mustakbali, hususan katika nyanja za dijitali na kawi,” afisi ya Raisi wa Ufaransa imesema. (Chanzo: AFP 05/04/2018)

Ziara ya Muhammad Bin Salman nchini Ufaransa inatarajiwa kutamatisha kutiwa saini kwa baadhi ya makubaliano ya mikataba katika nyanja tofauti tofauti, kama vile utalii, ambapo Paris itaisaidia Riyadh kuangazia eneo la Al Hijr (Mada’in Salih) iliyo orodheshwa na shirika la UNESCO kuwa Turathi ya Kiulimwengu katika eneo la kaskazini magharibi mwa Ufalme huo pamoja na nyanja nyenginezo kama afya, kawi, uchukuzi, nk. (Chanzo: AFP, 08/04/2018)   

4) Hivyo basi, hakuna kandarasi za maana za kiuchumi zilizotiwa saini katika ziara hii, kwa sababu ilikuwa ni ziara fupi (siku mbili), iliyo sababisha fedheha kwa Kasri la Elysee. Hii ndio sababu jibu la swali kuhusu ziara fupi ya mwana wa mfalme wa Saudia nchini Ufaransa baada ya ziara ya wiki tatu nchini Amerika, lili eleza: Kasri la Elysee linakaribisha kujumuishwa kwa Ufaransa kama mojawapo ya ziara za kwanza za kigeni za Mfalme Mtarajiwa … (Chanzo: France 24 / AFP 05/04/2018), na kutotia saini kandarasi hizo pia kulisababisha fedheha kwa kasri la Elysee: “Kwa upande mwengine, duru za kidiplomasia za Ufaransa zililiambia shirika la habari la France 24 kuwa Ufaransa “haifuatilii kandarasi za kibiashara na Saudi Arabia kama ilivyokuwa nyuma, bali inatafuta kujenga ushirika wenye maono sawa yaliyo jengwa kwa msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia ya muda mrefu”. (Chanzo: AFP, 08/04/2018)

5) Kutokana na yote hayo juu, ili kuitendea haki ziara hiyo, kuna makubaliano ambayo tayari yashatiwa saini, makubaliano yaliyouteka moyo wa Bin Salman; makubaliano hayo yalitiwa saini kuasisi bendi ya kitaifa na jumba la burudani, wapi huko? Katika ardhi ya Misikiti miwili Mitukufu!! Waziri wa Utamaduni wa Ufaransa Françoise Nyssen alisema Paris itaisaidia Riyadh kuunda bendi na kujenga jumba la burudani,” Nyssen alisema haya baada ya kutia saini makubaliano na Waziri wa Utamaduni na Habari Awad al-Awad jijini Paris. (Chanzo: tovuti ya Arab World mnamo 09/04/2018 (© REUTERS / POOL)

Bin Salman kabla ya makubaliano haya alifanya ziara mnamo Jumapili kabla ya ziara yake rasmi, alihudhuria tamasha la sherehe za Pasaka kusini mwa Ufaransa: Mwana wa Mfalme Salman aliwasili mnamo Jumapili 08/04/2018 akitokea Amerika. Anahudhuria tamasha la sherehe za Pasaka katika mji wa Aix-en-Provence karibu na mji wa Marseille kusini mwa nchi hiyo kufurahia mziki wa waandishi wa kale Debussy, Robert Schumann na Felix Mendelssohn. (Chanzo: AFP 08/04/2018)

6) Kwa hivyo ziara hiyo haikuwa na maana si kwa upande wa makubaliano wala kwa upande wa kandarasi, isipokuwa ikiwa jumba hilo la burudani litachukuliwa kuwa na maana, twajilinda na Allah kutokana na hili! Hili lilikuwa dhahiri katika mkutano wa mwisho wa waandishi habari uliofanywa mnamo Jumanne 10/4/2018, na kuchapishwa katika vyombo vya habari mnamo 11/4/2018. Ulieleza kuwa mikataba na makubaliano ya makusudi iliafikiwa, isipokuwa ya jumba la burudani, tayari ishatiwa saini! Mtandao wa Aljazeera net ulichapisha mnamo 11/4/2018:

Mfalme mtarajiwa wa Saudia Mohammad Bin Salman alitamatisha mnamo Jumanne ziara ya siku mbili nchini Ufaransa kwa kutia saini kandarasi za makubaliano 19 baina ya Ufaransa na kampuni za Kisaudi zenye jumla ya thamani ya zaidi ya dolari bilioni 18. Makubaliano hayo yaliyo afikiwa yanahusu sekta za viwanda kama kemikali za petroli na matibabu ya maji, vile vile utalii, utamaduni, afya na kilimo … miongoni mwa makubaliano makubwa ni tangazo la kampuni ya mafuta ya Kisaudi ya Aramco, la kutia saini makubaliano yenye thamani ya zaidi ya dolari bilioni 12 pamoja na kampuni za Kifaransa, zikiwemo, Total, Technip na Suez ya kuunda kwa pamoja kiwanda cha kemikali za petroli eneo la Jubail (Mkoa wa Kaskazini wa Saudi Arabia), ambao kampuni za Kifaransa zinamiliki kiwanda kikubwa zaidi cha kusafisha mafuta duniani. Hata makubaliano haya na Aramco hayakufungika tu na kuimarisha biashara ya Aramco, bali yanaangazia zaidi juu ya kuimarisha mapato ya kifedha ya kiwanda hicho cha usafishaji mafuta cha Kifaransa. 

Hili pia liliripotiwa na shirika la habari la AFP mnamo 11 Aprili 2018, kutoka katika mkutano huo wa waandishi habari. Duru hiyo pia inasema: “Mwishoni mwa ziara ya Mfalme Mtarajiwa wa Saudi nchini Ufaransa mnamo Jumanne, nchi hizo zilitia saini kandarasi za makubaliano 19 baina ya kampuni za Kifaransa na za Kisaudi zenye jumla ya thamani ya zaidi ya dolari bilioni 18. Barua hizo za maafikiano zinahusu sekta za viwanda kama vile kemikali za petroli na matibabu ya maji, vile vile utalii, utamaduni, afya na kilimo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baraza la kibiashara kati ya Ufaransa na Saudia, linalo jumuisha waajiri na wawakilishi wa serikali zote mbili”.  

Katika mkutano huo wa waandishi habari, Macron na Bin Salman walitaja kadhia za kawaida kama vile Iran, makubaliano ya nuklia, Syria, Yemen, nk. pasi na kufafanua suluhisho halisi la kadhia hizi.

Nne: Tamati:

Tunarudia yale tuliyo yasema juu: Ziara kuu ni ile ya kwenda Amerika; ziara yake ya Uingereza ni ziara ya maliwazo kwa sababu ya kuchukua kwake hatua kali dhidi ya vibaraka wake (Uingereza) nchini Saudi Arabia. Ziara yake nchini Ufaransa ni ziara ya pembeni ya kujenga mazingira ya umaarufu kwa Bin Salman, ili isemekane kuwa alizuru nchi kuu barani Amerika na Ulaya.

24 Rajab 1439 H

Jumatano, 11/4/2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 21:21

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu