Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali:
Ghasia Mpakani kati ya China na India
(Imetafsiriwa)

Swali:

Shirika la habari la Reuters lilichapisha mnamo 10/06/2020: "… Maafisa wa India wameripoti kuwa mamia ya wanajeshi wamewekwa sako kwa bako katika kijiji cha Ladakh eneo lenye barafu tangu Aprili katika ghasia hatari zaidi za mpakani kati ya pande mbili hizi kwa miaka, baada ya doria za China kuingia katika ule upande ambao India inachukulia kuwa ni wake wa mipaka halisi, na China inadai kwamba eneo hilo ni lake, na kupinga ujenzi wa barabara wa India katika eneo hilo." Eneo hilo la mpakani kati ya China na India limeshuhudia ghasia baina ya walinzi wa mipaka wa nchi hizi mbili tangu wiki ya kwanza ya Mei. Je, lengo ni la kindani, au Amerika iko nyuma yake ili kuihangaisha na kuishinikiza China? Na ni ipi athari ya mzozo huu kwa Waislamu katika Kashmir Iliyo Kaliwa, na Pakistan?

Jibu:

Ghasia za mpakani zilizo zuka mnamo 5 Mei iliyopita, katika Bonde la Galwan katika eneo la nyanda za juu la Ladakh kaskazini mashariki mwa India, na kisha baada ya siku tatu katika barabara ya mlima Nathula (katika Himalayas na yenye kuunganisha jimbo la India la Sikkim na eneo la Tibet). Ghasia hizi zilipelekea sintofahamu ya kijeshi na kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Historia ya uhasama katika mahusiano baina ya China na India ni ndefu, na hutokea mara kwa mara kunapotokea mzozo wa mipaka ambayo Waingereza waliichora mnamo 1980 pamoja na China katika makubaliano yanayojulikana kama Sikkim Tibet, walipolitawala eneo hilo na kulikoloni bara hindi la Kiislamu kwa njia ya moja kwa moja. Walipoondoka huko, waliligawanya kuwa India na Pakistan, na kuiacha Kashmir kuwa kama eneo la mlipuko baina yao… na hivyo ndivyo pia walivyo fanya kwa India na China ili kuchochea mzozo juu ya maeneo mingi ya mpakani. Ili kufafanua yaliyojiri hivi karibuni, tunatathmini yafuatayo:

Kwanza: Ghasia hizi za mpakani kati ya India na China sio za kwanza kwa aina yake. Majeshi ya nchi hizo mbili yalisimama ukingoni mwa vita kwa viwango tofauti katika miaka ya 2013, 2014, 2017, hii ni katika muongo uliopita pekee. Na nchi hizo mbili zilipigana vita vikali vya mpakani mnamo 1962 ambapo India ilishindwa na China kuikali Aksai Chin, kaskazini mwa Kashmir. Mzozo kati ya nchi hizi mbili katika mipaka ya mashariki ni matokeo ya ukoloni wa Uingereza na kuunganishwa kwa jimbo la Arunachal Pradesh na India, na kutochorwa mipaka na China katika kipindi chote cha ukoloni wa Uingereza kwa India. Ama mzozo juu ya mipaka ya magharibi, ni kutokana na ulafi wa nchi hizo mbili juu ya Kashmir ya Kiislamu hususan baada ya 1947. Lakini kutokana na mizozo hiyo ya mipaka, nchi zote mbili zilichapisha kwa upana data tofauti, hata kuhusu urefu wa mpaka kati yao, ambapo ni takriban kilomita elfu nne.

Ama makabiliano ya mnamo tarehe tano Mei iliyopita, yalitokea pindi majeshi yalipogongana katika kingo za theluji ya Pangong Tso, iliyo na kimo cha futi elfu 14, katika muinuko wa Tibetan, na kujeruhi wanajeshi kadhaa katika pande zote. Tangu wakati huo, kuyapa nguvu majeshi kumekuwa kukiendelea huku makabiliano yakiendelea. Tayari China imetuma takriban wanajeshi 5,000 na magari ya kijeshi katika eneo la mpakani linalozozaniwa la Ladakh. ["Gazeti la The Business Standard liliripoti kuwa zaidi ya wanajeshi 5,000 wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa China walivamia vituo vitano eneo la Ladakh na vinne kando kando ya Mto Gallowan, na kimoja karibu na Ziwa Pangong…"(www.defense-arabic.co 24/5/2020)].

Pili: Matukio baina ya nchi hizi mbili yamepamba moto baada ya India kulitenganisha jimbo la Ladakh kutoka Jammu na Kashmir. China ilifahamu kuwa utenganishaji wa Ladakh kutoka kwa Jammu na Kashmir ulikuwa ni kwa sababu za kimikakati ili kuendeleza makabiliano makali ya India dhidi ya China tangu Waziri Mkuu Narendra Modi aingie madarakani mwaka wa 2014 kama kiongozi wa serikali iliyoundwa na Chama cha Bharatiya Janata (BJP). Msemaji wa Wizara ya Kigeni ya China alisema akijibu tangazo la Amit Shah mnamo 5/8/2019 la nia ya India ya kuitenganisha Ladakh: "marekebisho ya India ya upande mmoja ya sheria yake ya ndani yana madhara kwa China na yanakiuka ubwana wa kieneo, na hili halikubaliki." Mizozo ya mpaka ambayo daima huzuka baina ya nchi hizi mbili iko katika mitazamo miwili mikuu: Wa kwanza ni juu ya mpaka wa mashariki, ambako China inataka kuliunganisha jimbo la Aurichal Pradesh lenye ukubwa wa kilomita 90,000 mraba na China inaliita Tibet kusini, ambapo India inakataa.

Mtazamo wa pili ni kuwa India inataka kurudishwa kwa ardhi zilizochukuliwa na China katika vita vya 1962 katika mipaka ya magharibi, yaani katika eneo la Kiislamu la Kashmir, ambalo ni eneo la Aksai Chin lenye ukubwa wa kilomita 38,000, ambalo ni nusu jangwa lililo na idadi ndogo ya watu, ambapo China inakataa. Bali China inataka ubwana zaidi wa eneo la Kashmir. Hivyo, matakwa ya China leo yamemakinika katika mipaka ya magharibi katika sehemu ya eneo la Kashmiri Ladakh linalopakana na eneo la Aksai Chin, ambalo lilikuwa sehemu ya njia za zamani za biashara za China, Barabara ya Silk.

Tatu: Eneo la Ladakh ambalo ghasia za hivi karibuni kati ya India na China zilitokea ni eneo la Kiislamu na sehemu muhimu ya Kashmir, lilitawaliwa na Uislamu kwa karne nyingi, na lilikuwa ndani ya jimbo la Jammu na Kashmir, hadi lilipotenganishwa na sheria mnamo 31/10/2019! Ni eneo lililo na idadi ndogo ya watu lakini lenye thamani kubwa ya kistratejia, ndio muinuko mkubwa zaidi wa India na inajumuisha bonde la Mto Hindus uliojuu, linapatikana katika Mpaka Halisi wa Udhibiti (LAC) wa China upande wa mashariki, na Mpaka wa Udhibiti (LoC) wa Pakistan upande wa magharibi, na upande wa kaskazini liko eneo la Karakorum. Vilevile, vijiji vya mwisho vya India kabla ya Karakorum ni Dola Beck Olde na kwa ajili ya taarifa, hii kwa lugha ya Kituruki yamaanisha "sehemu ambayo mtu mtukufu na tajiri alifariki." Inasemekana kuwa anakusudiwa Sultan Saeed Khan, mtawala wa Yarkand aliyekuja katika kampeni moja ya ukombozi mnamo 938 H, msimu wa kipupwe wa 1531 M, ili kuifungua Ladakh na Kashmir kwa Uislamu, na alipokuwa anarudi Yarkland mwishoni mwa 939 H aliumwa sana na inasemekana kuwa alikufia sehemu hii. Hivyo, ni ardhi ya Kiislamu na sasa India inaidhibiti ndani ya maeneo ya udhibiti wake katika jimbo la Kashmir, jimbo ambalo lina majeraha juu ya majeraha, kama ambavyo India inaidhibiti Jammu, Bonde la Kashmir, na Ladakh, China inaidhibiti Aksai Chin na barabara inayopitia Karakorum, ambayo yote ni maeneo ya Kiislamu katika jimbo la Kashmir. Huku Pakistan ikidhibiti tu eneo la Azad Kashmir na Gilgit-Baltistan pekee, ambayo pengine ni chini ya thuluthi moja ya ukubwa wa jimbo hilo. Azad Kashmir inapakana na maeneo yaliyo chini ya uvamizi wa India huku Gilgit ni jirani na maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa China na India. Kutokana na hali ya sasa ya udhaifu wa nchi za Kiislamu, hususan Pakistan, India inadai haki yake ya maeneo yanayo zozaniwa ya Ladakh kama sehemu ya jimbo la Jammu na Kashmir, huku China ikijibu na kudai haki yake ya maeno hayo kwa sababu ni sehemu ya jimbo la Xinjiang, yaani Turkestan Mashariki, nchi hizi mbili zinazozania haki na kuyang'ang'ania maeneo haya ya Kiislamu, huku Pakistan ikiendelea kuitumikia Amerika na Waislamu wengine wakisalia kimya!!

Nne: China inalitazama eneo la Ladakh, ambalo liko chini ya udhibiti wa India, kwa njia spesheli. Mbali na kuwepo kwa mabudha katika eneo hili, zimo njia mbili za zamani za biashara zinazofika Asia ya Kati, na uhalisia huu una umuhimu mkubwa katika mkakati mpya wa China, Barabara ya Silk. Ingawa kuna njia nyenginezo kwa China kufika Asia ya Kati, lakini, barabara ya kupitia Ladakh ni fupi zaidi katika kufikia vituo na masoko yaliyo na idadi kubwa ya watu katika Asia ya Kati. Jambo linaloongeza zaidi uzingatiaji huu pia ni kuwa njia hizi za zamani za biashara zinafupisha masafa mengi katika kufikisha bidhaa za China kutoka katika vituo vyao vya viwanda mashariki mwa China hadi kaskazini mwa Pakistan njiani kuelekea Bandari ya Gwadar, ikizingatiwa kuwa mradi huu ni mkondo muhimu mno wa kiuchumi ambao China imewekeza mabilioni ya dolari katika miaka ya hivi karibuni. Hivyo basi, mzozo huu hauko huru na kipimo hiki katika mtazamo wa Wachina. Endapo China itataka kufungua mzozo mwengine wa mpaka kati yake na India (mipaka ya mashariki) juu ya jimbo la Arunachal Pradesh, manufaa ya "mikondo ya kiuchumi" ambayo inayatafuta ndani ya muundo wa mkakati wa Barabara ya Silk, kwa kuepuka kupitia katika maeneo yanayo dhibitiwa na Majeshi ya Majini ya Amerika, hususan Eneo la Malaga, hayangepatikana. Kinacho ongeza shauku ya China kwamba India inatekeleza sera ya Amerika kuzuia kuinuka kwa China ni yafuatayo:

1- Baada ya janga la maambukizi ya virusi vya Korona, Amerika ilipata hoja mpya ya kuishambulia China chini ya visingizio kadha wa kadha. Washington inazungumzia sana kuhusu haja ya Beijing kuwajibika kwa ajili ya kuenea kwa virusi hivi, na inaziburuza pamoja nayo nchi nyengine ikiwemo India katika mwelekeo wa kutaka uchunguzi hususan katika Taasisi ya Virusi ya Wuhan. Kwa upande mwengine, kukatizwa kwa baadhi ya bidhaa kutoka China wakati virusi viliposhambulia kwa mara ya kwanza na uzalishaji ukaathiri viwanda vingi vya Ulaya na vya kimataifa kutokana na kukatizwa kwa mtiririko wa vipuri kutoka China ikisababisha matakwa ya kuachana na mtiririko wa bidhaa zinazopitia China, na kwa sababu ya mtindo huu, ambao umeongezea na juhudi za Raisi wa Amerika kuzirudisha kampuni za Kiamerika zinazo endesha shughuli zake nchini China, au hata kuzitoa nje ya China, Beijing sasa inahisi hisia ambayo haijawahi kuihisi ya uchumi wake kuwa chini ya tishio na shinikizo halisi. 

2- Kinachoashiria pia kuhusika kwa India katika siasa za Amerika ni jaribio lake la kuudhoofisha uchumi wa China: (Jenerali Vinod Bhatia, meneja mkuu wa zamani wa operesheni za kijeshi nchini India, anaiambia Anatolia kwamba China, kiulimwengu, inapoteza "ushawishi" wake katika kuamini kuwa ndiyo chanzo cha janga la maambukizi ya virusi vya Korona.) Aliongeza: "Kampuni za utengezaji zinaangalia namna ya kuondoka China; hii inailazimisha Beijing kujaribu kuleta ubabaishaji kutokana na janga la virusi vya Korona." Alidokeza kuwa ulimwengu baada ya Korona "utakuwa ni fursa kubwa kwa India…" (Anatolia ya Uturuki, 9/6/2020). Inaonekana kana kwamba fursa hii ambayo Wahindi wanaizungumzia ni uhamishaji wa kampuni za kigeni, hususan zile za Kiamerika, kutoka China hadi India. China inashuhudia kwamba Amerika iko nyuma ya kuimarika kwa uwezo wa India wa kuiwezesha kukabiliana na China, kwa kusaidia mradi wake wa nuklia mpaka India sasa imekuwa ni nchi ya kinuklia, ikiipa wadhifa wa kipekee na kipaumbele katika biashara na mahusiano ya kiuchumi, pamoja na kuilazimisha Pakistan kupunguza taharuki na India, na kuiruhusu India kuendesha sekta kubwa kubwa za kijeshi ambazo kwa miongo kadha zilikuwepo katika mipaka yake na Pakistan na sasa kuzipeleka katika mipaka yake na China. Sera hii sio mpya kwa Amerika kwa India, bali ni ya miaka mingi, na leo Amerika inaongezea ndani yake kwa kuihusisha India katika kuzitoa kampuni kubwa za kigeni nchini China, na kuifanya India kuwa badali yake, yaani kuihusisha katika kuushambulia uchumi wa China.

3- Ni muhimu kutambua kwamba kwa upande wa mtazamo wa kijeshi, China imeweza kuimarisha pakubwa jeshi lake, na imekuwa ni nchi ya pili kiulimwengu baada ya Amerika katika utumiaji kwa ajili ya jeshi huku bajeti ya kijeshi ya mwaka 2019 ikiwa ni dolari bilioni 261, bali inatumia zaidi ya Urusi, Uingereza na Ufaransa zikiunganishwa pamoja. Ingawa India katika mwaka wa 2019, ilikuwa nchi ya tatu baada ya China katika upande wa utumiaji kwa jeshi, kwa mara ya kwanza ikiwa na bajeti ya $ 72 bilioni, bado uwezo wa jeshi lake ungali mdogo ukilinganishwa na uwezo wa kijeshi wa Jeshi la Kitaifa la China. Jambo hili la uwezo wa kijeshi wa majeshi hayo mawili linaifanya India kuchukua tahadhari ya kutangaza vita vipana na China, kinyume na ilivyokuwa mnamo 1962.  Yote haya ni licha ya kuwa India ina manufaa makubwa katika silaha za kawaida katika eneo la mzozo wa hivi karibuni la Ladakh, hususan kwa kuwa sekta nyingi za jeshi lake ziko katika mipaka yake na Pakistan, yaani karibu na eneo la mzozo, kinyume na China, ambayo majeshi yake bado hayajakuwa katika eneo hilo, na uhalisia huu kuhusiana na uwezo wa kawaida wa kijeshi wa nchi zote mbili katika eneo la mzozo umethibitishwa na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Amerika cha Harvard… (Arabic Post 31/5/2020). Lakini, inaonekana baada ya ghasia hizi kwamba China imekuwa ikiyapeleka majeshi ya ziada katika eneo hili na kuongeza uwezo wake wa kijeshi dhidi ya India katika mipaka ya magharibi.

4- Na ikiwa mzozo wa India mnamo 2017 katika mpaka wa mashariki ulitatuliwa, kwa mkutano wa Waziri Mkuu Narendra Modi na Raisi wa China Xi Jinping mnamo 2018 [viongozi hawa wawili walifanya mkutano wao wa kwanza usio rasmi jijini Wuhan mnamo Aprili 2018 na wakati wa mkutano huu Xi alikubali mwaliko wa Modi kuzuri India kwa mkutano wa pili (Euro Arab News, 9/12/2019)], lakini mzozo wa sasa unasadifiana na juhudi maradufu za Amerika za kuihujumu China, zinazo sababisha matatizo zaidi na kufanya utatuzi wa mzozo huu kuwa vigumu zaidi. Matatizo haya mapya ambayo utawala wa Trump unayasababisha kwa China yanafahamika kikamilifu jijini Beijing, hivyo [Raisi wa China Xi Jinping alisema leo, Jumanne, "Beijing itakoleza matayarisho yake kwa ajili ya mapambano ya kijeshi na kuimarisha uwezo wake wa kutekeleza misheni za kijeshi, chini ya athari kubwa ya janga la maambukizi ya Korona katika Usalama wa Taifa." (Sputnik, Russia, 26/5/2020)].

Taarifa hii ya China, ingawa kidhati haiikusudii India, lakini Beijing, inahisi hatari kubwa inayoizunguka baada ya kuzitazama nia za Amerika za kuitaka iwajibike kutokana na kuenea kwa virusi vya Korona, hivyo China huenda ikatafakari na kupanga kuonyesha uwezo wake wa kijeshi ili kuzuia mpango wowote wa kijeshi wa Amerika dhidi yake ambapo unajumuisha washirika wa Amerika katika eneo hilo ikiwemo India. Kana kwamba inatuma ujumbe kwa maadui wake wa karibu kutoshirikiana na Amerika, la sivyo jeshi la China linauwezo wa kuleta madhara juu yao. Pengine ripoti ya ujasusi iliyotolewa na Wizara ya Usalama wa Dola nchini China mwanzoni mwa Aprili 2020 iliyoitaka Beijing kujitayarisha kwa makabiliano ya kijeshi inafichua umuhimu wa mipango ya Amerika dhidi ya China. Na ongezeko la matumizi katika jeshi la India, yakifikia hadi dolari bilioni 72 kwa mara ya kwanza mnamo 2019. Na mpango mkubwa wa silaha uliokamilishwa na jeshi la India, yote haya yanaweka tishio la moja kwa moja kwa China, na imekinai kwamba India,inawakilisha kichwa cha mkuki wa Amerika dhidi yake na miradi ya miundomsingi inayofanywa na India katika maeneo ya mpakani inayozozania na China, ikiongezewa na kuharakishwa kwa matayarisho yake ya kijeshi, yanaongeza wasiwasi nchini China kuhusu mustakbali wa mahusiano yake na India.

Tano: Ama msimamo wa Amerika juu ya mzozo wa hivi karibuni kati ya India na China, bila shaka ilikuwa inaiunga mkono India. Balozi Alice Wells, Naibu Mkuu wa Waziri Msaidizi wa Maswala ya Asia Kusini katika Wizara ya Kigeni ya Amerika, alikashifu vitendo vya China eneo la Ladakh na kuvihusisha na uchochezi wa Beijing katika Bahari ya China Kusini. (NEWS 18, 21/5/2020). Mwakilishi Eliot L. Engel, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Kigeni, alitoa taarifa akisema: "Nina wasiwasi mno na uchokozi unaoendela wa China katika Mstari Halisi wa Udhibiti katika mpaka wa India na China. China inaonyesha kwa mara nyengine tena iko tayari kuwahangaisha majirani zake kuliko kutatua mizozo kwa mujibu wa sheria ya kimataifa… Naisihi China kwa dhati kuheshimu tamaduni na kutumia diplomasia na utaratibu uliowekwa ili kutatua maswala yake ya mipaka na India." (American Foreign Affairs, 1/6/2020).

Hii ni kuongezea ukweli kwamba Amerika inajaribu kupatiliza fursa ya mizozo hii ya mipaka na kuitumia kama karata ya Trump mikononi mwake dhidi ya China ili kuishinikiza kuhusiana na sera yake, katika kudhibiti upenyaji wa ushawishi wake eneo hilo na kuishughulisha katika ghasia hizi, na kuisaliti katika vita vya kibiashara na uingiliaji wa mambo ya China. Hiyo ndio sababu Raisi wake, Trump, ametoa ofa ya kuzipatanisha India na China baada ya kuzuka kwa mzozo wa hivi karibuni baina yao, ili kuyadhibiti masuluhisho baina ya pande hizi mbili kwa manufaa yake, mnamo 27/5/2020 aliandika katika ukurasa wake wa Twitter: "Tumeiarifu India pamoja na China kuwa Amerika iko tayari, inataka na inaweza kuwapatanisha au kutoa uamuzi kwa mzozo mkali wa sasa wa mpaka". (Al-Hurra, 27/5/2020), ambapo China iliikata ofa hii, kama alivyo sema msemaji wa Wizara ya Kigeni ya China Lijian Zhao kuwa nchi mbili hizo hazitaki mtu wa tatu wa "kuingilia" kutatua tofauti zao. (Anatolia, Uturuki, 9/6/2020)].

Sita: Licha ya kuwa, Amerika haikutulia, bali iliendelea na amali yake katika eneo hilo ambalo inalichukulia kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi duniani, na kitendo chake cha kukabiliana na China kiliendela kuanzia chini hadi kufikia majaribio ya kukabiliana nayo kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja katika Bahari ya China Kusini. Lakini Amerika haiwezi tena kutekeleza vita kila mahali na kuhifadhi ushawishi wake mpana katika maeneo mingi ya ulimwengu isipokuwa kwa kutegemea dola za kikanda na kieneo ambazo inafaulu kuzipata kufanya kazi nazo. Kisha likaja janga la Korona kuifichua Amerika; kuwa sio dola inayo weza kufaulu kulidhibiti janga linaloikumba, bali imefichuliwa kama iliyo feli na dhaifu mbele ya kirusi! Na hili lilichochewa baada ya kadhia ya ubaguzi wa rangi kuzuka ndani yake baada ya polisi mmoja Mwamerika mweupe kumziba pumzi raia mmoja mweusi wa Amerika, jambo lililoifichua kimataifa… katika wakati ambao China ni dola kuu ya eneo. Hivyo basi, Amerika imekuwa sasa inategemea zaidi juu ya nchi zengine kuliko nyuma ili kunali maslahi yake na kudumisha ushawishi wake…

Amerika ilitafuta kuwaleta vibaraka wake nchini India mamlakani, ili India iwe chini ya amri yake, na kwamba Amerika inadhamini kuwa matokeo yake daima itakuwa upande wake, na kwamba vibaraka wake wataifuata. Inafanya kazi kwa nguvu zake zote kukileta Chama cha Bharatiya Janata (BJP) mamlakani, hivyo chama hiki kilicho tiifu kwa Amerika kiliwasili kwa mara ya kwanza chini ya uraisi wa Vajpayee kuitawala India mnamo 1998 hadi 2004. Ambapo uchaguzi ulifanyika katika mwaka huo, kilipoteza nafasi yake kwa Chama cha Congress, na kurudi tena na kushinda mnamo 2014 na kingali mamlakani.  Amerika ilianza kuitumia India dhidi ya China, na ili kuiruhusu India icheze dori hii, Amerika iliizima Pakistan na kuifanya ikae mbali na mzozo wake na India ili India ijitolee katika mzozo wake wa hivi karibuni na China. Hii ndio sababu watawala wa Pakistan waliitupilia mbali Kashmir pindi India ilipo tangaza mwaka jana mnamo 5/8/2019 kuwa Kashmir iliyo kaliwa imekuwa ni sehemu ya India, na tulitaja katika jibu la swali la tarehe 18/8/2019: (Marekani iliona kuwa taharuki juu ya Kashmir baina ya India na Pakistan zinaathiri kudhoofika kwa makabiliano ya bara Hindi dhidi ya Uchina… Ili kumaliza taharuki hizi Marekani ilianza mchakato wa upatanishi baina ya India na Pakistan, na lengo la upatanishi lilikuwa ni kuzima vita baina ya majeshi ya India na Pakistan kwa sababu ya Kashmir, na kuelekeza juhudi katika ushirikiano pamoja na Marekani hatimaye kuzuia kuinuka kwa Uchina. Marekani iliamini kuunganishwa kwa Kashmir na India na shinikizo la Marekani juu ya serikali nchini Pakistan ili kuizuia kutokana na amali ya kijeshi na kuhamisha mada ya mazungumzo kutatua kadhia hiyo na kuzuia mzozo wa kijeshi baina yao, kama vile mamlaka ya Abbas nchini Palestina na biladi za Kiarabu pambizoni mwao kutochukua hatua ya kijeshi dhidi ya umbile la Kiyahudi linaloikalia na kudai chochote linalotaka kwa Palestina!)  

Na watawala wa Pakistan wamejitolea kwa hili, na wametangaza, kama alivyo eleza Waziri Mkuu Imran Khan, aliposema: "Serikali yake itaijibu vilivyo serikali ya India endapo itaanzisha shambulizi kwa Pakistan." (Anatolia, 30/8/2019). Yaani, sio kwa ukombozi wa Kashmir! Baada ya takriban mwezi mmoja, alisema, ["Kamanda wa Jeshi Bajwa amemhakikishia kuwa jeshi la Pakistan liko tayari kukabiliana na India, endapo itaanzisha shambulizi kwa Kashmir iliyo kombolewa…" (Pakistani Geo News Channel 26/12/2019)], ikimaanisha kuwa Azad Kashmir haipaswi kuikomboa Jammu na Kashmir kutoka kwa udhibiti wa India!

Saba: Ama Pakistan, inayo dumisha mahusiano imara na China, kamwe haitaki haki zozote katika eneo la Aksai Chin ambalo China imelikalia kutoka India, ambalo ni sehemu ya Kashmir, wala haitaki haki zozote eneo la Kashmir la Ladakh lililo chini ya udhibiti wa India ambalo China inataka sehemu yake! Na Pakistan, ambayo inatumiwa kuonyesha kupendezwa kwake na mizozo ya India pamoja na China, ikizingatiwa kuwa China itavunja pua ya India, adui mkubwa wa Pakistan, lakini, wakati huu imekuwa kimya. CNN News-18, mnamo 26/5/2020 ilishangazwa na kimya hiki, ambapo pia ilijumuisha vyombo vya habari vya Pakistan, na haikueleza msimamo wake juu ya mzozo huu kama ilivyo kawaida. Hili haliwezekani isipokuwa kutokana na shinikizo la Amerika, kwa sababu Amerika inataka India ijihisi vizuri katika mahusiano yake na Pakistan, na isihisi tishio lolote, kama vile jeshi la Pakistan kusubiri kuishambulia endapo itaingia vitani na China. Yote haya ni kuifanya India kutekeleza uhamishaji wa majeshi yake zaidi kutoka katika mipaka yake na Pakistan hadi katika mipaka yake na China, ili iwe katika nafasi nzuri ya kutia shinikizo kwa China, na kutawanya nguvu za jeshi la China badala ya kuzikusanya katika eneo la Bahari ya China, na hili litaidhoofisha China hata bila ya vita wakati rasilimali zake za kijeshi zitakapo gawanywa kati ya kujitayarisha kukabiliana na India kusini magharibi na kujitayarisha kukabiliana na maadui wakuu baharini. Majeshi ya Maji ya Amerika na Jeshi la Japan ambalo pia linaongezea nguvu yao dhidi ya China.  

Nane: Kwa yote haya, Waislamu wa Kashmir wanahisi kuwa ardhi za eneo lao zimekuwa mada ya mzozo baina ya dola mbili za kikafiri, kila moja inataka kuzifuja na kuzidhibiti, katika wakati ambapo watawala wa Pakistan na watawala wengine wa Waislamu wamesimama pasi na kuchukua hatua yoyote. Pakistan hata imeyaandama makundi ya kisilaha ya Kashmir katika ardhi zake ili kuyazuia kuidhuru India. Uhalisia huu wa Pakistan na mzozo kati ya China na India unawadhoofisha pakubwa Waislamu wa Kashmir. Baada ya Kashmir kuwa katika makabiliano na uvamizi wa India, na kusaidiwa pakubwa na jeshi la Pakistan, leo inajipata ikikabiliana na nchi mbili kuu pasi na usaidizi wowote kutoka Pakistan, ambayo inaachana zaidi na viwanja vya mizozo na India kwa kuitumikia Amerika!!   

Inauma sana kwamba mzozo kati ya India na China ni juu ya ugavi wa maeneo ya Kiislamu, hususan Kashmir na viunga vyake; India inataka kurudishiwa ardhi zilizochukuliwa na China katika vita vya 1962, katika mpaka wa magharibi, ambalo ni eneo la Aksai Chin la jimbo la Kashmir ya Kiislamu, na China inataka sehemu ya eneo la Kashmir la Ladakh linalopakana na eneo la Aksai Chin, na kudai haki zake katika maeneo hayo kwa sababu ni sehemu ya jimbo la Xinjiang, yaani eneo la Kiislamu la Turkestan Mashariki. Nchi hizi mbili zinapigania haki katika maeneo haya ya Kiislamu, huku Pakistan ikitekeleza utumwa kwa Amerika na Waislamu wengine wakinyamaza kimya! Maisha ya Waislamu yako katika matatizo yao na chumo lao ni duni kwa sababu ya yale ambayo ardhi zao zimevuna, na Mwenyezi Mungu (swt) ni Mkweli, Mwenye Nguvu na Hodari:

[وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنْكاً وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَى * قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَى وَقَدْ كُنْتُ بَصِيراً * قَالَ كَذَلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا وَكَذَلِكَ الْيَوْمَ تُنْسَى]

“Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu. Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona? (Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa.” [Ta-Ha: 124-126].

Hivyo basi, ukombozi wenu uko hapa, Enyi Waislamu: katika kufuata ayah za Mwenyezi Mungu (swt), na Hadith za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kupitia kusimamisha utawala wa Mwenyezi Mungu, Khilafah Rashidah, kwani ndio njia ya uongofu na Jihad, njia ya utukufu, nguvu na ulinzi kutokana na uovu, na Mtume mkweli wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema katika Hadith, iliyo pokewa na Bukhari na Muslim, kutoka kwa Abu Hurairah, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe pamoja naye kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«الْإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ»

“Hakika Imam ni Ngao, watu hupigana nyuma yake na hujilinda kwayo.” Hivyo chukueni tahadhari Enyi Watu wenye macho.

30 Shawwal 1441 H

21/6/2020 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu