Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu la Swali:

Kafara ya Kuvunja Kiapo (Kafarat ul-Yameen)
Kwa: Гаджимурад Гамзатов
(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Sheikh wetu muheshimiwa,

Je, kafara ya kuvunja kiapo (kafarat ul-yameen) inaweza kupewa mtoto mchanga ambaye hali chakula anakunywa tu maziwa ya mama pekee au maziwa ya unga ya watoto wachanga? Iwapo kafara imetolewa na mtu akasahau kuhusu hali hii (imepewa mtoto mchanga), je mtu huyo anapaswa kurudia kutoa kafara kwa masikini?

Na swali jengine linalohusiana na kafara ya kuvunja kiapo: Je, inatosha kumlisha masikini mara moja, au ni lazima kumlisha mara mbili (chakula cha mchana na jioni?)

Na swali la tatu: mtu anayeishi barani Ulaya na akatoa kafara ya kiapo kwa maskini nchini Ukraine kwa kufuata kiasi cha kafara ya kiapo nchini Ukraine. Je, ilikuwa ni lazima kwake kufuata kiasi cha kafara barani Ulaya, au ilitosha kufuata kiasi katika nchi iliyotumwa?

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

1- Kanuni msingi kuhusiana na kafara ya kiapo (kafarat ul yameen) ni maneno ya Mwenyezi Mungu (swt):

[لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَكِنْ يُؤَاخِذُكُمْ بِمَا عَقَّدْتُمُ الْأَيْمَانَ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ فَمَنْ لَمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ذَلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ]

“Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru.” [Al-Ma’idah: 89]. Kuwalisha masikini kumi ni mojawapo ya machaguo yaliyotajwa katika ayah hii:

[فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ] “Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu” [Al-Ma’idah: 89].

2- Inaeleweka kutokana na aya hiyo tukufu kwamba idadi ya kumi ni ya kulazimisha, yaani, masikini kumi lazima walishwe, hivyo sio sahihi kulisha maskini mmoja mara kumi, kwa mfano. Tumefafanua hili hapo awali katika Jibu la Swali la tarehe 29/4/2022 M, ambapo yafuatayo yalielezwa:

[na rai ambayo naoina kuwa sahihi zaidi ni kwamba ikiwa maandiko yametajwa na idadi fulani ya watu masikini, kama vile

[فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ] “Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu au kuwavisha [Al-Ma’ida: 89]

[فَمَنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَإِطْعَامُ سِتِّينَ مِسْكِيناً] “...Na asiye weza hayo basi awalishe masikini sitini.” [Al-Mujadila: 4]. Katika hali hii, idadi iliyotajwa hapo juu (kumi, sita) ni lazima izingatiwe, iwe utoaji ni wa aina au wa thamani, kwa sababu nambari ndio iliyo dhamiriwa, ni ufungaji wa lazima, lakini ikiwa andiko linahitaji kuwapa masikini pasi na kutaja idadi, inaruhusiwa kumpa masikini mmoja kwa sababu hakuna ufungaji wa idadi, na pia yaweza kupeanwa kwa zaidi ya masikini mmoja, kama alivyo sema Mwenyezi Mungu (swt) kuhusiana na zaka:

[إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ]

“Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.” [At-Tawba: 60]. Kwa hivyo inajuzu kwa mwenye kutoa Zaka kumpa masikini mmoja, na inajuzu kuigawanya kwa masikini wengi, kwa sababu hakuna idadi maalum katika Aya, bali neno "masikini" limetajwa namna hiyo bila ya idadi... Lakini anazingatia tu kwamba wanastahiki kupewa zaka kwa sababu wamesifiwa kuwa ni masikini.]

3- Kwa hiyo, kukamilika kwa kafara kunahitaji kuwalisha masikini kumi chakula cha wastani, na hii ina maana kwamba masikini anayepewa kafara ndiye anayeweza kula chakula cha wastani. Ama mtoto anayenyonyeshwa sidhani kuwa amejumuishwa katika fahamu hii, na kwa hivyo hahesabiwi miongoni mwa masikini wanaolishwa katika kafara ya kiapo. Ikiwa mtu alisimama na kupeleka chakula kwa familia maskini yenye watu kumi, akiwemo mtoto mchanga, basi kafara hii haijakamilika; ni sawa na kulisha watu tisa na sio kumi, kwa sababu mtoto hawi chini ya fahamu ya wale wanaolishwa. Hii ndiyo ninayoiona kuwa sahihi zaidi na ndiyo ninayoridhika nayo. Kwa hiyo, ni lazima akamilishe kwa kumlisha masikini mwingine pamoja na wale aliowalisha ili kukamilisha kafara ya masikini kumi. Hii ni tofauti na mtoto anayekula chakula, kama vile mvulana mwenye akili razini na mfano wake, kwani hawa wanahesabiwa katika kafara. Ikiwa katika familia masikini walikuwepo watoto kama hawa, basi kafara ni halali kwa kuwalisha, kwa sababu wanaingia katika fahamu ya wale wanaolishwa.

4- Mafakihi wamekhitilafiana katika kupambanua kiasi cha chakula kwa kila masikini katika kafara ya kuvunja kiapo (kafarat ul yameen), na katika aina ya chakula kinachotolewa kafara n.k. Encyclopedia ya Fiqh ya Kuwait

[“Pili: Kuhusu kiasi”

- Maliki, Shafi'i na Hanbali wana rai kwamba ni sharti kwamba kila masikini apewe kibaba (mudd) moja (kipimo cha uzito) kutoka katika sehemu ya chakula cha nchi kinacholiwa zaidi, na hairuhusiwi kutoa thamani ya chakula kulingana na andiko la aya:

[فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ] “Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi” [Al-Ma’idah: 89]. Ni sharti kwamba hisa zisipunguzwe, kwa hivyo haijuzu kuwapa masikini ishirini vibaba (mudd) kumi; kwa kila mmoja wao nusu kibaba isipokuwa atimize kwa kumi hao kile kilichopungua. Vile vile inatakikana ulishaji uwe kwa watu kumi, kwa hivyo uzushi haufai, hivyo ikiwa alilisha watano na akavisha tano, haijuzu. Vile vile inatakiwa kibaba kitolewe kwa kila mmoja katika watu kumi kwa msingi wa umiliki, na hairuhusiwi kwa mujibu wa madh’hab ya Malik kurudia kumpa mmoja. Mahanafi wana rai kwamba ni sharti kwamba kila masikini apewe nusu pishi (saa') (kipimo cha uzito) ya ngano, au pishi ya tende au mawele, au thamani ya hizo kwa pesa au ofa biashara, kwa sababu lengo ni kulipa hitaji, na hilo linaweza kufikiwa kwa thamani.

Ama kiasi cha chakula kinachoruhusiwa kwao: milo miwili yenye shibe, yaani, inatakiwa kila masikini apate chakula cha mchana na cha jioni, na vivyo hivyo akiwapa chakula cha jioni na suhur, au awape chakula cha mchana mara mbili na kadhalika, kwa sababu ni milo miwili iliyokusudiwa.

Lakini akimpa mtu mmoja chakula cha mchana na mwingine chakula cha jioni moja, hiyo si halali, kwa sababu atakuwa amegawanya chakula cha wale kumi kuwa ishirini, jambo ambalo si sahihi.

Vile vile wameweka sharti kwamba asitoe kafara yote kwa masikini mmoja kwa siku moja mara moja au tofauti kwa zaidi ya mara kumi. Lakini ikiwa alimlisha masikini mmoja kwa siku kumi, chakula cha mchana na cha jioni, au akampa masikini mmoja siku kumi kila siku nusu pishi, hiyo inajuzu kwa sababu hitaji linafanywa upya kila siku na kumfanya mithili ya masikini mwengine, kana kwamba alitumia thamani hiyo kwa watu kumi maskini.

"Tatu: Kuhusu aina"

- Hanafi wana rai kwamba kinachotosheleza katika kulisha ni ngano, au mawele, au tende, unga wa kila moja ya hizo ni mithili ya asili yake kwa kipimo, yaani, nusu pishi katika unga wa ngano na pishi katika unga wa mawele na ikasemwa: Kinachozingatiwa katika unga ni thamani, sio kipimo, na inajuzu kuvua thamani kutoka kwa aina zisizokuwa hizi. Maliki walikwenda kwenye ukweli kwamba kulisha ni kutokana na ngano ikiwa wameila, kwa hivyo haikubaliki kutoka kwa mawele au mahindi au nafaka nyinginezo. Ikiwa walikula isiyokuwa ngano, basi kilicho sawa nayo ni kushiba, na sio kipimo (kinachotolewa). Shafii wana rai kwamba kulisha ni kutokana na nafaka na matunda ambayo zakat inastahili kutolewa, kwa sababu miili huimarishwa nazo, na inatakiwa iwe kutoka kwa wingi wa chakula cha nchi. Hanbali walikwenda kuweka sharti kwamba kulisha kunapaswa kuwe kutokana na ngano, mawele na unga wao, tende na zabibu kavu, na hakuna kitu chengine chochote kinachoruhusiwa, hata kama ni chakula cha nchi yake, isipokuwa kiwa vyakula hivyo havipatikani.] Mwisho.

5- Ninachokiona kuwa sahihi zaidi kuhusiana na kulisha masikini kumi ni kwamba wanapewa milo miwili ili iwe maana ya kweli ya Aya:

[فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ]

Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu [Al-Ma’idah: 89]. Kulisha familia ni mara mbili kwa siku, ili iweze kuitwa kulisha, kama vile chakula cha mchana na chakula cha jioni; Vyenginevyo, hajamaliza kulisha familia yake, na vile vile kuhusu masikini katika kafara, ni lazima awalishe mara mbili kwa siku mpaka kafara ikamilike, basi akitosheleza kwa chakula cha mchana bila chakula cha jioni, au kwa chakula cha jioni bila chakula cha mchana hii haikubaliki, na pia, Shariah imekifanya chakula katika Ramadhan kuwa milo miwili: chakula cha kabla ya alfajiri na cha futari, hivyo kulisha kamili ni kwavyo au mfano wake.

6- Ama kuhusu swali lako: (mtu anayeishi Ulaya na akatoa kafara ya kiapo kwa masikini wa Ukraine kwa kufuata kiasi cha kafara ya kiapo cha Ukraine. Je, ilikuwa ni lazima kwake kufuata kiasi cha kafara huko Ulaya, au ilitosha kufuata kiasi katika nchi ilikopelekwa?) jibu la hilo na kile nilicho na imini nacho ni kwamba kiasi kinachotumwa ni kulingana na wastani wa chakula katika nchi ambayo mtu anayepewa kafara inaishi, na hiyo ni kwa sababu Aya tukufu inasema:

[فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ]

Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu [Al-Ma’idah: 89]. Hili humfanya ahisi kuwa kulisha ni kulingana na mahali alipo mtu huyo, kwa sababu kinachotakiwa ni kuwalisha masikini kumi kutokana na wastani wa kile anacholisha familia yake. Ikiwa alilisha, kwa mfano, nchini Ukraine kwa dolari kumi, basi hizi zinaweza kutosha kulisha watu kumi masikini huko, lakini hazitoshi kulisha watu kumi masikini kulingana na hali ya Ulaya. Kwa mfano, anapaswa kulisha kwa dolari mia moja ili aweze kulisha kwa wastani wa kile anacholisha familia yake. Kwa hivyo, nadhani ni bora na busara zaidi kutoa kiasi cha kulisha watu kumi maskini katika nchi anayoishi.

Hili ndilo ninaloliona kuwa sahihi zaidi, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi, ni Mwenye hekima.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu