Jumanne, 24 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Katika Vita vya Urusi na Ukraine: Afrika Haipaswi Kumuunga Mkono Yeyote

Habari:

Vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine vinaonekana kuigawa Afrika juu ya kuunga mkono upande gani na kwa nini? Viongozi wengi wa Afrika wameamua kutofungamana na upande wowote huku wachache baadhi yao wakionesha wazi pande zao. Licha ya misimamo binafsi ya nchi, Umoja wa Afrika (AU) ulituhumu uvamizi wa Moscow na kutoa mwito wa kusitisha mapigano mara moja. Raisi wa Senegal Macky Sall ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahmat wanaitaka Urusi kuheshimu sheria za kimataifa na mamlaka huru ya nchi ya Ukraine.

Maoni:

Kama tukitazama pande mbili za mgogoro huu, yaani Urusi na Ukraine ambayo inaungwa mkono na Ulaya na Amerika, ni wazi kuwa hakuna anayepaswa kuungwa mkono. Vita halisi hapa ni kati ya Urusi upande mmoja, na Ulaya na Amerika hususan katika upande mwingine, huku Ulaya na Amerika ikiitumia Ukraine kama mbuzi wa kafara.

Kwa hivyo, ikiwa mjadala wetu utakuwa katika wahusika wakuu wa vita hii, yaani Urusi, Ulaya na Amerika, nukta zifuatazo za mjadala ni lazima zihusishwe ili tuweze kujua ni upande upi wa mgogoro au ni msimamo upi Afrika inatakiwa ichukue kuhusu vita hivi vinavyoendelea.

Nchi za Ulaya ambao wanaunga mkono Ukraine ili kudhibiti ushawishi wa Urusi hawana maana. Ni wanafiki, wenye historia ndefu ya uvamizi, ukatili, na umwagaji wa damu za Waafrika.

Walisababisha kupotea kwa watu milioni 100 na vifo milioni 12.5 katika Afrika katika kipindi cha utumwa kabla ya ukoloni wa kinguvu. Katika karne za biashara ya utumwa ya Kuvuka Atlantiki inakadiriwa takribani watu milioni 100 walitolewa katika makaazi yao (Dr Sheila S. Walker: Faces and Voices of the African Diaspora, USA, 2008). Katika kipindi hicho inakadiriwa Afrika ilikuwa na watu takribani milioni 62.2 mwaka 1500 na mwaka 1900 walikuwa karibu milioni 140.755,000 pekee.

Baada ya utumwa, nchi za Ulaya zilikoloni kwa mabavu Afrika na kuweka sera kandamizi za kimabavu za kufanyisha kazi na kodi, sheria kandamizi za udhibiti wa kumiliki ardhi na baadaye unyonyaji wa rasilimali uliochangia Afrika kudumaa kimaendeleo kwa Afrika huku wakilifanya Bara Ulaya kusonga mbele kwa  kiwango kikubwa.

Ulipokuja uhuru wa bendera, Ulaya na Amerika waliendelea kupambana kuigawa tena Afrika na kuendelea kulinda ushawishi wao kupitia ukoloni mamboleo.

Afrika ilikumbwa na mapinduzi na vita vingi vya wao kwa wao vilivyosababishwa na ushindani kati ya Ulaya na Amerika, kila mmoja wao akitaka kuweka kibaraka wake katika utawala.

Kupitia ukoloni mamboleo, Amerika na Ulaya waliitengeneza Afrika utegemezi kupitia Mfuko wa Fedha wa Kimataifa na Benki ya Dunia na kupitia biashara kwa mfumo usio wa haki kwa mbinu ya soko huria. Amerika na Ulaya wanatumia misaada na mikataba ya kilaghai ya kibiashara kama ‘ramba ramba tamu’ baina ya Afrika na nchi zao.

Kuhusu Urusi, ni kweli kuwa haikuwahi kulikoloni Bara la Afrika moja kwa moja, lakini katika kipindi cha zama za Usovieti ilisambaza kwa kulazimisha mfumo wake wa Ujamaa uliosababisha majanga mengi na umwagaji damu katika kusambazwa katika mchakato huo.

Kulikuwa na vita vingi vilivyopiganwa kwa niaba yao katika kipindi cha Vita Baridi kati ya Usovieti na Amerika, mfano Vita vya Ogaden nchini Somalia (1977-1978) na Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe nchini Angola (1975-2002) vikiwa na malengo ya kupanua wigo wa ushawishi wa Usovieti, ambavyo viliiathiri Afrika kwa kupelekea, vurugu mauaji na  kukosekana utangamano.

Kwa sasa Urusi inahuisha tena maslahi yake ndani ya Afrika si kwa ajili ya kueneza mfumo wake baada ya kushindwa mfumo wake wa Ujamaa dhidi ya ubepari, bali ni kwa ajili ya unyonyaji wa kiuchumi, kwani Urusi tayari imeshachukua mfumo wa ubepari.

Biashara ya silaha ya Urusi kwa Afrika na vifaa vya kijeshi inachukua zaidi ya asilimia 50 ya biashara yake na Afrika. Katika mkutano wa Sochi mwaka 2019, vifaa vya kijeshi vilitawala maonesho hayo.

Makampuni yenye uhusiano na Kremlin kama Gazprom, Alrosa, Rosatom na Rosneft yanahusika kuendesha migodi ya madini na nishati nchini Angola, Algeria, Ghana, DRC, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zimbabwe, nk. Biashara kati ya Urusi na Afrika ilifikia dolari bilioni 17.4 mwaka 2017.

Hivyo, washirika wa Ukraine yaani Ulaya na Amerika kwa upande mmoja, na Urusi upande mwingine, makundi yote mawili yana ajenda ya unyonyaji kwa Afrika.

Kulaani kwa nchi za Magharibi dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni wa kinafiki, na Afrika haipaswi kuunga mkono upande wowote. Unafiki mwingine wa wazi wa Wamagharibi ni kuhusu ubaguzi wa wakimbizi. Licha ya ukweli kuwa Urusi, Ulaya na Amerika ndio wanaotengeneza vita vingi katika Afrika, na kufaidika na vita hivyo na migogoro hiyo isiyokwisha, bali pia wamekuwa wakiwabagua kwa ukatili wahanga na wakimbizi kutoka Afrika kama ilivyo kwa wakimbizi kutoka Mashariki ya Kati. Imeripotiwa kuwa ndani ya robo ya kwanza ya mwaka 2021, zaidi ya nusu ya watu walioingia Italia kutokea Tunisia ambao wengi ni raia kutoka nchi za Afrika za Kusini mwa Jangwa la Sahara na kiasi cha wahamiaji 453 walikufa wakijaribu kuingia Ulaya kutokea Afrika Kaskazini kutokana na kuzuiwa, kubaguliwa na mazingira magumu wanayopata katika kuingia Ulaya.

Ummah wa Kiislamu katika Afrika unapaswa kutambua kuwa wote Ulaya, Amerika, Urusi na Ukraine wanahusika na umwagaji damu wa kaka zetu na dada zetu wa Kiislamu. Mifano ya karibuni  zaidi ni uvamizi wa Amerika  kwa Iraq wa mwaka 2003 uliopelekea vifo zaidi ya Waislamu milioni 1.2 vita ambavyo Amerika, Ulaya, ikiwemo na  Ukraine zilishiriki kwa kutuma zaidi ya wanajeshi 5,000  nchini Iraq.

Pia walivamia Afghanistan mwaka 2001 na kuua watu zaidi ya nusu milioni, Ukraine iliruhusu Amerika na Washirika wake kutumia anga na kambi zake za kijeshi pamoja na kutoa wanajeshi. Urusi pia haina tofauti na wenzake katika hili, imeua mamilioni ya Waislamu katika kipindi cha mfumo uliofeli wa Ujamaa. Nchi zote za Kiislamu zilizokuwa sehemu ya Umoja wa kiSovieti zilishuhudia mauaji ya kutisha, mateso, kufungwa kwa misikiti nk. Urusi imeuwa wengi Afghanistan na inaendelea na mauaji ya halaiki katika Syria, Libya nk. Bila ya kusahau namna inavyofunga Waislamu wanaolingania Uislamu. 

Kwa hivyo, kwa Waislamu popote walipo, kwa kuunga mkono Urusi ni kama kuunga mkono Ukraine, Ulaya na Amerika kwa sababu makundi yote mawili ni wauwaji wa kaka zetu na dada zetu.

Hali ya ushindani wa kimataifa kati ya Mabepari kama Amerika, Ulaya, Urusi na China juu ya mrundo wa rasilimali ya mafuta na madini ya Afrika inalazimisha hitajio la haraka la kurejeshwa kwa dola ya uadilifu ya Khilafah, ili kuliokoa bara hili na kuliinua juu ili kuwa na sauti na maamuzi huru katika kadhia za kimataifa.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu