Jumanne, 24 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kujiuzulu kwa Spika wa Bunge la Tanzania ni Dhihirisho la Ubatili na Kushindwa kwa Demokrasia

Habari:

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai mnamo tarehe 06/01/2022 alijiuzulu nafasi yake hiyo kufuatia ukosoaji wake wa karibuni wa wazi kwa Raisi kuhusu mikopo na ukuaji wa deni la taifa.

Maoni:

Mnamo tarehe 28/12/2021 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ambaye ni Spika wa 7 tangu uhuru alitoa kauli iliyohoji juu ya mwenendo wa mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa ambapo alidai kuwa Tanzania ipo katika hatari ya kupigwa mnada kutokana na kukua kwa deni la taifa.

Hivi karibuni Tanzania ilipata mkopo wa takriban dolari bilioni 3 ambapo dolari bilioni 2.29 ni kutoka Benki ya Dunia, dolari milioni 567 kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa na dolari milioni 256 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Ukosoaji wa Job Ndugai ulipokelewa kwa upinzani mkubwa hususan kutoka kwa maafisa wa chama chake tawala (CCM) na wabunge wenzake, jambo lililomfanya awali kuomba msamaha hadharani, lakini msamaha huo unaonekana kana kwamba haukukubaliwa. Siku chache baadaye, wakati Raisi Samia Suluhu Hassan akizungumza na Baraza la Mawaziri, wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa mikoa alitoa kauli nzito dhidi ya Ndugai kwa kusema:

Ni jambo lisiloingia akilini kwamba kiongozi wa mmoja wa muhimili wa dola adiriki kusimama na kusema aliyoyasema. Jambo hili hapana shaka ni kuhusiana na kadhia ya 2025 (uchaguzi mkuu)”  alisema Rais Hassan.

Katika hali kama hii, Spika Ndugai hakuwa na namna ila kujiuzulu.

Hapana shaka yoyote kauli ya Ndugai ilikuwa nzito na ya aina yake, na ni kauli ya kweli lakini kutoka kwa mtu mrongo. Kwa vile inafahamika vyema kuwa bajeti ya taifa na uidhinishaji wa mikopo unafanywa na Bunge ambalo Spika ana mamlaka nalo na ana ushawishi wa kuweza kuzuiya mikopo hiyo kupitia Bunge, lakini yeye pamoja na wabunge wenzake waliidhinisha uamuzi wa kukopa.

Zaidi ya hapo, Spika kama mkuu wa mojawapo wa muhimili wa dola alikuwa na nafasi  na uwezo wa kukutana na Raisi kibinafsi na kujadili kuhusu mwenendo wa mikopo.

Kwa yote haya inaonesha wazi kuwa Spika hana tofauti na wanasiasa wengine wa kidemokrasia ambao hujifanya kujali maslahi ya jamii lakini kiuhalisia wanacheza na akili za watu ili kufikia ajenda zao za kisiasa.

Tukio hili linatupa picha halisi kuwa dhana ya “uhuru wa kujieleza” katika demokrasia ni kauli mbiu bila ya ukweli, hutumika pale tu ambapo haigongani na kuathiri maslahi ya serikali na wanasiasa. Kwa hiyo, madai ya kuwa ni haki ya msingi ya wananchi kujieleza, kupata na kupewa taarifa zinazohusu maisha yao ipo mbali na ukweli.

Kwa upande mwingine, inaonesha wazi kutokuwepo kwa uhalisia wa mgawanyo wa madaraka na kujitegemea kwa mihilimli ya dola, yaani watendaji (serikali), Bunge na Mahakama. Madai haya ya uhuru na kujitegemea kwa mihimili yamebakia kuwa ndoto na kukosa uhalisia tangu kuasisiwa kwake na mwanafikra wa kifaransa Baron de Montesquieu mwaka 1748 mpaka leo hii.

Juu ya yote, demokrasia kutokana na kujengwa juu ya kipimo cha maslahi, daima itasababisha kutokuelewana, mivutano ya madaraka, vurumai na husuma miongoni mwa watu jumla na viranja wake ambao usiku na mchana wamo mbioni kwa uroho wa madaraka.

Nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na watu wote kiujumla wanapaswa kuzingatia ubatili na udhaifu wa mfumo wa kisiasa wa demokrasia kushindwa kutatua matatizo ya binadamu. Badala yake wanapaswa kufikiria kuhusu Uislamu ambao una mfumo mbadala wa uadilifu wa kisiasa katika kuwasimamia mambo yao na maisha yao na kuuokoa ubinadamu kutokamana na mazonge yote ya kisiasa na kiuchumi.

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu