Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ripoti ya Kadhia ya Hamza si ya Kuaminika, na Inadhihirisha Uwongo katika Kesi za Ugaidi Tanzania

Habari:

Mnamo tarehe 2 Septemba, 2021 Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Tanzania Bw. Camilius Wambura alitoa ripoti yake kuwa Hamza Mohamed (30) mfanyabiashara na mwanachama wa chama tawala (CCM) aliyeuawa na polisi siku ya tarehe 25 Agosti 2021 baada ya kuwaua askari watatu na mlinzi mmoja jijini Dar es Salaam kwamba alikuwa gaidi wa kujitoa muhanga.

Maoni:

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai bwana Wambura alidokeza kuwa uchunguzi wake zaidi ulijikita katika maeneo matatu: ambayo ni kufahamu utambulisho wa Hamza Mohamed, kilichompelekea kufanya mauaji, na ni kina nani anaoshirikiana nao.

Kuhusiana na utambulisho wa Hamza, uchunguzi umedai kubaini kuwa alikuwa akiishi maisha ya siri yaliyokuwa na viashiria vya ugaidi aliojifunza kupitia mitandaoni.

Kuhusu kilichompelekea kufanya mauaji yale, uchunguzi umeweka wazi kuwa alikuwa gaidi mwenye msimamo mkali wa kidini aliyekuwa tayari kuifia dini yake.

Ama ni kina nani anaoshirikiana nao, uchunguzi umeeleza kuwa Hamza alikuwa ana mawasiliana ya moja kwa moja na watu katika nchi zenye uwezekano na mafungamano na ugaidi, japo inafahamika wazi kuwa, watu watano  bado wanashikiliwa na polisi kuhusu suala hili.

Ripoti hii ya uchunguzi ni finyu, iliyokosa weledi na iliyoegemea upande mmoja, kwani taarifa zake zinapingana na uhalisia. Takriban watu wote waliohojiwa na vyombo vya habari kuhusu Hamza, Waislamu na wasiokuwa Waislamu, ndugu, marafiki, wanachama wenzake, wafanyakazi wake, majirani nk  walikuwa na jibu moja tu na mtazamo chanya kuwa Hamza alikuwa mtu mwema mwenye maadili mema ya dini ya Kiislamu. Venance Kalinga, jirani wa Hamza alinukuliwa akisema kuwa Hamza “ni mtu mwenye maadili anayefuata mafundisho ya Kiislamu, anapenda kwenda msikitini kila asubuhi, mchana na jioni” (Reuters 02/09/2021). Zaidi ya hayo yote Hamza alikuwa mfanyabiashara akijumuika na watu ikiwemo kuajiri wafanyakazi. Hivyo, maisha ya Hamza hayakuwa ya usirisiri na yasiyofahamika kama ilivyoripotiwa bali alifahamika na watu wengi waliotokea kuishi naye.

Dhana kwamba Hamza alijifunza ugaidi kupitia mtandao wa internet na mitandao ya kijamii haina msingi wowote na ni hoja iliyokosa uwazi, kwani ripoti imeshindwa kabisa kutaja ukurasa, tovuti au mitandao ipi ya kijamii aliyoitumia. Kiukweli nukta hii inaibua maswali mengi kuliko majibu, kwa mfano, vipi mtu anaweza kujifunza kwa mtandao kutungua kwa bunduki, na vipi angeweza kufanyia mazoezi ulengaji shabaha kupitia mitandao?  Na kama walilifahamu hilo, kwa nini hawakumzuiya? Kama Hamza alikuwa na viashiria vya ugaidi, vipi aliweza kuwa mwanachama mashuhuri wa chama tawala (CCM), bila ya kutaja kumiliki kwake silaha kisheria? Haya yote yanaonesha ripoti ni batili na haina uhalisia.

Kuhusiana na suala la kuwa eti msimamo mkali wa dini wa Hamza ndio uliomshawishi kufanya mauaji, hili pia halikinaishi, bali kimsingi limetumika kutusi dini ya Hamza ambayo ni Uislamu. Ni jambo lenye kufahamika wazi kuwa Uislamu hauruhusu mauaji ya watu wasio na hatia. Hivyo, ripoti hii ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ni jaribio la kuuchafua Uislamu na kamwe halikubaliki. Kiuhalisia ripoti imeshindwa kuonesha uhusiano kati ya dini ya Hamza na kile ilichokiita ugaidi. Hii inaonesha kuwa kujaribu kuunganisha baina ya dini ya Hamza na mauaji ya polisi ni jambo lisilo na msingi wowote.

Maelezo ya ripoti kuwa Hamza alikuwa na mawasiliano na watu katika nchi zenye uwezekano wa kuwa na ugaidi, kwa mara nyengine imeshindwa kutaja nchi mahsusi na watu hao. Hata hivyo, kwa jinsi propaganda chafu za vita dhidi ya ugaidi zilivyo duniani, suala la ugaidi lipo kila nchi. Je hili ndio limemtosha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuthibitisha madai ya ugaidi dhidi ya Hamza?

Ugaidi kama maarufu unavyotafsiriwa kimataifa kama matumizi yasio halali ya nguvu dhidi ya raia kufikia malengo fulani ya kisiasa. Kwa muktadha wa Hamza, ripoti imeshindwa kuelezea ni malengo gani ya kisiasa aliyotaka kuyafikia. Kinyume chake, kwa vile Hamza alikuwa mwanachama wa chama tawala (CCM) ni wazi kuwa alitumia njia ya kidemokrasia kufikia malengo yake ya kisiasa. Hili linatilia mkazo mtazamo wa wengi kuwa tukio hili la mauwaji halikuwa la ugaidi bali uhalifu wa kawaida.

Pia ripoti ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) inaonesha kukosa uaminifu kwa vile imepuuza maneno ya Hamza kabla ya kuuawa na Polisi tarehe 25 Agosti mwaka 2021 ambapo alitoa madai yake dhidi ya polisi hususan Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kwa kuhusika kwao katika kuuwa Waislamu. Suala la ukatili wa polisi, mauwaji, mateso, kunyakua, kudhalilisha Waislamu wasio na hatia nchini Tanzania linafahamika shahir dhahir, na hii ni mifano michache:

Mnamo tarehe 14/01/2006, Juma Ndugu, Muislamu, dereva wa teksi na wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro waliuawa kikatili katika msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (SP) Christopher Bageni. (Global Publisher 16/09/2016)

Kadhalika, mwezi Mei mwaka 2017, askari Polisi walimuua Salum Muhammad Almas aliyekuwa Imamu na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam kwa kumtuhumu tu na uporaji bila ya kuwa na ushahidi wowote.

Aidha, tarehe 21/07/2017, Polisi walivamia Waislamu wakiwa katika ibada katika Msikiti wa Ali Mchumo katika wilaya ya Kilwa na kuteka Waislamu 10. Baadaye baadhi waliripotiwa kufariki dunia na baadhi kupata ulemavu kutokana na mateso waliyopewa na Polisi. (Mwananchi 27/07/2017 & Mwananchi Digital 09/04/2018)

Kwa kuongeza, ikumbukwe kuwa ripoti ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ilinajisiwa awali kwa kuwa ilitanguliwa na msimamo wa IGP kuwa Hamza alikuwa na uhusiano na wapiganaji wa Msumbiji, na kuwa shambulizi lake linaweza kuhusika na ushiriki wa Tanzania katika mapigano nchini Msumbiji. Kauli hii ndio iliyochora sura ya matokeo ya uchunguzi wa ripoti ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Kwa kukhitimisha, ripoti ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai sio tu imejifedhehi wazi wazi kuwa iliegemea upande mmoja, bali pia imethibitisha uwongo juu ya kutokamilika kwa upelelezi dhidi ya Waislamu wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ameweza ndani ya wiki moja kufanya upelelezi na kugundua kuwa Hamza alikuwa gaidi licha ya mtuhumiwa kutokuwepo,  ilhali kuna mamia ya Waislamu wametuhimiwa kwa makosa ya ugaidi katika mikoa mingi nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Mtwara ambako wanaharakati watatu wa Hizb ut Tahrir Tanzania; Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso, Omar Salum Bumbo, na Waziri Omari Mkaliaganda wanashikiliwa kwa miaka minne sasa kwa makosa ya kubambikiwa ya ugaidi kwa kisingizio cha “upelelezi kutokamilika”.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu