Jumanne, 24 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Vita dhidi ya Virusi vya Korona Vimezalisha Kirusi Chengine cha Ufisadi na Kuunda Mamilionea wa Covid-19

Habari:

Maafisa wa upelelezi wa Kenya watapendekeza kushtakiwa kwa maafisa wakuu wasiopungua 15 wa serikali na wafanyibiashara juu ya madai ya matumizi mabaya ya mamilioni ya dolari yaliyokusudiwa kununua vifaa vya matibabu vya Covid-19. Awamu ya kwanza ya uchunguzi imejikita katika madai ya matumizi mabaya ya $7.8m zilizokusudiwa kununua vifaa vya dharura vya PPE kwa wafanyikazi wa huduma za afya na hospitali kote nchini. Wachunguzi kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini Kenya (EACC) wanasema matokeo ya awali yameonyesha kuwa sheria kadhaa juu ya ununuzi wa umma zilikiukwa wakati wa utoaji wa zabuni. Uchunguzi umethibitisha kosa la jinai kwa maafisa wa umma katika ununuzi na usambazaji wa bidhaa za dharura za Covid-19 katika Mamlaka ya Ugavi wa Vifaa vya Matibabu ya Kenya (Kemsa) ambayo ilipelekea matumizi mabaya ya fedha za umma. Awamu ya pili ya uchunguzi itazingatia kampuni ambazo zinadaiwa kufaidika na zabuni hizo, ingawa hakuna ishara kwamba yoyote katika kampuni hizo zilifuja fedha za Covid-19. (BBC)

Maoni:

Katika wakati mgumu ambapo mamilioni ya Wakenya maskini wanahimili mshtuko wa virusi vya Korona, ni wazi kama mwangaza wa mchana kwamba vita vyake vimeunda wale wanaoitwa mamilionea wa Covid-19, ambao wamefaidika na mikataba ya ulaghai. Mamilioni ya shilingi hazijafanyiwa uhasibu, fedha za Covid-19 ambazo zilipaswa kwenda kwa umma zimeenda kwenye akaunti za kibinafsi. Ni vigumu kuvuta taswira ya kiwango cha hatari ambazo watu wamehatarishwa nazo kutokana na ubinafsi na ulafi. Katika ufichuzi mwingine wa runinga NTV ulionyesha jinsi mabilioni ya shilingi yalivyotiririka kwa kampuni - katika ngazi zote za kitaifa na za kaunti - zilizopwa, kwa sakata ya vifaa ambapo imeunda mamilionea kadhaa wa Covid-19.

Ufisadi umeikumba Kenya kwa muda mrefu, ukikwamisha maendeleo yake, ukiongeza ukosefu wa usawa na kukandamiza uwezo wake wa kiuchumi. Zimwi hili ni la muda mrefu kama vilivyo vita vyenyewe vilivyoingizwa siasa ambapo kila kashfa mpya inapoibuka, maafisa wa serikali wanaohusishwa na kesi za ufisadi wamekuwa wakiachiliwa kwa dhamana na kesi hizo huchukua muda mrefu kukamilika na mwishowe hakuna mtu anayepatikana "na hatia kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi".

Ufisadi ni zimwi linalozila Serikali zote zilizofungwa kwa mfumo fisadi wa Urasilimali. Kwa maana nyengine, msingi wa ufisadi katika tawala hizi uko katika mfumo wa Kirasilimali unaotekelezwa kwa jamii. Mfumo huu umesheheni kuridhika kimada kama kigezo pekee maishani hivyo basi kusababisha jamii haswa maafisa wa serikali kuvutiwa na hamu ya kukusanya mali kupitia mipango ya kifisadi. Kwa kuwa Kenya inaukumbatia mfumo Kirasilimali ambao umeambukizwa na hamu kubwa ya kujilimbikizia utajiri kwa njia zote basi uporaji wa  hazina ya umma utaenea.

Ni Uislamu pekee ndio unaoweza kupambana na janga la ufisadi hivyo basi huwalaani wale wote wanaojihusisha na rushwa na ufisadi. Wajibu na jukumu la kupambana na ufisadi ni la pamoja kwa wote sio watu fulani au tume. Uislamu unamtaka kiongozi wa dola (Khalifah) kuchukua hatua yoyote kali dhidi ya afisa yeyote wa serikali anayehusika katika kupora mfuko wa umma bila kujali hadhi yake katika jamii. Kwa kuongezea, Khalifah hutekeleza Shariah inayoamua jinsi Dola inavyokusanya na kutumia rasilimali zake. Kwa karne kumi na tatu wakati Uislamu ulipotawala nusu ya ulimwengu, kashfa za kifedha zilikuwa nadra kama kulikuwepo na yoyote. Kwa sasa ni Khilafah pekee itakayosimamishwa tena kwa njia ya Utume, ndiyo itakayo angamiza hatari ya ufisadi na maovu mengine.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu