Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

  Harakati ya Kiislamu ya Taliban Kuchagua Moja ya Machaguo Mawili!
Na: Saifullah Mustanir*

(Imetafsiriwa)

Imekuwa karibu miezi miwili tangu Taliban ikamate udhibiti wa Kabul. Lakini, injini ambayo ilikuwa ikifanya maendeleo ya haraka katika uwanja wa kijeshi inaonekana kwenda kwa kujivuta sana katika jukwaa utawala kushughulikia maswala ya watu.

Katika mwezi mmoja uliopita, Taliban ilitangaza baraza la mawaziri la muda kwa kuufafanua mfumo huo kama "Imarati ya Kiislamu". Kutangaza kwa Taliban mfumo wao kama 'Imarati ya Kiislamu' ilipingwa na matamko na maazimio ya kikanda na kimataifa; lakini, hakuna nchi hata moja ambayo bado imechukua msimamo wowote mkali juu ya kurudi kwa Imarati.

Uendeshaji wa utawala wa Taliban haujaregea katika hali ya kawaida kwani shida ya kiuchumi inazidi kuwa mbaya kila uchao. Foleni ndefu nyuma ya mabenki, ambapo watu wanaruhusiwa kutoa tu $200 kwa wiki kutoka benki baada ya siku chache za kukabiliana na shida na umati wa watu, ni dhahiri wanazungumza juu ya hali ngumu ya kiuchumi. Ingawa sehemu ya tatizo ni urithi wa utawala uliopita, Taliban bado hawajaweza kupata utaratibu wa kushughulikia shida iliyopo.

Vyenginevyo, Kaimu Waziri wa Haki katika mkutano mmoja na Balozi wa China nchini Afghanistan amesema: "Katika kipindi cha mpito, Imirati ya Kiislamu ya Afghanistan ataitekeleza kivitendo Katiba ya Mohammad Zahir Shah, Mfalme wa zamani wa Afghanistan, kwa kuviondoa vile vifungu vyake ambavyo ni kinyume na Sharia na kanuni za Imarati ya Kiislamu.”

Lakini, tangazo kama hilo lilifuatwa na mawimbi ya kukatisha tamaa miongoni mwa watu wa Afghanistan, mtu hawezi kukataa shinikizo za kiulimwengu zinazoiathiri Taliban kuweka macho yao kwenye Katiba hiyo kama msingi. Uamuzi huu umesababisha upinzani kutoka kwa Taliban na kwingineko. Kuweka Katiba hii kama msingi, hata kwa kipindi cha muda mfupi, ni hatari sana na kunachochea kutoaminiana kwa sababu Katiba ya Zahir Shah sio zaidi ya sheria kisekula iliyoundwa na wanadamu ambayo iliidhinishwa kwa msingi wa kura za watu kupitia Loya Jirga. Kwa kweli, sheria hii, badala ya Sharia, imechukua uhalali kutoka kwa watu; na badala ya imani ya Kiislamu, imejengwa juu ya fikra za kisekula na vile vile kutenganisha Dini na maisha.

Kwa kitendo kama hicho, Taliban wanajaribu kuonyesha mwelekeo wao laini na tofauti kwa ulimwengu. Hawataki kutengwa kisiasa na kiuchumi kama vile walivyokuwa miaka ya 1990; kwa hivyo, wanajaribu kuingia katika uhusiano wa kirafiki na wenye manufaa pamoja na ulimwengu. Kama Abdul Ghani Baradar, naibu wa kwanza wa Waziri Mkuu wa Taliban, alivyosema wakati wa karamu na mabalozi na wanadiplomasia wa kigeni jijini Kabul:  "Imirati ya Kiislamu haina sera ya kudhuru nchi zengine za ulimwengu na inataka kuwa na uhusiano mzuri na zote." Alitoa wito kwa nchi za kigeni kufungua balozi zao jijini Kabul. "Tunataka kufungua sura mpya ya kisiasa ya utawala bora nyumbani na uhusiano na eneo na ulimwengu," Amir Khan Mottaqi, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje alisema. Taliban pia wamewahakikishia mabalozi wa kigeni kuwa usalama wao na wa raia wengine wa kigeni nchini Afghanistan utahakikishwa.

Misimamo hiyo laini inaonyesha wazi juhudi kubwa za Harakati ya Taliban kupata kutambuliwa kimataifa kwani hakuna nchi ambayo bado imeitambua Taliban, na Taliban wanajaribu kuvunja barafu. Hakika, ulimwengu umeanza mchezo wa sura mbili na Taliban. Kwa kuwa hawajaitambua Taliban wala hawajakata kabisa mafungamano yao na Taliban, wakikubali uhalali wa Taliban 'usio rasmi'. Kwa sasa, mabalozi na wawakilishi wakuu wa nchi 12 za kigeni wamo nchini Afghanistan. Kwa kuongezea, INGO's, chini ya pazia la kutoa misaada ya kibinadamu, wamekuwa wakijaribu kuanza tena shughuli zao kwa wiki kadhaa. Baadhi ya majirani wa Afghanistan wana uwezekano wa kuitambua serikali ya Taliban kutokana na maslahi ya kisiasa na kiuchumi, lakini nchi za Ulaya na Amerika hazina haraka ya kuitambua Taliban hivi karibuni. Lakini, misheni zao za kidiplomasia jijini Kabul na Doha zinafanya kazi kwa karibu na Taliban.

Nchi za Magharibi na majirani wa Afghanistan wanaonekana wamekuwa wakisisitiza juu ya haki za wanawake, haki za binadamu, na uundaji wa serikali ya mjumuiko kama sharti la kutambuliwa, lakini hizi ni zile pande zinazoonekana za hadithi hiyo. Kwa kweli, nchi za Magharibi na za eneo zinajaribu kuufunga ushindi wa kisiasa na kijeshi wa Taliban katika mipaka ya kitaifa kwa hivyo hawatafuata ajenda zaidi ya Afghanistan kwa sababu makamanda kadhaa wa jeshi la Taliban wako tayari kufanya hivyo. Suala jingine la wasiwasi ni uwepo wa wapiganaji wa kigeni nchini Afghanistan ili wasiwe tishio kwa nchi za eneo na Magharibi. Ingawa Taliban mara kadhaa wameonyesha wasiwasi huu kuwa sio wa kihakika, Magharibi bado ina shaka, ikizua mada ya uwezekano wa kurudi kwa al-Qaeda na vikundi vyengine vya waasi katika mwaka ujao.

Kilicho muhimu kwa Harakati ya Kiislamu ya Taliban kutambua ni kwamba idadi kubwa ya vikundi vya Kiislamu ulimwenguni vimeibuka washindi katika mapambano ya kijeshi, lakini wameshindwa katika siasa, utawala, na utekelezaji wa Uislamu. Kwa sababu kubadilisha mfumo na kuugeuza kuwa sura ya Kiislamu haifanyiki tu kwa kubadilisha nyuso [tawala] isipokuwa 1) msingi na imani ya mfumo huo zijengwe juu ya Uislamu, 2) mtawala ananyakua kiti cha enzi kupitia bay'ah na kuridhika kwa watu na 3) kwamba mtawala anatabikisha tu Uislamu pekee na kuubeba kwa mataifa mengine. Iwapo masharti haya matatu hayatatimizwa, mfumo unaoitwa kuwa wa Kiislamu utakumbwa ma maswali mazito. Kwa kweli, hali hizi zinaonekana kuwa zinakinzana na mahitaji ya Magharibi, zikizuia kupatikana kwa uhalali wa kimataifa.

Taliban pia wanajaribu kufanya mabadiliko ya Kiislamu hatua kwa hatua katika jamii wakati utabikishaji wa hatua kwa hatua wa hukmu za Sharia hauruhusiwi katika Uislamu. Kwa kuongezea, Taliban wana uwezo wa kutabikisha Uislamu kikamilifu katika maswala ya kimahakama, kiuchumi, kisiasa na maswala ya sera ya nje, badala ya kuregelea utekelezaji wa Uislam hatua kwa hatua.

Kwa sasa, Taliban wanakabiliwa na machaguo mawili makubwa ya kuchagua kutokana nayo: 1) kuanzisha mfumo safi wa Kiislamu kupitia kutabikisha na kuubeba Uislamu kwa wengine ili hatimaye kupata radhi za Mwenyezi Mungu (swt) au 2) kujifunga na mipaka ya kitaifa kwa kung'ang'ana kutambuliwa katika vikao vya kimataifa ili hatimaye kupata radhi za watu. Ikiwa Taliban itakwenda kwa chaguo la pili, wataelekea katika kifo cha taratibu.

«مَنِ الْتَمَسَ رِضَاءَ اللَّهِ بِسَخَطِ النَّاسِ كَفَاهُ اللَّهُ مُؤْنَةَ النَّاسِ، وَمَنِ الْتَمَسَ رِضَاءَ النَّاسِ بِسَخَطِ اللَّهِ وَكَلَهُ اللَّهُ إِلَى النَّاسِ»

“Yeyote anayetafuta radhi za Mwenyezi Mungu kupitia hasira za watu, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kutokana na maudhi ya watu, na yeyote anayetafuta radhi za watu kupitia hasira za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamwakilisha kwa watu.”

* Imeandikwa kwa Ajili ya Gazeti la Ar-Rayah – Toleo 360
* Mkurugenzi wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir katika Wilayah Afghanistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu